MOROGORO: HALMASHAURI ya Wilaya ya Kilosa, mkoani Morogoro inaendelea kukamilisha ujenzi wa miradi mipya ya maendeleo ikiwemo Shule ya Sekondari ya Wasichana Kilosa.
Shule hiyo inajengwa kwa mapato ya ndani pamoja na nguvu za wananchi itagharimu zaidi ya Sh bilioni 1.5 hadi kukamilika kwake.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Aman Sewando amesema hayo wakati wa ziara yake ya kukagua miradi ya maendeleo iliyokamilika na inayoendelea kujegwa ili kutoa huduma bora kwa wananchi.
Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, alilidhishwa na hatua iliyofikiwa kwa kuwa mradi huo ulikwama uendelezaji wake kwa zaidi ya miaka mitatu kuanzia 2022.

Shule hiyo kwa mwaka wa masomo 2026 imepokea wanafunzi wa kike wa kidato cha kwanza wenye ufaulu wa juu na wanaokosa nafasi katika shule za vipaji maalumu kuendelea na masomo.
“Nichukue nafasi hii kumpongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri yetu ya Kilosa tangu amefika ndani ya mwaka mmoja amefanya kazi kubwa kuendeleza ujenzi wa shule hii maalum ya wasichana ambayo ilikwama kwa miaka mitatu, sasa hivi watoto wetu wameanza kusoma hapa,” amesema Sewando.
Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo amesema Serikali inapotoa fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo kinachotakiwa kuonekana ni matokeo chanya na miradi hiyo iwe inatoa huduma kwa wananchi kwa wakati ili kuwaondolea kero zinazowakabili hususani katika sekta ya afya na elimu.

Sewando amewataka watumishi wa halmashauri hiyo wanaopewa kazi ya kusimamia miradi ya maendeleo kuhakikisha inakamilika kwa wakati na kuanza kuhudumia wananchi ili kupunguza kero zinazowakabili.
Naye, Kaimu Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Kilosa, Dominica Swai amesema hadi kukamilika itakuwa na madarasa 10 na jengo moja la utawala .
Swai amesema majengo mengine ni maabara tatu ya masomo ya sayansi , maktaba moja, chumba cha tehama kimoja ,mabweni manne, nyumba mbili za walimu, vyoo matundu 18, kichomeo cha taka kimoja pamoja na ujenzi wa uzio.

Kaimu Mkuu wa shule hiyo amesema majengo yote hayo yatagharimu kiasi cha Sh bilioni 1.5 mpaka kukamilika kwake na unatekelezwa wa mradi huo unatokana na mapato ya ndani ya halmashauri pamoja na nguvu za wananchi na unafanyika kwa awamu tatu.
Wakati huo huo Mwalimu mkuu wa Shule ya msingi Shikizi Chief Ngwila iliyopo Kijiji cha Lumango, kata ya Kidodi, Daniel Lumbe ameelezea namna ujenzi wa shule hiyo ulianza mwaka 2025 na kugharimu kiasi sh milioni 305.8.
Amesema Shule hiyo ni mkombozi kwa wanafunzi zaidi ya 208 waliokuwa analazimika kusafiri umbali mrefu kwenda shule mama.
Lumbe amesema shule iliyojengwa ina vyumba saba vya madarasa , jengo la vyumba viwili vya elimu ya awali na jengo la vyoo matundu 14 na imeanza kutumika mwaka wa masomo 2026 kwa kupokea wanafunzi 208 kuanzia darasan awali hadi darasa la saba na kati ya wavulana ni 92 na 116.
“Wanafunzi hawa ni kutoka vitongoji viwili vilivyopo katika kijiji cha Lumango na kabla kujengwa shule hii ya msingi shikizi walikuwa wakisafiri kwenda shule mama ya msingi Lumango iliyopo umbali wa zaidi ya kilometa saba hadi 10,”alisema Mwalimu Lumbe.