
Wimbi la upinzani limeibuka miongoni mwa Wabunge wa Marekani dhidi ya sera za Rais Donald Trump zinazochochea vita dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Kulingana na Pars Today, huku uvumi kuhusu uwezekano wa hatua za kijeshi za Marekani dhidi ya Iran ukiongezeka, maseneta kadhaa wenye ushawishi na wawakilishi wa Bunge la Marekani wamechapisha jumbe mbalimbali kwenye mitandao ya kijamii, wakipinga waziwazi chokochoko yoyote ya kijeshi ya Donald Trump dhidi ya Iran.
Wabunge hawa, ambao wengi wao ni kutoka vyama vya Democrat na Republican, Alkhamisi iliyopita walitoa mwito wa kusitishwa mara moja kwa sera hizi, wakiashiria matokeo mabaya ya vita hivyo, na kuheshimu mamlaka ya Bunge katika kuchukuua uamuzi wa kuingia vitani.
Don Beyer, Mdemokrati wa Virginia katika Baraza la Wawakilishi la Marekani, aliandika kwenye mtandao wa kijamii wa X akizungumzia kujiondoa Trump katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA mwaka 2018: “Trump anatishia kwamba Marekani itaingia vitani na Iran isipokuwa kama Tehran itasaini makubaliano kama ya awali.” Alisisitiza: “Hapana kupigana vita na Iran.”
Wakati huo huo, mwakilishi wa Chama cha Democrat mjini Washington, Pramila Jayapal, akinukuu Katiba, alipinga kuchukuliwa hatua yoyote ya kijeshi bila idhini ya Bunge na kutoa wito wa kusitishwa uzushaji mizozo.
Jim McGovern, Mdemokrati mwakilishi wa Bunge la Marekani kutoka Massachusetts, pia alisisitiza vipaumbele vya ndani na yeye anaona kuwa vita na Iran ni kinyume na matakwa ya watu wa Marekani, akisema, “Wamarekani wanataka kushushwa zaidi bei za bidhaa na huduma bora za afya, na si vita.”
Kiujumja nchini Marekani kumeibuka wasiwasi wa kukaririwa makosa ya huko nyuma katika Asia Magharibi
Baadhi ya wabunge wa Marekani pia sambamba na kuashiria uzoefu mchungu wa vita vya huko nyuma wameonya juu ya kukaririwa makosa ya huko nyuma. Jason Crow, mwakilishi wa chama cha Democrat katika jimbo la Colorado na veterani wa vita, alikumbushia jinsi Trump alivyolipua mabomu katika nchi saba na kusisitiza kwamba, watu wa Marekani wamechoka na migogoro isiyoisha. Andy Kim, mwakilishi mwingine wa chama cha Democrat katika jimbo la New Jersey, pia aliuliza katika ujumbe wake: “Vita na Iran inakuletea nini? Je, itakufanya wewe uwe salama zaidi?” Alimshutumu Trump kwa kuisukuma nchi hiyo kwenye ukingo wa vita bila sababu au mpango.
Hata baadhi ya shakhsia wa chama cha Republican wamejiunga na mrengo wa upinzani. Mbunge Thomas Massie, anayewakilisha jimbo la Kentucky, alitoa wito wa kura katika Bunge kuhusu hatua yoyote ya kijeshi, akisema: “Nitapiga kura ya ‘Marekani Kwanza,’ ambayo ina maana ya kura ya kupinga vita zaidi katika Mashariki ya Kati.”
Mwakilishi wa zamani wa Republican Marjorie Taylor Greene pia alisisitiza hamu ya umma ya kukomeshwa vita vya kigeni, akiashiria matokeo ya uchaguzi wa 2024.
Wataalamu wa kimkakati pia walitathmini hatua hizi kama zinazohudumia maslahi ya utawala wa Kizayuni. Mtaalamu wa usalama wa taifa David Payne alielezea vitendo hivi kama “vita vya uchokozi vya Marekani visivyo na haki kwa niaba ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu” na kuonya kwamba chokochoko kama hizo zinaweza kusababisha kushindwa Marekani na kutoweka utulivu wa kiuchumi. Pia aliashiria uwezo wa Iran kufunga Lango Bahari la Hormuz na athari zake mbaya katika kupanda bei ya mafuta katika soko la dunia.