
Mahakama ya Morocco imewahukumu mashabiki 19 wa soka kifungo cha mwaka mmoja jela kwa vitendo vya kihuni walivyovionesha wakati wa mchezo wa fainali ya AFCON 2025 kati ya Morocco na Senegal, ambapo walijaribu kuvamia uwanja.
Baada ya kikao cha mahakama kilichodumu kwa zaidi ya masaa matano, Jaji aliyekuwa akiongoza kesi hiyo aliamua kuwa mashabiki hao, raia 18 wa Senegal na mmoja wa Ufaransa, walikuwa na hatia ya zaidi ya mashtaka sita, yakiwemo ya kuharibu miundombinu ya uwanja wa michezo na kufanya vurugu wakati wa tukio la michezo.
Kwa mujibu wa Wakili Naima El Guellaf, mashabiki 11 wamehukumiwa kifungo cha mwaka mmoja jela na kutozwa faini ya dola 550. Wanne wengine wamehukumiwa kifungo cha miezi sita na faini ya dola 218. Na wanne waliobaki wamehukumiwa kifungo cha miezi mitatu jela na faini ya dola 130.
Ripoti zinasema, mmoja wa washtakiwa alizimia baada ya kusomewa hukumu. Wengine walikataa kusimama kutoka kwenye benchi la washtakiwa walipoelekezwa kuelekea kwenye chumba kidogo cha mahabusu. Aidha ndugu zao, wakiwa na mshtuko mkubwa, walisisitiza kuwa jamaa zao hawana hatia.
Mawakili wa utetezi wamesema wanapanga kukata rufaa dhidi ya uamuzi huo wanaouona kuwa ni mkali kupita kiasi.
Washtakiwa hao walikamatwa mwezi uliopita baada ya mashabiki wenye hasira kujaribu kuvamia uwanja wakipinga penalti ya dakika za mwisho iliyotolewa kwa wenyeji Morocco katika fainali hiyo, ambayo Senegal iliibuka mshindi kwa bao moja sufuri. Mashabiki hao walizuiliwa rumande kwa zaidi ya mwezi mmoja wakisubiri hukumu.
Katika kikao cha kesi hiyo kilichohudhuriwa na wanadiplomasia wa Senegal na Ufaransa pamoja na ndugu wa baadhi ya washtakiwa, mawakili walidai kwamba mahakama haikuwa na ushahidi wa kutosha kuwatia hatiani mashabiki hao.
Mwendesha mashtaka wa serikali aliiomba mahakama itoe adhabu ya juu zaidi dhidi ya mashabiki hao, akisema walivuruga utaratibu wa mechi hiyo. Alidai kwamba uharibifu uliotokea unakadiriwa kupindukia dola 476,719.
Morocco imekuwa kwa muda mrefu ikikabiliwa na matukio ya uhuni yanayohusiana na soka, na mara kwa mara mahakama zake hushughulikia kesi za aina hiyo. Hata hivyo, kesi hii ilikuwa ya kipekee kwa kuwa imehusisha raia wa kigeni pekee…/