Moscow imetangaza kuwa mazoezi ya pamoja ya majini kati ya majeshi ya Iran, Russia na China yatafanyika katika Lango -Bahari la Hormuz.

Nikolai Patrushev, Msaidizi wa Rais wa Russia na Mkuu wa Kikosi cha Wanamaji cha nchi hiyo alitangaza  17 mwezi huu wa Februari kwamba Iran, Russia na China zitafanya mazoezi katika ya kijeshi Lango- Bahari la Hormuz. Patrushev alisema kuwa China na Iran zimetuma meli kushiriki kwenye maneva hayo katika Lango-Bahari la Hormuz. Nikilai Patrushev ametaja mazoezi ya “Ukanda wa Usalama wa Bahari-2026” kati ya Russia, China na Iran katika Lango-Bahari la Hormuz kuwa tukio muhimu na la wakati unaofaa. 

Nikolai Patrushev

Maneva ya baharini yaliyopewa jina la ” Ukanda wa Usalama wa Bahari -2026″ yamekuwa yakifanyika tangu mwaka 2019 kwa ubunifu wa Kikosi cha Wanamaji cha Iran. Lengo la mazoezi hayo ya kijeshi limetangaza kuwa ni kuimarisha usalama wa biashara ya baharini duniani, kuboresha hatua za pamoja za kukabiliana na uharamia, ugaidi wa baharini na kufanya shughuli za uokoaji. 

Mazoezi ya pamoja ya baharini kati ya nchi za kundi la BRICS yalifayika mwanzoni mwaka huu lengo likiwa ni  kulinda njia za baharini dhidi ya kile kinajulikana kama “uharamia wa Magharibi.” Maneva ya kundi la BRICS chini ya anwani ” Azma ya Amani -2026″ pia yalifanyika mwezi Januari mwaka huu kusini mwa Bahari ya Atlantiki yakishirikisha majeshi ya  Russia, China, Iran, Imarati na Afrika Kusini. Hivi sasa pia maneva ya “Ukanda wa Usalama wa Baharini – 2026” kati ya Russia, China na Iran yanafanyika katika Lango – Bahari la Hormuz.

Akifafanua maneva ya baharini ya hivi karibuni kati ya Russia na nchi nyingine zikiwemo nchi wanachama wa kundi la BRICS, afisa huyo wa ngazi ya juu wa Russia amesema: “Mazoezi haya yanafanyika ili kulinda njia za biashara, ambazo sasa zimeathiriwa pakubwa, ikiwa ni pamoja na kile kinachoitwa uharamia wa Magharibi.”

Kufanyika maneva ya pamoja ya baharini kati ya Iran, Russia na China mwezi huu wa Februari kuna umuhimu mkubwa wa kimkakati zaidi ya kuwa ya mazoezi ya kawaida ya kijeshi. Katika upande wa matukio ya haraka ya kikanda na kimataifa, tukio hili linatoa jumbe tofauti kwa wachezaji wa kimataifa. Kuna sababu kadhaa za udharura wa kuchunguzwa mazoezi haya.

Ukanda wa Usalama wa Baharini-2026

Sababu ya kwanza ni umuhimu wa mazoezi yenyewe katika kipindi cha sasa, ambapo ni kukabiliana kimkakati na misimamo ya upande mmoja ya kijiopolitiki. 

Katika hali ambayo Marekani hivi karibuni ilifanya oparesheni kubwa za kijeshi huko Karibiani na katika Bahari ya Pasifiki na kuonyesha kuwa inatumia nguvu ili kudhamini maslahi yake, na wakati huo huo kutuma wanajeshi wake wa majini huko kaskazini mwa Bahari ya Hindi na katika Bahari ya Arabia, kuwepo muungano kati ya Tehran, Moscow na Beijing kunaleta mlingano wa nguvu katika uwanja huu. Mazoezi hayo ya kijeshi yanaidhihirishia Washington kwamba hatua za kijeshi za upande mmoja popote pale duniani zitakabiliwa na majibu ya pamoja na makali kaskazini mwa Bahari ya Hindi na katika eneo la Ghuba ya Uajemi; na kwamba eneo la Asia Magharibi kamwe halitakuwa uwanja wa  maamuzi ya kambi moja. 

Sababu ya pili, kudhamini usalama wa njia za kiuchumi na nishati. Mwaka huu wa 2026 umeshuhudia mabadiliko makubwa katika masoko ya kimataifa. Usalama wa Lango-Bahari la Hormuz ni muhimu kwa China ambayo ni mtumiaji mkubwa wa nishati kwa upande mmoja, na kwa upande wa pili kwa Russia ambayo ni mhusika mkuu katika masoko ya nishati. Kufanyika mazoezi hayo ya kijeshi ya pamoja sambamba na Marekani kufanya kila iwezavyo kuibua ukosefu wa usalama na wasiwasi katika Ghuba ya Uajemi na katika Bahari ya Oman, kunatuma ujumbe kwa wawekezaji na kwa nchi mbalimbali duniani kote kwamba usalama wa biashara ya kimataifa na usafirishaji  wa nishati unadhaminiwa na nchi za kikanda na washirika wao, na hakuna haja ya kuwepo wanajeshi wa nchi ajinabi katika eneo hili.

Sababu ya tatu, ni  kuimarisha ushirikiano kati ya nchi na kambi kadhaa duniani. Kufanyika maneva tajwa katika mwezi huu wa Februari hususan wakati huu ambapo nchi za Magharibi zinafanya kila ziwezalo kuziwekea vikwazo na mashikinizo ya kiwango cha juu na kuzitisha kijeshi nchi huru hususan Iran, kuna umuhimu maalumu. Maneva haya ya baharini yanaonyesha kuwa mbinu za Magharibi za kuzitenga nchi mbalimbali duniani zimegoga mwamba na kufeli; na Iran, Russia na China zinaweza kuwa kigezo kipya kwa ajili ya ushirikiano huru wa kiulinzi, mbali na mifumo ya kijeshi ya nchi za Magharibi. Hii itazidisha hadhi ya kisiasa na kijeshi kwa nchi zote tatu katika majukwaa ya kimataifa.

Sababu ya nne, kuboresha utaratibu wa kimbinu na kubadilishana taarifa. Vitisho vya sasa vya baharini, kuanzia magendo ya dawa za kulevya hadi mashambulizi ya pande kadhaa na ugaidi wa baharini vinahitaji jibu madhubuti la pamoja. Maneva haya ni fursa ya dhahabu kwa ajili ya kuratibu mifumo ya mawasiliano na rada za vikosi vya baharini vya nchi hizo tatu ambazo katika hali ya mgogoro zinaweza kufanya kazi kama mfumo mmoja wa pamoja kwa ajili ya kupashana taarifa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *