Usiku wa Februari 19, 2026, Tanzania imempoteza mmoja wa viongozi wa dini  wakubwa. Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, Askofu Mkuu mstaafu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, aliaga dunia akiwa katika Taasisi ya Matibabu ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) jijini Dar es Salaam, mahali alipokuwa akipatiwa matibabu.

Taarifa ya rasmi ya kifo chake ilitolewa na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Yuda Thaddeus Ruwa’ichi, ambaye alisema: “Kanisa Katoliki limepata msiba mkubwa kufuatia kifo cha Mwadhama Kardinali Polycarp Pengo, aliyefariki akiwa anapatiwa ya matibabu.” Maneno haya mafupi yalibeba uzito wa pengo kubwa—pengo ambalo si tu kwa Kanisa, bali ya taifa zima la Tanzania.

Pengo alikuwa kardinali wa pili Mtanzania katika historia, akifuata nyayo za Kardinali Laurean Rugambwa, aliyepewa cheo hicho mwaka 1960 na Papa Yohane XXIII, akiwa pia kardinali wa kwanza Mwafrika.

Pengo alipewa cheo cha kardinali mwaka 1998 na Papa Yohane Paulo II—miaka 38 baadaye, akithibitisha kwamba Tanzania ina nafasi yake katika moyo wa Kanisa Katoliki la ulimwengu.

Alizaliwa Jumamosi ya Agosti 5, 1944 katika Kijiji cha Mwazye, parokia iliyokuwa ndani ya Jimbo la Sumbawanga, Mkoa wa Rukwa, Tanzania, wakati huo bado ikiitwa Tanganyika chini ya utawala wa Uingereza.

Ulimwengu aliokulia ulikuwa wa vijijini, ambapo maisha yalitegemea kilimo na dini kama nguzo ya jamii. Katika mazingira kama hayo, familia nyingi ziliamini kwamba kumsomesha mtoto katika Kanisa ilikuwa njia bora ya kumwandalia siku zijazo.

Mazingira ya Mwazye hayakuwa ya starehe kiuchumi, lakini yalikuwa na utajiri wa imani, moyo wa jamii na mfano wa wazee waliomcha Mungu. Hizo zilikuwa nguzo alizozibeba Pengo katika safari yake yote.

Safari ya elimu

Mwaka 1959, akiwa na umri wa miaka 15, Pengo alijiunga na Seminari Ndogo ya Kaengesa, ambapo alisomea miaka sita, hadi 1964. Miaka hiyo ilikuwa muhimu katika kujenga tabia, thamani na mwelekeo wake wa kiroho.

Seminari ndogo zilikuwa, na bado ni, shule za malezi ambayo si ya masomo peke yake, bali ya maadili, nidhamu na upendo wa Mungu.

Kisha akajiunga na Seminari Kuu ya Kipalapala mwaka 1965, akisomea falsafa kwa miaka mitatu (1965–1967) na theolojia kwa miaka minne (1968–1971). Kipalapala ilikuwa na bado ni moja ya taasisi ya Kanisa Katoliki Tanzania, ikizalisha viongozi wengi wa Kanisa na hata wa Serikali.

Juni 20, 1971, Polycarp Pengo aliwekwa wakfu kuwa padri na Askofu Charles Msakila katika Jimbo la Sumbawanga. Baada ya kuwekwa wakfu, alitumikia kwa muda mfupi kama Katibu wa Askofu wa Jimbo la Sumbawanga.

Mwaka 1973, Pengo alipelekwa Roma kwa masomo ya juu zaidi. Alikaa Chuo Kikuu cha Kipapa cha Lateran, hasa katika Chuo cha Mtakatifu Alfonso, ambapo alisomea Teolojia ya Maadili.

Mwaka 1977 alihitimu akiwa na shahada ya udaktari wa falsafa katika taaluma hiyo. Mtu aliyekuja kutoka Mwazye, kijiji kimoja nchini Tanzania, sasa alikuwa daktari wa teolojia kutoka Roma.

Baada ya kurejea Tanzania, Pengo alitoa ujuzi wake katika Seminari Kuu ya Kipalapala kwa miezi tisa, akifundisha Teolojia ya Maadili. Kisha mwaka 1978 akawa Mkurugenzi wa Kwanza (Rector) wa Seminari Kuu ya Segerea jijini Dar es Salaam – wadhifa alioushika hadi mwaka 1983. Kwa miaka mitano aliijenga seminari hiyo mpya, akiiweka katika msingi imara ambao umeidumu hadi leo.

Hatua kwa hatua katika uongozi

Novemba 11, 1983, Papa Yohane Paulo II alimteua Pengo kuwa Askofu wa Jimbo la Nachingwea, kusini mwa Tanzania. Aliwekwa wakfu kama askofu Januari 6, 1984, katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro, Vatican, siku ya Epifania, sikukuu inayokumbuka ufunuo wa Yesu kwa mataifa yote.

Oktoba 17, 1986, Pengo alihamishwa kuwa Askofu wa Jimbo jipya la Tunduru-Masasi, pia kusini mwa Tanzania, jimbo lililoundwa upya kutokana na mahitaji ya ukuaji wa Kanisa katika eneo hilo.

Januari 22, 1990, Papa Yohane Paulo II alimteua kuwa Askofu Mkuu Mwandamizi (Coadjutor Archbishop) wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, akisubiri kurithi nafasi ya Kardinali Laurean Rugambwa.

Julai 22, 1992, baada ya Kardinali Rugambwa kujiuzulu, Pengo aliingia rasmi kama Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam. Alikaa katika kiti hicho kwa miaka 27.

Ainuliwa kuwa Kardinali

Februari 21, 1998, Papa Yohane Paulo II alimteua Polycarp Pengo kuwa kardinali katika Mkutano Mkubwa (Consistory) uliofanyika Vatican. Alipewa cheo cha kardinali-padri na jina la kanisa lake la Vatican: Nostra Signora de La Salette (Bikira Maria wa La Salette).

Kama Kardinali, Pengo alishiriki katika mikutano ya kumchafua papa (conclaves) miwili; mwaka 2005 alishiriki katika uchaguzi wa Papa Benedict XVI na mwaka 2013 alishiriki katika uchaguzi wa Papa Francis.

Kama Kardinali pia, Pengo alikuwa mwanachama wa vyombo mbalimbali vya Vatican, vikiwamo: Baraza la Uenezaji wa Injili, Baraza la Imani, Baraza la Kidiplomasia la Dini, Baraza la Utamaduni na Baraza Maalum la Afrika la Sinodi ya Maaskofu.

Miaka 27 ya utumishi

Moja ya mafanikio makubwa katika miaka 27 ya uaskofu mkuu, ilikuwa katika uwanja wa malezi ya makasisi. Wakati alipoingia Dar es Salaam, kulikuwa na mapadri 20 tu. Katika kipindi chake, alizalisha mapadri 73 wapya, ongezeko ambalo linaonyesha bidii yake katika mafunzo na malezi ya nguvu kazi ya Kanisa.

Aliimarisha Seminari ya Segerea na kusaidia kwa njia mbalimbali, ikiwamo kwa kuwatumia Wawata (Wanawake Wakatoliki wa Tanzania) kushiriki katika msaada wa Seminari ya Visiga.

Alikuwa pia mwenye msimamo wa wazi katika masuala ya kijamii. Alishiriki katika mijadala ya kitaifa kuhusu maadili, utawala bora na nafasi ya dini katika jamii.

Maoni yake hayakuwa ya Kanisa tu, yaligusa mioyo na akili za Watanzania wengi, Wakatoliki na wasio Wakatoliki. Alionekana mara nyingi kama sauti inayozungumza ukweli bila hofu.

Askofu Mkuu mstaafu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es salaam Polycarp Kardinali Pengo akimuombea aliyekuwa Rais wa Tanzania, Dk John Magufuli Aprili 16, 2017 baada ya ibada ya Pasaka katika Kanisa la Mtakatifu Petro jijini Dar es salaam. Picha na Maktaba

Katika Ibada ya Kitume ya Papa Yohane Paulo II Tanzania Septemba 2, 1990, Pengo, wakati huo akiwa Askofu Msaidizi, ndiye aliyetoa hotuba ya kumkaribisha Papa mbele ya mapadri na watawa katika Kanisa la Mtakatifu Petro jijini Dar es Salaam.

Uongozi wa SECAM—sauti ya Kanisa la Afrika

Januari 2007, Kardinali Pengo alichaguliwa kuwa Rais wa SECAM, Kongamano la Mabaraza ya Maaskofu wa Afrika na Madagascar. SECAM ni mwili wa kiuongozi unaounganisha mabaraza yote ya maaskofu Afrika na Madagascar, na unawakilisha Kanisa la takriban waumini zaidi ya milioni 200 barani Afrika.

Kuwa Rais wa SECAM ni wadhifa mkubwa kwa kuwa ni kuwa msemaji mkuu wa Kanisa Katoliki barani Afrika.

Pengo alishika wadhifa huu hadi mwaka 2013, kipindi cha miaka sita ambapo aliongoza SECAM kupikatikatia changamoto kubwa za kijamii, kisiasa na kitheolojia barani Afrika.

Katika kipindi hicho, SECAM ilitoa waraka muhimu kuhusu utawala bora, haki za binadamu, na mchango wa Kanisa katika ustawi wa jamii, waraka ambao Pengo mwenyewe aliuwasilisha mjini Accra, nchini Ghana.

Alihimiza mabaraza yote ya maaskofu barani Afrika kuimarisha juhudi za uinjilishaji, akisema wazi kwamba ukuaji wa idadi ya watu Afrika unahitaji pia ukuaji wa Kanisa na nguvu ya ushuhuda wake. Aliweka mkazo wa pekee katika umoja wa mabaraza ya maaskofu, akiamini kwamba nguvu ya Kanisa Afrika ipo katika ushirikiano na si katika kujitenga.

Pia, alikuwa Mwakilishi wa Papa Francis katika ‘Beatification’ (Kutangazwa mwenye Heri) Sista Irene Stefani (Nyaatha) nchini Kenya Mei 23, 2015.

Mchango kwa Taifa, zaidi ya Ukatoliki

Pengo alikuwa kiongozi wa Kanisa, lakini mchango wake ulifikia zaidi ya malango ya kanisa. Kama Rais wa TEC, alishiriki moja kwa moja katika mazungumzo ya kitaifa, akishirikiana na Serikali, makundi ya kiraia, na vyombo vya kidini vingine.

Aliongea waziwazi kuhusu masuala ya kimaadili yanayoligusa taifa, kuhusu haki za binadamu, na kuhusu wajibu wa Serikali kwa wananchi wake. Wakati mwingine misimamo yake iliibua mjadala, lakini hilo ni asili ya kiongozi wa kweli: kusimama kwa imani yake hata palipokuwa na upinzani.

Suala la Ukimwi, ambalo kwa miaka mingi lilikuwa tatizo zito la Tanzania na Afrika, lilimsumbua sana Kardinali Pengo. Mara kwa mara alieleza msimamo wa Kanisa, kwamba suluhisho la kweli si katika usambazaji wa kondomu bali katika elimu ya watu mmoja mmoja kuwajibika, uaminifu katika ndoa na kushikilia maadili. Maoni haya yalipingana na baadhi ya taasisi za kimataifa, lakini Pengo alisimama imara akiamini kwamba elimu ya maadili ndiyo nguzo ya kweli.

Novemba 2018, aliongea waziwazi kwa hadhi kuhusu athari za “ukoloni wa kiitikadi” akionya Tanzania dhidi ya kukubali misaada ya nje ambayo inakuja na masharti ya kukubaliana na mtazamo wa Magharibi kuhusu masuala ya jinsia.

Alisema maneno mazito ambayo yalishtua wengi: kwamba ni bora kufa njaa kuliko kupokea msaada wenye “sumu” ya itikadi inayokinzana na dini na utamaduni wa Tanzania. Hilo lilikuwa ni sauti ya kiongozi aliyejua anachokiamini.

Kustaafu na miaka ya mwisho

Agosti 15, 2019, Papa Francis alikubali ombi lake la kustaafu, Pengo alikuwa amefikia umri wa miaka 75 wa kisheria. Aliacha wadhifa alioshika kwa miaka 27, akifungua ukurasa mpya wa historia ya Jimbo Kuu la Dar es Salaam.

Aliyevaa viatu vyake ni Askofu Mkuu Jude Thaddaeus Ruwa’ichi, ambaye aliendelea kusimamia Jimbo hilo na ambaye ndiye aliyetangaza habari ya msiba huu.

Katika miaka yake ya kustaafu, Pengo aliendelea kazi na Kanisa, akishiriki katika ibada mbalimbali, kutoa hekima yake kwa viongozi wachanga, na kuendelea kuwa sauti ya uzoefu katika mambo ya kijamii na kiroho.

Rais Samia Suluhu Hassan (kulia) akisalimiana na aliyekuwa Askofu Mkuu Mstaafu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, aliyefariki dunia usiku wa Februari 19, 2026. Picha na Maktaba

Mwaka 2022, alihusika katika uzinduzi wa majengo mapya ya Hospitali ya Mwenyeheri Joseph Allamano Makiungu huko Singida, akisema maneno muhimu: kwamba Kanisa lina wajibu wa pekee kwa wagonjwa na maskini, kwani hawa ndio “amana na utajiri wa Kanisa.”

Hata katika uzee wake, akili yake ilibaki makini na moyo wake ulibaki ukijaa upendo kwa Kanisa na kwa Tanzania.

Kilichobaki

Kardinali Polycarp Pengo anaondoka akiacha urithi mkubwa wa aina nyingi. Kwanza, ni urithi wa taasisi: Seminari ya Segerea ambayo yeye alikuwa mkurugenzi wake wa kwanza; mapadri 73 waliofunzwa na chini ya uongozi wake Dar es Salaam; vyama vya waumini vilivyoimarishwa; na Kanisa ambalo msingi wake ulitenganishwa kutoka utegemezi wa nje.

Pili, ni urithi wa kiakili na kiteolojia. Kama daktari wa Teolojia ya Maadili kutoka Roma, Pengo alitoa mchango wa kifikra ambao ulisaidia Kanisa Tanzania na Afrika kupaza sauti yake katika mazungumzo ya kimataifa.

Katika sinodi mbalimbali, ikiwamo Sinodi ya Maaskofu ya Afrika ya 1984 (ambapo alizungumza kuhusu “Kuimarisha Imani ya Kikristo katika Maisha ya Kila Siku”) na Sinodi ya 13 ya Kawaida ya Maaskofu mwaka 2012, Pengo aliwakilisha Afrika kwa ujasiri.

Tatu, ni urithi wa kimataifa. Kuwa Rais wa SECAM kwa miaka sita kuliipa Tanzania na Afrika Mashariki hadhi na uwakilishi katika ngazi za juu za Kanisa la ulimwengu.

Yeye binafsi alishiriki katika uchaguzi wa mapapa wawili ni uthibitisho kwamba sauti ya Tanzania inasikika katika chumba cha siri kinachochagua kiongozi wa Kanisa la ulimwengu.

Nne, ni urithi wa mfano wa maisha: mtu aliyetoka kijijini akiwa na ndoto tu, akasoma kwa bidii, akajitoa kwa Kanisa bila kujutia, na hatimaye akasimama mbele ya ulimwengu kama kiongozi anayeheshimika.

Kwa vijana wa Tanzania, Wakatoliki na wasio Wakatoliki, hadithi ya Pengo ni ushahidi kwamba asili ya mtu haidhibitishi mwisho wake.

Safari imekamilika

Mwazye ni kijiji kimoja Tanzania. Vatican ni kitovu cha Kanisa Katoliki la ulimwengu, taasisi yenye historia ya miaka elfu mbili, yenye nguvu za kiroho za waumini zaidi ya bilioni moja.

Umbali kati ya Mwazye na Vatican si wa kilomita tu, ni wa utamaduni, elimu, historia na hatima. Kuvuka umbali huo si kazi rahisi. Polycarp Pengo alifanya hivyo.

Kutoka Mwazye, kupitia Kaengesa, Kipalapala, Roma, Nachingwea, Tunduru-Masasi na Dar es Salaam hadi Vatican, kila hatua ilimfanya awe zaidi ya alivyokuwa.

Tanzania imepoteza mwana wake mkubwa. Kanisa Afrika limepoteza nguzo yake kuu. Lakini historia haina uwezo wa kufuta aliyoandika na kizazi kilichomfuata kitaendelea kuchota katika kisima alichocha.

Raha ya Milele umpe ee Bwana, mwanga wa milele umwangazie, Kardinali Pengo. apumzike kwa amani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *