
Nyota wa kimataifa wa riadha wa Tanzania, Gabriel Geay amefanya kweli katika Mbio za Daegu Marathon 2026 kwa kutetea ubingwa wa mbio hizo kwa mara ya pili mfululizo zilizofanyika asubuhi ya jana Korea Kusini.
Geay alimaliza akiwa nafasi ya kwanza akiwa sambamba na Muethiopia Chimdesa Gudeta kila mmoja akitumia muda wa saa 2:08:08, huku Mtanzania mwingine Emmaneul Dinday akimaliza wa tatu kwa muda wa 2:08:16.
Ushindi huo umemfanya Geay kuvuna Dola 200,000 (zaidi ya Sh 514 milioni) na medali ya dhahabu, huku Dinday akipata Dola 45,000 (Sh 115 milioni) na medali ya shaba, wakati mshindi wa pili akizoa Dola 80,000 na medali ya fedha.
Hii ni mara ya pili kwa Geay kufanya kweli katika mbio hizo za Daegu kwani mwaka uliopita aliandika rekodi kwa kutumia muda wa saa 2:05:22 na kuzoa medali ya dhahabu pamoja na kitita cha fedha mbele ya Addidu Gobena pia wa Ethiopia.
Katika mbio hizo za jana Jumapili, Geay na Chimdesa walikuwa wakichuana ng’adu kwa ng’adu tangu mwanzo na haikushangaza kumaliza ndani ya muda sawa, japo Mtanzania huyo aliyekuwa wa kwanza kugusa mstari kuliko mwenzake na kunyakua medali ya dhahabu na mpinzani wake kunyakua medali ya fedha.