
Kundi la mawakili wanaowakilisha jamii za Kongo limetangaza mipango ya kufungua kesi katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) kuhusu madai ya utakaso wa kikabila na uhalifu dhidi ya ubinadamu uliofanywa dhidi ya makundi kutoka jamii ya walio wachache ya Banyamulenge, Hema na Watutsi.
Imechapishwa:
Dakika 2 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Katika taarifa ya tarehe 17 Juni, kundi la mawakili hao ulisema unakusanya ushuhuda wa mashahidi kuhusiana na shughuli za kijeshi huko Minembwe, Kivu Kusini, ambapo vurugu zimeongezeka katika miaka ya hivi karibuni.
“Kundi hili la mawakili linafanya kazi katika ukusanyaji wa ushahidi kuhusu shughuli za kijeshi zinazohusisha mamashambulizi dhidi ya raia katika nyanda za juu za Minembwe huko Kivu Kusini,” mawakili walisema.
Kundi hilo lilisema ushahidi huo unajumuisha picha, video na ushuhuda uliokusanywa kutoka kwa waathiriwa na mashahidi, ambao linakusudia kuwasilisha mbele ya ICC.
“Picha, video na ushuhuda mwingi upo. Vitendo hivi vya utakaso wa kikabila vinajumuisha uhalifu dhidi ya ubinadamu ,” taarifa inaelezea.
Waliotia saini ni pamoja na mawakili Amedeo Kamoto wa Bukavu, Bernard Maingain, wakili mwenye makao yake Brussels na mwanachama wa Baraza la ICC, Léon Lef Forster, wakili mwenye makao yake Paris, na Innocent Nteziryayo, mratibu wa kundi hilo.
Walisema walichukua hatua hiyo kutokana na taarifa walizopokea kutoka kwa wakazi, raia wa Banyamulenge ambao wanaendelea kuripoti mashambulizi dhidi ya raia katika eneo hilo.
“Mkakati wa mashambulizi ya ambomu yanayolenga watu una athari mbaya,” walisema.
Mawasilisho yaliyopangwa yanawakilisha jaribio la hivi karibuni la kutafuta uwajibikaji wa kimataifa kwa vurugu ambazo zimeharibu Minembwe, eneo katika mkoa wa Kivu Kusini linalokaliwa zaidi na Banyamulenge.
Kwa miongo kadhaa, Banyamulenge wamekabiliwa na mateso ya mara kwa mara, kuhamishwa na migogoro kuhusu uraia wao licha ya uwepo wao wa muda mrefu mashariki mwa Kongo. Tangu 2017, jamii hiyo imepitia mashambulizi ya mara kwa mara yanayotekelezwa na makundi yenye silaha, na kusababisha uharibifu wa vijiji, upotevu wa mifugo, mauaji na raia kuhamishwa kwa wingi.
Mgogoro huo ulizidi kuwa mbaya katika miaka ya hivi karibuni huku Minembwe ikijikuta katika migogoro mipana inayohusisha wanamgambo wa ndani, vikosi vinavyoungwa mkono na serikali na makundi ya kigeni yenye silaha. Viongozi wa jamii na watetezi wa haki za binadamu mara nyingi wamekuwa wakiwashutumu wanajeshi wa serikali na wahusika wengine wenye silaha kwa kuwalenga raia kwa sababu ya utambulisho wao wa kikabila.