
Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia imetangaza kuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo Sergey Lavrov amesema Moscow inaunga mkono kufikiwa suluhisho la kisiasa na kidiplomasia litakaloheshimu haki za kisheria za Iran katika mazungumzo ya nyuklia na Marekani.
Lavrov ametangaza msimamo huo katika mazungumzo aliyofanya kwa njia ya simu siku ya Ijumaa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Jmahuri ya Kiislamu ya Iran Sayyid Abbas Araghchi.
Katika mazungumzo hayo, Araghchi na Lavrov walibadilishana mawazo kuhusu hali ya sasa ya kadhia ya nyuklia ya Iran, ikiwa ni pamoja na matokeo ya mazungumzo yasiyo ya ana kwa ana yaliyofanyika kati ya Marekani na Iran siku ya Jumanne mjini Geneva, Uswisi kwa uunganishi wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman Badr Albusaidi.
Kwa mujibu wa ripoti ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia, Moscow imetangaza kwa mara nyingine tena uungaji mkono wake kwa mchakato wa mazungumzo yanayolenga kupata suluhisho la kisiasa na kidiplomasia linaloheshimu haki za kisheria za Iran, kwa mujibu wa misingi ya Mkataba Unaopiga Marufuku Uenezaji Silaha za Nyuklia, NPT.
Katika mazungumzo hayo ya simu, Araghchi na Lavrov walijadili pia masuala kadhaa yanayohusu maslahi ya pamoja katika uhusiano kati ya pande mbili za Iran na Russia.
Kwa mujibu wa shirika la habari la IRNA, mazungumzo hayo ya simu ya mawaziri wa mambo ya nje wa Iran na Russia yalifanyika baada ya pande mbili kusaini hati ya ushirikiano na hati nne za makubaliano mwishoni mwa kikao cha 19 cha Tume ya Pamoja ya Ushirikiano wa Kiuchumi ya Iran na Russia kilichofanyika mjini Tehran mnamo Februari 18. Kikao hicho kiliongozwa kwa pamoja na Waziri wa Mafuta wa Iran na Waziri wa Nishati wa Russia…/