
Songwe. Wanawake wa Kijiji cha Kilimampimbi, Wilaya ya Mbozi mkoani Songwe, wametangaza kususia kubeba mimba na kuzaa kama njia ya kushinikiza Serikali kukamilisha ujenzi wa zahanati ya kijiji hicho uliokwama tangu mwaka 2014.
Uamuzi huo umetolewa mara kadhaa katika mikutano ya kijiji, ambapo wanawake hao wameeleza kuwa hawapo tayari kuendelea kubeba jukumu la uzazi huku wakikosa huduma za afya karibu na makazi yao.
Mwenyekiti wa kijiji hicho, Daud Mwalwanda, akizungumzia msimamo huo, amekiri kuwepo kwa tishio hilo na kusema kuwa malalamiko ya wanawake yamekuwa yakiwasilishwa mara kwa mara katika mikutano mbalimbali ya kijiji kwa muda mrefu.
“Bado hatuwezi kusema kama msimamo wao unaweza kufanya kazi, lakini mara kadhaa kwenye mikutano wamekuwa wakieleza hilo, ingawa inaweza ikawa ni kauli tu, bila kujali mazingira na uhalisia wake,” amefafanua Mwalwanda.
Amesema Kijiji cha Kilimampimbi chenye vitongoji vinne na wakazi 540 hakina kituo cha kutolea huduma za afya, hali inayowalazimu wananchi kutembea umbali mrefu kufuata huduma katika vijiji vya Msamba na Ikomela au hadi Hospitali ya Wilaya ya Mbozi.
Mariam Mtafya, mmoja wa wanawake wa kijiji hicho, akizungumza kijijini hapo, amesema uamuzi wao unatokana na mateso wanayopitia wanapohitaji huduma za uzazi.
“Tukienda kujifungulia katika zahanati ya kijiji jirani tumekuwa tukipewa maneno ya kebehi na karaha, sasa tumeamua kusimama kuzaa hadi tutakapopata huduma yetu hapa,” amesema Mariam.
Naye Francis Msyani, mkazi wa Kitongoji cha Kizonda katika kijiji hicho, amesema hali huwa ngumu kwa wajawazito hasa nyakati za masika, kwani hulazimika kujifungulia kwa wakunga wa jadi baada ya kushindwa kufikia huduma za uzazi katika vijiji jirani kutokana na barabara kutopitika wakati wa mvua.
Kwa upande wake, Mtendaji wa Kijiji hicho, Stewart Mtawa, akizungumzia sababu za kusuasua kwa mradi huo, amesema ni kweli ujenzi wa zahanati ulianza mwaka 2014 kwa nguvu za wananchi.
Ameeleza kuwa mwaka 2024, baada ya Serikali kubaini kuwapo kwa mkwamo huo, iliingilia kati na kutoa Sh50 milioni ambazo ziliwezesha kukamilika kwa zaidi ya asilimia 95 jengo la huduma za nje (OPD).
Hata hivyo, amesema zahanati hiyo imeshindwa kuanza kutoa huduma kwa sababu fedha zilizotolewa ziliambatana na maelekezo ya kuongeza miundombinu mingine, ikiwemo vyoo, jambo lililoongeza mzigo wa utekelezaji na kusababisha mradi kushindwa kukamilika hadi sasa.
Ameongeza kuwa changamoto nyingine inayokwamaisha mradi huo ni mfumo wa manunuzi, pamoja na baadhi ya wazabuni kususia kutoa vifaa na huduma katika halmashauri hiyo, hali iliyochangia kuchelewa kwa ukamilishaji wa mradi.
Katika kikao cha Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi kilichoketi kujadili taarifa ya utekelezaji wa robo ya pili ya mwaka wa fedha 2025/2026, madiwani waliibua malalamiko kuhusu miradi mingi kusuasua, ikiwemo vituo vya afya, kutokana na baadhi ya wazabuni kususia kutoa huduma.
Akihitimisha mjadala huo, Mwenyekiti wa Halmashauri, Maarifa Mwashitete, alimwagiza Mkurugenzi Mtendaji kuitisha kikao cha pamoja kati ya madiwani, wazabuni na wadau wengine ili kutafuta suluhu ya mkwamo huo.