
Serikali ya Kenya imeitaka Russia iirejeshe nyumbani miili ya raia wake waliouawa na wale waliokamatwa kama wafungwa wa vita, ambao wameripotiwa kuwa walipiigania Russia katika vita na Ukraine.
Hayo yanajiri kufuatia ufichuzi wa shirika kuu la kijasusi la Kenya, ambalo lililiarifu bunge la nchi hiyo kwamba zaidi ya Wakenya 1,000 kwa sasa wanapigana upande wa Russia katika vita vya Ukraine.
Takwimu zilizotolewa na maafisa wa ujasusi wiki hii zimeonyesha kuwepo ongezeko kubwa kutoka Novemba mwaka jana, wakati Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya Musalia Mudavadi alipowafahamisha wabunge kuwa Wakenya wapatao 200 wanaipigania Russia katika mzozo huo.
Serikali ya Kenya imeelezea wasiwasi wake mkubwa kuhusu suala hilo wakati Katibu Mkuu wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo, Korir Sing’Oei, alipokutana kwa mazungumzo na Balozi wa Russia nchini humo, Vsevolod Tkachenko, jijini Nairobi.
“Wakati wa mazungumzo yetu, niliwasilisha wasiwasi mkubwa wa Serikali kuhusu raia wa Kenya walionaswa kwa sasa katika mzozo wa Russia na Ukraine,” ameeleza Sing’Oei katika taarifa baada ya mkutano huo uliofanyika jana Ijumaa.
“Nilitoa wito wa kufikiwa kibalozi raia wetu bila vikwazo na kutafuta itifaki zilizo wazi na za uwazi kuhusu kurejeshwa nyumbani wafungwa wa vita na mabaki ya marehemu,” amebainisha afisa huyo wa wizara ya mambo ya nje ya Kenya.
Dk. Sing’Oei amesema: “Kipaumbele chetu ni usalama na heshima ya kila Mkenya aliyeko nje ya nchi. Nilithamini ushirikiano wa ubalozi katika kuzuia uajiri haramu wa Wakenya”.
Siku ya Alkhamisi, serikali ya Moscow ilikanusha madai kwamba, iliwaandikisha Wakenya kupigana nchini Ukraine.
Hayo yanaripotiwa huku serikali kote barani Afrika na Asia zikiwa hapo awali zimewaonya raia wao dhidi ya kujiunga na mzozo huo, na kuonya juu ya athari zinazoweza kutokea za kisheria, kidiplomasia na kiusalama.
Nchi za Afrika, ikiwa ni pamoja na Nigeria, Kenya na Afrika Kusini, zimeonyesha wasiwasi juu ya hatima ya raia wao walioajiriwa na Moscow.
Mnamo mwezi Novemba mwaka jana, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine, Andriy Sybiga, alidai kwamba kwa akali, raia 1,436 kutoka nchi 36 za Afrika walitambuliwa miongoni mwa vikosi vya Russia…/