Mwandishi maarufu wa gazeti la Marekani la New York Times, Thomas Friedman, ameonya kwamba waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu anamhadaa Rais wa Marekani, Donald Trump, na makundi ya jamii ya Wayahudi wa Marekani ili kuendeleza malengo yake ya kisiasa yenye utata, ikiwa ni pamoja na kuongezeka mvutano na Iran.

“Bibi anamchezea Rais Donald Trump na Wayahudi wa Marekani kama wapumbavu. Na ikiwa Marekani itaruhusu akwepe kuadhibiwa, tutakuwa sisi ndio wapumbavu,” Friedman ameandika katika makala yake kwenye gazeti la New York Times.

“Netanyahu anatema mate usoni mwa Marekani na kisha ananiambia kunanyesha. Lakini hakuna mvua,” ameandika Friedman akitumia lugha chafu kuonyesha jinsi alivyokatishwa tamaa na upotoshaji wa kimkakati.

Kwa mujibu wa Friedman, Netanyahu anaelekeza makusudi mazingatio ya Washington kwenye vita na Iran ili kuficha yanayoendelea katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu na Israel na msimamo wa muda mrefu wa Israel huko Gaza.

Wiki iliyopita Netanyahu alitembelea Ikulu ya White House kujadili kadhia ya Iran. Wachambuzi wanasema Netanyahu alikwenda huko Marekani ili kuingilia juhudi za kidiplomasia, huku mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya Tehran na Washington yakiendelea kuwa chanya.

Msimamo huu wa mwandishi maarufu wa gazeti la Marekani la New York Times Marekani, Thomas Friedman, unakuja huku kukiwa na ongezeko kubwa la maneno ya vitisho kutoka Washington na mkusanyiko mkubwa wa zana za kijeshi za Marekani karibu na nje ya pwani ya Iran.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inasisitiza kuwa haitaanzisha vita, lakini itatoa jibu zito kwa kitendo chochote cha uchokozi.

Friedman amesema Netanyahu anaendeleza sera zake katika Ukingo wa Magharibi na Gaza ambazo zinatishia maslahi mapana ya Marekani katika Mashariki ya Kati na usalama wa muda mrefu wa Wayahudi duniani kote.

Ameonya zaidi kwamba kuharakisha hatua za kunyakua eneo la Ukingo wa Magharibi na kudumisha udhibiti wa muda mrefu wa Gaza bila kuwapa Wapalestina haki za kisiasa kutakuwa na matokeo mabaya ya kimaadili, kwa idadi ya watu, na ya kimkakati.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *