
Hai. Wananchi wa Kijiji cha Mbatakero, kata ya Weruweru, Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro wameishukuru Serikali kwa kuwajengea shule ya sekondari Mbatakero ambapo wanafunzi walikuwa wakitembea zaidi ya kilomita 18 kila siku kwenda kufuata shule maeneo ya jirani.
Shule hiyo ambayo imewekwa jiwe la msingi na kuzinduliwa leo Jumamosi Februari 21, 2026 na Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba, ina jumla ya wanafunzi 94 na imegharimu zaidi ya Sh584 milioni hadi kukamilika kwake.
Wakizungumza hilo, wananchi wa kijiji hicho, wamesema watoto walikuwa wakishindwa kumaliza shule kutokana na umbali mrefu na baadhi yao kurubuniwa kwa kupewa lifti na madereva bodaboda ambao mwisho wa siku huishia kuacha shule kutokana na ujauzito.
Sabina Kilenga, mmoja wananchi wa kijiji hicho, amesema awali baadhi ya wanafunzi wa kike kijijini hapo walikuwa wakishindwa kumaliza shule kutokana na changamoto ya kutembea umbali mrefu na baadhi yao kuacha shule kutokana na kubeba ujauzito kwa kurubuniwa na madereva bodaboda.
“Kijijini hapa tulikuwa tunapata mateso sana ya watoto kusoma kwa sababu watoto walikuwa wanatoka hapa kwenda shule ya mbali sana, watoto wa kike walikuwa wanateseka wengine wanabeba mimba kabla ya kumaliza shule kutokana na kurubuniwa,” amesema.
Aidha, amesema kutokana na umbali huo, wakati mwingine mwanafunzi anakua amechoka na hata anapoingia darasani hamwelewi mwalimu kwa kuwa ametembea umbali mrefu.
“Tunamshukuru Mungu kupata hii shule ya Mbatakero, tunamwambia Mungu asante, tunaishukuru sana Serikali kwa sababu watoto wetu wa kike walikuwa wakipata sana changamoto.
“Ukiangalia huku hakuna usafiri zaidi ya kutembea kwa miguu na njiani unakuta watoto wa kike wanapewa lifti, wanadanganyika barabarani, kwa hiyo watoto wengi hawamalizi shule,” amesema mwananchi huyo.
Kwa upande wake, mkazi mwingine wa kijiji hicho, Saida Mandai, mkazi wa Kijiji cha Ngusero, amesema kutokana na kwamba shule ilikuwa mbali wazazi walikuwa wakiacha shughuli zao kuwasindikiza watoto wao kwa kuwa walikuwa wakiamka mapema na kwenda shule na giza, hali ambayo ilikuwa ikiwapa wazazi hofu.
“Watoto wetu walikuwa wanatoka hapa Mbatakero wanakwenda kusomea kata ya Machame, walikuwa wanatembea umbali mrefu, wakati mwingine wanakata tamaa, akiingia kidato cha kwanza, cha pili haendelei tena anaacha shule kutokana na changamoto wanazokutana nazo njiani,” amesema mwananchi huyo.
Akitoa taarifa ya ujenzi wa shule hiyo mbele ya Waziri Mkuu, Mhandisi wa Halmashauri hiyo, Anord Matandiko amesema ujenzi wa shule hiyo iliyogharimu zaidi ya Sh584 milioni, itasaidia kupunguza changamoto ya wanafunzi kutembea umbali mrefu.
“Mwaka 2024 tulipokea fedha Sh584.2 milioni kwa ajili ya ujenzi wa mradi huu ambapo kwa sasa shule hii ina wanafunzi wa kidato cha kwanza 94 na walimu 11 na katika ujenzi huu tumeokoa Sh4.3 milioni,” amesema Matandiko.
Aidha, amesema ujenzi wa mradi huo wa shule utasaidia kuwapa fursa wananachi wanaomaliza darasa la saba katika kijiji hicho kuendelea na shule kijijini humo na kumaliza adha ya wanafunzi kutembea zaidi ya kilomita 18.
“Faida ya mradi huu kutawapa fursa wanafunzi wote waliomaliza shule ya msingi, waliokuwa wanatembea umbali mrefu zaidi ya kilomita 18 kwenda na kurudi,” amesema Matandiko.
Naye Mbunge wa Hai (CCM), Saashisha Mafuwe ameishukuru Serikali kwa kuona umuhimu wa kujenga shule hiyo kwa kuwa wanafunzi walikuwa wakipata changamoto ya kutembea umbali mrefu.
“Watoto walikuwa wanatembea kilomita 19 kwenda na kurudi, kwa kweli tunaishukuru sana Serikali kwa kutujengea shule hii ambayo itakuwa ni msaada mkubwa kwa wananchi wa eneo hili,” amesema Mafuwe.
Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amesema kwa kutambua umuhimu wa shule hiyo kwa wanafunzi wanaosoma katika shule hiyo, Serikali imeona namna ya kuifanya kuwa shule ya amali.
“Mkoa wa Kilimanjaro una shule za amali tano, na kwenye hii shule kuna uwezekano wa kubadilisha kuwa shule ya amali,” amesema Profesa Mkenda.
Akizungumzia mafanikio ya elimu, Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba amesema Serikali imetenga zaidi ya shule za Sekondari 1,300 ili kuwarithisha wanafunzi wa Kitanzania elimu bora.
“Ni mateso sana kwa mtoto kutembea kilomita 18 kila siku, kwa ujumla ndani ya kipindi cha miaka mine, Rais Samia Suluhu Hassan amejenga zaidi ya shule 1300 za sekondari, hii ni kazi kubwa ambayo Rais amewapa utithi watoto wa Kitanzania,” amesema Dk Mwigulu.