Unguja. Wakati kukiwa na malalamiko ya upungufu wa mafuta Zanzibar, Serikali imesema hakuna changamoto hiyo na kueleza kilichotokea.

Hata hivyo, kiuhalisia katika baadhi ya vituo vya mafuta mjini hapa, vingine vimefungwa hakuna huduma inayotolewa na vingine kuna foleni za watu wanaotaka nishati hiyo.

Akitoa ufafanuzi leo Februari 20, 2026 katika Mkutano wa pili wa Baraza la 11 la Wawakilishi, Waziri wa Maji, Nishati na Madini, Nadir Abdulatif amesema kilichotokea ni kwamba meli iliyokuwa inaleta mafuta Zanzibar ilipata hitilafu hivyo zikachukuliwa jitihada za kuagiza meli zingine za mafuta.

“Kilichotokea, haijawahi kutokea kwa miaka mingi, meli iliyokuwa inaleta mafuta ilipata hitilafu katikati ya safari, ikabidi kuchukua jitihada za kuagiza meli zingine na meli hizo zimeshafika na mafuta yapo ya kutosha,” amesema Waziri Nadir.

Kwa mujibu wa waziri huyo, kuna dizeli lita za ujazo milioni saba na petroli kuna lita za ujazo milioni tatu baada ya meli tatu kushusha nishati hiyo kutoka Mombasa, Kenya.

Hata hivyo hakusema hitilafu hiyo ilitokea lini na meli hizo tatu zimeshusha lini mafuta hayo

Awali akiuliza swali la Barazani, Mwakilishi wa Paje Jaku alitaka kujua changamoto ya ukosefu wa mafuta umesababiahwa na nini.

Swali hilo alilielekeza kwa Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Badria Natai Masoud ambaye katika majibu yake alisema hawajapokea taarifa yoyote kuhusu kukosekana kwa mafuta lakini akaahidi kufuatilia.

Katika maeneo mbalimbali kumekuwapo na maelezo ya watumiaji wa nishati hizo wamesema baadhi ya vituo vya mafuta havina nishati hiyo.

“Hali ya mafuta imekuwa changamoto baadhi ya sheli yapo na baadhi zinasema hazina, hatujui tatizo ni kitu gani, amesema mmoja wa watumiaji nishati hiyo Hussein Mjaku mkazi wa Miembeni Unguja

Kwa upande wake Haroub Haroun ambaye amekutwa na dumu la kuchukulia mafuta katika moja ya kituo cha mafuta Unguja, amesema hicho ni kituo cha nne anazunguka lakini kila anapokwenda anaambiwa hakuna.

Amesema kukosekan a nishati hiyo kunasababisha usumbufu na kufanya bidhaa zingine zipande bei husuani ikiangalia katika kipindi hiki cha mwezi mtukufu wa Ramadhan.

“Nadhani ni katika utaratibu wa kushusha na kusambaza mafuta kwenye vituo ndio inatokea changamoto lakini kwasasa mafuta yapo,” amesema mmoja wa wauzaji mafuta ambaye hakuwa tayari kutaja jina lake kwa madai siyo msemaji.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *