Marekani. Mwanamitindo na mwanzilishi wa kampuni ya Rhode, Hailey Bieber, 29, amefunguka kuhusu maisha yake ya ndoa akisema anatamani kuongeza watoto zaidi katika familia yao lakini hana haraka.

Hailey ambaye yupo katika ndoa na Justin Bieber, 31, tangu mwaka 2018, pia alieleza mapenzi yake katika muziki wa mumewe akitaja albamu mbili anazozikubali zaidi kutoka kwake.

Akizungumza na Podcast ya Therapuss, Hailey alisema mtoto wao wa pekee, Jack Blues Bieber mwenye umri wa miezi 16, tayari ameanza kuonyesha dalili za kurithi kipaji cha muziki kutoka kwa baba yake.

Katika Podcast hiyo inayoendeshwa na Jake Shane, mrembo huyo alieleza namna mtoto wao alivyoanza kuimba wimbo maarufu wa Justin Bieber, Baby (2010).

“Ndiyo anafanya hivyo. Amekuwa akisema, ‘Baby, oh baby, oh baby oh.’ Na mimi nikawa kama, ‘wow, hiyo ni nzuri sana,’” alisema Hailey.

Alieleza kuwa tayari Jack anaongea maneno kadhaa na anaonesha wepesi wa kujifunza, mathalani kila mara anatamka neno ‘basketball’ kwa sababu ni moja ya michezo anayoipenda baba yake.

“Anaongea sana kwa umri wake. Anasema ‘basketball’ muda wote… Pia alijua kusema ‘sorry’ kwa lugha ya alama kabla hata hajaanza kulitamka neno hilo kwa sauti,” ameeleza.

Kuhusu uzazi, Hailey alisema siku zote alijua kuwa anataka kuwa mama na amefurahia kila hatua ya safari hiyo. Alipoulizwa kama yeye na Bieber wamepanga kupata watoto zaidi, alijibu ‘ndiyo’ bila kusita.

“Kwa hakika nataka kuwa na mmoja zaidi. Sina haraka, lakini hakika nataka watoto zaidi. Labda nitapata wanne, labda watatu. Sijui, kwa kweli sijui,” alisema Hailey.

Ingawa sura ya mtoto wao haijawekwa hadharani hadi sasa, Hailey alimwonyesha Jake Shane picha ya mtoto huyo (Jack) na kueleza kuwa hivi karibuni alimnyoa nywele zake.

“Kwa sasa anaonekana kufanana kabisa na baba yake Bieber,” alisema Jake Shane baada ya kuona picha hiyo huku akionyesha kushangazwa na ukuaji wake. “Oh Mungu wangu, ni mzuri sana na ni mchanganyiko wenu kamili”.

Mbali na familia, Hailey pia alizungumzia muziki wa mume wake na kutaja albamu anazozipenda zaidi kutoka kwake. Albamu ya kwanza ni Journals (2013), na ya pili ni Purpose (2015) yenye nyimbo kali kama What Do You Mean?, Sorry na Love Yourself.

Kuhusu albamu mpya ya Bieber, Swag (2025), ambayo ilifikia nafasi ya pili kwenye chati ya Billboard 200, Hailey alisema. “Ni albamu nzuri sana kuisikiliza kuanzia mwanzo hadi mwisho,”.

“Ni wazi labda nina upendeleo kidogo, lakini nadhani ishara ya albamu nzuri ni ile ambayo baada ya muda unarudi kuisikiliza tena na tena, na mimi bado naendelea kuirudia mara kwa mara,” aliongeza.

Ikumbukwe mwaka mmoja baada ya wawili hao kufunga ndoa  ya kiserikali, ndipo walifanya harusi yao iliyohudhuriwa na familia, ndugu na marafiki wao zaidi ya 150 katika hoteli ya Montage Palmetto Bluff.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *