Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Haki za Binadamu, Volker Türk, ameonya kuwa bila kuweka mifumo madhubuti ya udhibiti kwa haraka, akili mnemba (AI) inaweza kuongeza pengo la usawa, kuimarisha upendeleo na kusababisha madhara halisi katika jamii.

Türk amesema hayo katika mahojiano kando ya Mkutano wa Athari za Akili Mnemba ambao umemalizika jijini New Delhi, nchini India Jumamosi Februari 21. Ameongeza kuwa teknolojia hiyo inapaswa kuongozwa na mfumo wa haki za binadamu unaohakikisha uwazi, uwajibikaji na ushirikishwaji.

Amesema mashirika ya kiteknolojia yanapaswa kuwajibishwa yafanya tathmini ya athari kwa haki za binadamu wanapozibuni, kuzisambaza na kuziuza.

Ameongeza kuwa kwa muda sasa tumeshuhudia baadhi ya kampuni zikiwa na bajeti kubwa kuliko hata nchi ndogo.

Afisa huyo wa Umoja wa Mataifa amesema: “Ukiweza kudhibiti teknolojia si tu katika nchi yako bali duniani kote, unakuwa na nguvu kubwa. Unaweza kuitumia kwa mema, kama kusaidia sekta ya afya, elimu na maendeleo endelevu, lakini pia kwa mabaya, kama silaha zinazojiendesha zenyewe, kusambaza taarifa potofu, chuki na dhuluma.”

Aidha amesema anatumai kutakuwa na maendeleo jumuishi ya akili mnemba, ambapo nguvu haitakuwa mikononi mwa kampuni chache tu Amerika Kaskazini, na ambapo maendeleo ya akili mnemba yataakisi utajiri na utofauti wa kila jamii.

Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Haki za Binadamu amebainisha matarjio yake kuwa akili mnemba itaweza kutatua changamoto nyingi za dunia ya leo,  kama janga la tabianchi, upatikanaji wa huduma za afya na elimu kwa wote. 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *