DAR ES SALAAM;  IKIWA ni muendelezo wa kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia, Kampuni ya Oryx Gas imezindua kampeni ya msimu wa mwezi wa Ramadhan na Kwaresma inayoitwa Pishi la Kibabe ikiwa ni sehemu pia kurejesha shukrani kwa wateja wao.

Akizungumza leo Februari 20,2026 jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi huo Meneja Masoko na Mauzo wa Oryx Gas Tanzania , Shaaban Fundi amesema huu ni mwezi wa kujitafakari ,kushirikiana ,kujitolea na zaidi ya yote kuunganisha watu wote.

“Ili kuunga mkono wateja wetu katika kipindi hiki maalumu tunatoa bei ya promosheni kwenye mitungi yetu mipya ya kilo sita itauzwa kwa Sh.37000 Tanzania Bara na Zanzibar, ”amesema Fundi

Pia amesema mbali ya kupunguza bei katika kipindi hiki cha Ramadhan na Kwaresma wateja wao watakaonunua au kujaza gesi kwenye maduka maalumu ya Oryx na Mangi Shop watapokea zawadi ya futari kama ishara ya shukrani yao kwao.

Akizungumza kuhusu gharama za mtungi wa kilo sita amesema mpaka  unafika nchini Tanzania gharama yake haipungui Sh.80,000, lakini Oryx katika soko mtungi huo unapatikana kwa Sh.40000 na sasa unauzwa kwa promosheni mpaka Sh.37000.

“Oryx Gas tunashusha bei kwa ajili ya kuiwezesha jamii iweze kutumia nishati safi ya kupikia.Pia tunaishukuru serikali kwa mfano sasa hivi tuna msamaha wa kodi katika mitungi pamoja na jitihada nyingine wanazochukua.

“Hata hivyo tunaomba serikali iendelee kuangalia katika maeneo mengine ili kuhakikisha kwamba gesi pamoja na mtungi bei yake inakuwa chini, ili wananchi waweze kupata kwa bei nafuu.Kwa kufanya hivyo Oryx Gas kwa kushirikiana na serikali tunaweza kufanikisha matumizi ya nishati safi kwa wananchi wengi zaidi.

“Kuhusu gharama ukilinganisha mkaa na kuni bei yake iko juu zaidi ya nishati safi ya kupikia,  kwani kwa familia ya kawaida kwa siku moja inatumia kopo moja la mkaa ambalo linauzwa Sh.2000 hivyo kwa mwezi ni Sh.60,000 wakati mtungi wa gesi ya oryx wa kilo 6 ni Sh 40,000.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Oryx Gas Tanzania, Benoit Araman amesema lengo la kampeni iliyozinduliwa kwa ajili ya Mfungo wa Mwezi wa Ramadhan na Kwaresma ni muendelezo wa kuhamasisha matumizi ya nishati safi nchini ikiwa ni kuunga mkono juhudi za serikali za kuhimiza wananchi kutumia nishati safi ya kupikia.

Wakati huo huo Mkuu wa Idara ya Mauzo ya Gesi kwa Ujumla, Carloline Msokwa amesema kipindi hiki Waislamu na Wakristo wanaungana pamoja kuomba toba na ni kipindi ambacho familia zinakaa kufanya ibada na kuomba toba lakini pia ni wakati wa kupika chakula kizuri kwa ajili ya kufutur na ndiyo sababu ya Poshi la Kibabe.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *