SHINYANGA: WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana, Dk Joel Nanauka amezindua rasmi Jukwaa la Vijana la Mkoa wa Shinyanga litakalowakutanisha na kuwashirikisha vijana pamoja ili kujadili fursa za kiuchumi na namna wanavyoweza kuzitekeleza ili kuleta maendeleo.
Akizindua jukwaa hilo leo Februari 21, 2026, DkNanauka amesema jukwaa hili ni sehemu ya utekelezaji wa Sera ya Maendeleo ya Vijana iliyoboreshwa ya Mwaka 2024 lakini pia linaendana na Maono ya Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 inayolenga kuwafanya vijana kuwa kitovu cha ubunifu ili kuwawezesha kiuchumi na kuleta maendeleo.
“Jukwaa hili linafungua ukurasa mpya wa uwezeshaji wa vijana kiuchumi kwa kuendana na Sera ya Maendeleo ya Vijana ya 2024 na maono ya Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 ya kuwafanya vijana kuwa kitovu cha ubunifu na maendeleo,” amesema Dk Nanauka.
Aidha ameongeza kuwa kupitia jukwaa hili litaimarisha mawasiliano kati ya Serikali na Vijana pamoja na kutoa mikopo isiyo na riba ili kuwawezesha vijana kiuchumi huku akiwataka vijana kushiriki kikamili katika jukwaa hili na kuongeza ubunifu.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mboni Mhita amesema Serikali ya Mkoa inaendelea kuweka mazingira rafiki kwa wajasiriamali vijana kwa kuendesha mazoezi mbalimbali kama vile kusajili wajasiriamali wadogo wadogo ambapo jumla ya wafanyabishara 2453 wamesajiliwa, pamoja na utoaji wa mikopo ya asilimia 10 ambapo kwa mwaka 2025/2026 jumla ya shilingi bilioni 1 zimekopeshwa kwenye vikundi 98.
Aidha Mhita amewataka vijana kutumia jukwaa hili kuwa mwanzo wa mapinduzi ya kifikra kwa kujiimarisha kiuchumi na kujenga mitandao ya kibiashara na kubadilisha uzoefu kwa maendeleo endelevu.
Mhita amesema kwa kutambua vijana ni rasilimali muhimu katika kuleta maendeleo ya kiuchumi na kijamii, Mkoa wa Shinyanga kupitia halmashauri zake 6 umetenga maeneo maalumu kwa ajili ya kujenga viwanda vidogo vidogo vitakavyowainua vijana kiuchumi.
Ikumbukwe kuwa Januari 10, 2026 Jukwaa la Vijana lilizinduliwa rasmi mkoani Dar es Salaam na Shinyanga ni mkoa wa 3 kwa jukwaa la vijana kuzinduliwa ambapo kwa takwimu za sensa za mwaka 2022 inaonesha mkoa una jumla ya vijana 697,756.