
Matamshi ya balozi wa Marekani katika utawala wa kizayuni wa Israel Mike Huckabee kwamba utawala huo ghasibu una haki ya kupanua eneo lake kwa kupora eneo kubwa la Mashariki ya Kati la nchi kadhaa za Kiarabu na Kiislamu za eneo hilo yamekosolewa na kulaaniwa vikali na nchi hizo, Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu, OIC, Jumuiya ya Waarabu na makundi ya ukombozi wa Palestina.
Huckabee alitoa matamshi hayo wakati wa mahojiano na mchambuzi wa habari wa Marekani Tucker Carlson, yaliyotangazwa siku ya Ijumaa, alipokuwa akitilia mkazo suala la mipaka ya kijiografia ya utawala wa kizayuni.
Eneo hilo alilopendekeza balozi wa huyo wa Marekani ni Lebanon ya sasa, Syria, Jordan na sehemu kadhaa za Saudi Arabia.
Itakumbukwa kuwa, mnamo mwaka 2008 Huckabee alifikia hatua hata ya kuhoji utambulisho wa Palestina aliposema, “kiuhakika hakuna kitu kama Mpalestina.”
Matamshi aliyotoa Huckabee siku ya Ijumaa yameibua mjibizo wa haraka wa kukosoa na kulaani kutoka nchi za Misri na Jordan, Saudi Arabia, Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu, OIC, Jumuiya ya Waarabu na makundi ya ukombozi wa Palestina.
Wizara ya mambo ya nje ya Saudi Arabia ilielezea maoni ya Huckabee kuwa ni “maneno ya msimamo mkali” na “yasiyokubalika”, na ikaitaka wizara ya mambo ya nje ya Marekani itoe ufafanuzi.
Wizara ya mambo ya nje ya Misri imeyaita matamshi hayo “ukiukwaji mkubwa wa sheria za kimataifa”, ikiongeza kwamba “Israeli haina mamlaka juu ya eneo la Palestina linalokaliwa au ardhi nyingine za Kiarabu.”
Wizara ya mambo ya nje ya Jordan imeyatoa maanani matamshi ya Huckabee kwa kuyaita “ya kipuuzi na kichochezi,” yanayokiuka kanuni za kidiplomasia na “ukiukaji wa mamlaka ya kujitawala ya nchi za eneo hili”.
Wakati huohuo, Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS, imelaani matamshi ya balozi wa US katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu zilizopachikwa jina bandia la Israel ikisema yanaakisi mawazo ya kikoloni na kuonyesha jinsi Washington inavyoafikiana na miradi ya “udhibti na uunganishaji wa ardhi unaofanywa na utawala wa Kizayuni”.
Taarifa iliyotolewa na Hamas imesema matamshi ya Mike Huckabee ni “mfano dhahiri wa mawazo ya kikoloni ambao ndio msingi wa kuasisiwa vuguvugu la Kizayuni.”
Hamas imesema, matamshi hayo “yanafichua kiwango cha upendeleo wa wazi wa Marekani kwa miradi ya Israel ya udhibiti na unyakuzi wa ardhi, ambao ni ukiukaji mkubwa wa sheria za kimataifa na Mkataba wa Umoja wa Mataifa, na dharau kwa uhuru wa nchi za eneo na haki za watu wao.”
Baadhi ya wanasiasa wa Israel, akiwemo waziri mkuu wake Benjamin Netanyahu, wametangaza hadharani uungaji mkono wao kwa wazo la uwepo wa “Israel Kubwa” yenye mipaka iliyopanuliwa.
Katika mahojiano ya televisheni aliyofanyiwa mwaka uliopita wa 2025, Netanyahu alisema anaunga mkono maono hayo, akiyaelezea kuwa ni “misheni ya kihistoria na ya kiroho” na kuthibitisha kufungamana kwake na maono ya kile kinachoitwa “Ardhi Iliyoahidiwa”…/