Leo ni Jumamosi 3 Ramadhani 1447 Hijria ambayo inasadifiana na 21 Februari 2026 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1034 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria alifariki dunia Muhammad bin Nu’man mwenye lakabu ya Sheikh Mufid, msomi na mwanafaqihi mkubwa wa ulimwengu wa Kiislamu katika mji wa Baghdad. Sheikh Mufid alilelewa katika familia ya kielimu, kidini na yenye imani na kisha kujipatia elimu kutoka kwa wanazuoni wakubwa katika zama hizo. Miongoni mwa harakati za kifikra na kiutamaduni za Sheikh Mufid ilikuwa ni kufanya midahalo na mafaqihi na wasomi wa madhehebu mbalimbali. Sheikh Mufid ametuachia vitabu mbalimbali vyenye thamani vikiwemo al Irshaad, al Arkaan na Usuulul Fiqh.

Katika siku kama ya leo miaka 880 iliyopita aliaga dunia Ibn Khashhab mhakiki na mwandishi mashuhuri wa Kiislamu wa karne ya sita Hijria. Alizaliwa mwaka 492 Hijria huko Iraq na kuanza kujifunza masomo ya zama hizo tangu akiwa mdogo. Ibn Kashshab hatua kwa hatua alijifunza masomo ya mantiki, hadithi na uandishi na kuanza kuandika vitabu mbalimbali katika nyanja hizo. Ibn Khashshab alikuwa shakhsiya wa aina yake na ndio maana akafahamika sana kwa jina la Allamah. Aidha alitajwa kama bwana wa maqarii wa zama zake kutokana na umahiri wake katika kusoma na kufahamu vyema Qur’ani Tukufu. 

Siku kama ya leo miaka 110 iliyopita, inayosadifiana na 21 Februari 1916 vilianza vita vikubwa vya umwagikaji damu vilivyojulikana kwa jina la ‘Verdun’ kati ya Ujerumani na Ufaransa. Vita hivyo vilivyoendelea kwa muda wa miezi kumi vilimalizika kwa kushindwa vikosi vya jeshi la Ujerumani na wanajeshi karibu milioni moja wa nchi hizo mbili kuuawa. Tukio hilo ni miongoni mwa sababu za kushindwa Ujerumani kwenye Vita vya Kwanza vya Dunia. 

Katika siku kama ya leo miaka 68 iliyopita, wananchi wa Misri na Syria walishiriki kwenye kura ya maoni ya kuunganisha nchi mbili hizo chini ya Jamhuri ya Muungano wa Kiarabu. Wananchi wa nchi hizo mbili walimchagua Jamal Abdul-Nasser kiongozi wa wakati huo wa Misri, kuwa rais wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Kiarabu.Baada ya kupita miezi kadhaa, Yemen nayo ilijiunga kwenye muungano huo. Hata hivyo muungano huo haukudumu kwa zaidi ya miaka mitatu, kwani Syria ilitangaza kujitoa kwenye muungano huo kutokana na kutoridhishwa na uongozi wa Jamal Abdul-Nasser.

Siku kama ya leo mia 61 iliyopita, Malcolm X, Mmarekani mweusi aliuawa baada ya kushambuliwa na magaidi nchini humo. Malcolm X alizaliwa mwaka 1925, na wakati alipokuwa kwenye rika la ujana alifahamiana na makundi ya vijana wa Kiislamu na hatimaye kusilimu. Itikadi za mwanaharakati huyo wa Kiislamu ziliwachukiza watawala wa Marekani na makundi ya ubaguzi wa rangi nchini humo. Malcolm X aliuawa akihutubia mkutano. Alikuwa akisisitiza mara kwa mara kuwa, Wamarekani weusi ambao wanakandamizwa na kubaguliwa na serikali ya Marekani wanaweza kujipatia uhuru na uadilifu chini ya mwavuli wa utawala wa Kiislamu.

Tarehe 21 Februari miaka 53 iliyopita ndege ya abiria ya shirika la ndege la Libya iliyokuwa ikielekea Misri ilidunguliwa na wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel. Ndege hiyo ya raia ilikuwa njiani kutoka Tripoli, mji mkuu wa Libya, kuelekea Cairo, mji mkuu wa Misri, ilipopoteza njia kutokana na hali mbaya ya hewa na kuonekana kwenye jangwa la Sinai kaskazini mwa Misri. Wakati huo, eneo la Sinai lilikuwa linakaliwa kwa mabavu na utawala wa Kizayuni wa Israel, na ndege za kijeshi za utawala huo ziliishambulia bila kujali kwamba ndege hiyo ya Libya ilikuwa ya abiria. Abiria 108 kati ya 113 waliokuwemo kwenye ndege hiyo waliuawa. Uhalifu huu uliamsha hasira ya walimwengu na ulilaaniwa piia na Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga (ICAO).

Miaka 26 iliyopita kwa mara ya kwanza “Siku ya Kimataifa ya Lugha ya Mama” iliadhimishwa. Uamuzi wa kuitangaza siku hii kuwa ni Siku ya Kimataifa ya Lugha ya Mama ulichukuliwa Novemba 1999 na Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) ambapo mwaka 2008 ulipewa pia jina la ‘Mwaka wa Kimataifa wa Lugha”. Sisitizo la kulinda na kuimarisha lugha ya mama linatokana na kuwa, takribani nusu ya lugha 6,000 zinazotambulika duniani zimo katika hatari ya kutokomea kutokana na sababu mbalimbali hususan uingiaji na utwishaji wa lugha za kimataifa kwa kutumia mbinu mbalimbali. 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *