
KOCHA wa kikosi cha Timu ya Taifa ya Wanawake ‘Twiga Stars’, Bakari Shime ameita majina 34 ya wachezaji watakaoingia kambini hivi karibuni kujiandaa na mashindano ya Fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (WAFCON) na jina la supastaa wa Al Nassr, Clara Luvanga akiwemo.
Katika majina hayo 34, jina la Clara limejumuishwa kwenye kikosi hicho ikiwa ni siku chache baada ya mshambuliaji huyo kukosekana kwenye mechi mbili za kimataifa za kirafiki za Twiga Stars dhidi ya Malawi.
Ndani ya misimu mitatu nyota huyo alikuwa miongoni mwa wachezaji muhimu wa Al Nassr, akiongoza safu ya ushambuliaji ya timu hiyo na kuendelea kuthibitisha uwezo wake wa kufunga mabao katika Ligi Kuu ya Wanawake nchini Saudi Arabia.
Msimu wake wa kwanza 2024/25, alifunga mabao 11 na asisti saba, msimu uliofuata alifunga mabao 21 na asisti saba na msimu huu alimaliza mfungaji bora akiwa na mabao 24.
Licha ya mafanikio hayo, mara kadhaa amekuwa akiachwa kwenye kikosi cha Twiga Stars au kuitwa na kushuhudia akianza mechi akiwa benchi, hali inayowafanya mashabiki wengi kuamini bado hajapata nafasi inayolingana na kiwango anachoonyesha klabuni.
Katika kikosi hicho kilichotangazwa na Shime, wapo pia nyota wanaocheza nje ya nchi akiwemo Julietha Singano (Juarez ya Mexico), Opah Clement wa Eibar ya Hispania, Diana Lucas wa Trabzonspor ya Uturuki, Noela Luhala wa MFA Žalgiris ya Lithuania pamoja na Enekia Kasonga anayekipiga Gallos Femenil ya nchini Mexico.
Kwa wachezaji wa ndani Makipa Najiath Abbas (JKT Queens)
Nusra Hamis (Fountain Gate Princess),Janeth Shija (Simba Queens) Mabeki ni Asha Omary (Simba Queens),Ester Mabanza (Yanga Princess),Diana Mnaly (Yanga Princess)
Donisia Minja (JKT Queens),Fatuma Issa (Simba Queens)
Anastazia Katunzi (JKT Queens) na Ester Maseke (JKT Queens).
Viungo ni Elizabeth Chenge (JKT Queens),Stumai Abdallah (JKT Queens),Marry Siyame (Fountain Gate Princess),Veronica Mapunda (Mashujaa Queens),Elizabeth Joseph (JKT Queens)
Aliya Fikiri (JKT Queens),Bahati Steven (Bunda Queens)
Rehema Ramadhani (Fountain Gate Princess),Anastazia Shau (JKT Queens),Winfrida Charles (Fountain Gate Princess)
na Asha Mlangwa (JKT Queens)
Wengine ni washambuliaji Edna Makamba (Tausi FC)
Aisha Mnunka (Simba Queens) na Elizabeth Joseph (Simba Queens).
Macho ya wengi kwa sasa yatakuwa kwa Clara kuona kama safari hii atapewa nafasi ya kucheza na kuonyesha uwezo wake akiwa na jezi ya taifa.
Wakati Clara akirejea, mshambuliaji Aisha Masaka anayekipiga Brighton ya England hayupo kwenye orodha hiyo.
Kuhusu kutomjumuisha Masaka kwenye kikosi hicho Shime alisema majeraha na kutoonekana muda mrefu uwanjani kumelifanya benchi la ufundi kutokuwepo kwenye listi hiyo.
“Bado kuna changamoto kwake alipatwa na majeraha tangu Wafcon iliyopita bado tunawasiliana na madaktari wa timu yake tujue tunafanyaje lakini hatuwezi kulazimisha kuhusu afya yake,” alisema Shime
“Tumepewa maagizo kuhusu hali ya Aisha lakini tunaamini kwenye uwezo wake na tuna kambi ya muda mrefu ambayo tunaweza kumtumia kama tukipewa ruhusa.”