MABAO mawili ya kiungo mshambuliaji wa Azam FC, Idd Seleman ‘Nado’, dhidi ya KMC, yametosha kuipa timu hiyo ushindi wa 2-0, katika mechi ya Ligi Kuu Bara, huku kikosi hicho cha Kinondoni, jijini Dar es Salaam kikiendeleza mwenendo mbovu.

Mechi hiyo iliyopigwa leo Februari 22, 2026 kwenye Uwanja wa KMC Complex jijini Dar es Salaam, Nado alianza kufungua ukurasa wa mabao dakika ya 55, baada ya kupiga mpira wa frii-kiki ya moja kwa moja, uliomshinda kipa wa KMC FC, Mrundi, Fabien Mutombora.

Bao la pili la nyota huyo, alilifunga dakika ya 65, akipiga mpira wa moja kwa moja uliotokana na kona fupi iliyochongwa na kiungo mshambuliaji wa kikosi hicho, Feisal Salum ‘Fei Toto’, kisha kuzama wavuni na kuzidisha maumivu kwa timu hiyo.

Mechi ya leo ni ya tisa kwa Azam msimu huu katika Ligi Kuu, ambapo kati ya hizo imeshinda tano na kutoka sare nne, ikiwa nafasi ya nane na pointi 19, huku ikifunga mabao 13 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara mbili.

Kwa upande wa KMC, inaendelea kuburuza mkia na pointi nane, baada ya kikosi hicho kushinda mechi mbili tu msimu huu, sare mbili na kupoteza 12, kati ya 16, jambo linaloiweka katika nafasi mbaya zaidi ya kujinasua kushuka daraja.

Pia, kocha wa timu hiyo, Abdallah Mohamed ‘Baresi’, ameendeleza rekodi mbaya tangu alipojiunga na kikosi hicho, Desemba 30, 2025, akichukua nafasi ya Mbrazil Marcio Maximo, aliyeondoka, Desemba 6, 2025, kutokana na mwenendo mbaya msimu huu.

Tangu Baresi akabidhiwe kikosi hicho, Desemba 30, 2025, amekiongoza katika mechi saba za Ligi Kuu Bara, kati ya hizo ameshinda moja tu kwa bao 1-0 dhidi ya Mashujaa, Februari 3, 2026, akitoa sare moja na kuchapwa mara tano.

Kwa msimu wa 2025-2026, Maximo aliiongoza KMC katika jumla ya mechi tisa za Ligi Kuu, kati ya hizo alishinda moja tu, sare moja na kuchapwa saba, huku kikosi hicho kikifunga mabao mawili na kuruhusu 14, akikiacha mkiani na pointi nne.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *