London, England. Kocha wa Chelsea, Liam Rosenior, amewashukia baadhi ya wachezaji wake kufuatia sare dhidi ya Burnley, akifichua kuwa mchezaji mmoja alishindwa kutekeleza majukumu yake ya kumkaba mpinzani, jambo lililosababisha bao la kusawazisha.

Burnley walisawazisha katika Uwanja wa Stamford Bridge baada ya mshambuliaji wao Mholanzi, Zian Flemming, kuachwa peke yake na kufunga kwa kichwa kufuatia kona iliyopigwa na James Ward-Prowse.

Tukio hilo limetokea licha ya Rosenior kufanya mabadiliko ya kuongeza mabeki warefu, akiwemo Jos Acheampong na Mamadou Sarr, baada ya Wesley Fofana kutolewa kwa kadi nyekundu.

Akizungumza kwa hasira baada ya mechi, Rosenior amesema kulikuwa na jukumu lililokosekana katika safu ya ulinzi.

“Kazi ya ulinzi haikufanyika. Tulijua Flemming ndiye mchezaji wao bora wa kupiga vichwa. Kulikuwa na mchezaji tuliyempa jukumu hilo, lakini alimlinda mtu asiye sahihi,” amesema Rosenior, huku akikataa kumtaja mhusika hadharani.

Kocha huyo amesisitiza kuwa hataki kuwatupa wachezaji wake mbele ya vyombo vya habari, akiahidi kulishughulikia suala hilo ndani ya timu wiki ijayo.

Mbali na kosa hilo, Rosenior amekosoa pia ukosefu wa umakini na uwajibikaji kwa baadhi ya nyota wake katika nyakati za presha.

“Kuna matukio mengi tunaruhusu mabao kutokana na kukosa umakini na uwajibikaji. Unahitaji wachezaji unaoweza kuwategemea katika nyakati ngumu. Hili si jambo la kiwango cha klabu kama Chelsea,” amesema.

Chelsea walikuwa na mabeki sita uwanjani baada ya Fofana kutolewa kwa kadi nyekundu, wakiwemo mabeki wa kati wanne, lakini bado walishindwa kuzuia. Rosenior ameeleza kuwa mpango wake ulikuwa wazi akiamini njia pekee ambayo Burnley wangeweza kufunga ilikuwa kupitia mipira ya adhabu.

“Nilijaribu kuongeza uimara. Tulikuwa na wachezaji wa kutosha kukabiliana na hali ile, lakini hatukufanya hivyo. Hii imetugharimu pointi mbili,” amesema.

Mashabiki wa Chelsea walionyesha kutoridhishwa na matokeo hayo na kuanza kuzomea kocha huyo baada ya filimbi ya mwisho.

Kwa upande wa Burnley, kocha Scott Parker amewapongeza wachezaji wake kwa kupambana hadi mwisho.

“Tumeingia katika ligi hii kubwa na wakati mwingine tumekuwa chini ya kiwango, lakini hatujapungukiwa na moyo wa kupambana. Presha imekuwa kubwa, lakini tumeonyesha uimara,” amesema Parker.

Amemsifia pia Ward-Prowse kwa ubora wake katika mipira ya adhabu.

“Unaweza kuwa na makocha bora wa mipira ya adhabu, lakini mwisho wa siku unahitaji mpira uende mahali sahihi. Ward-Prowse anafanya hivyo mara kwa mara,” ameongeza.

Sare hiyo inaongeza presha kwa Rosenior, huku macho yakielekezwa kuona namna Chelsea watakavyojirekebisha katika mechi zijazo huku ikitarajiwa kutupa karata yake nyingine kwenye Ligi Kuu dhidi ya Arsenal Machi Mosi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *