Riyadh, Saudi Arabia. Nahodha wa Al-Nassr, Cristiano Ronaldo, hatimaye amevunja ukimya kuhusu hatma yake katika Ligi Kuu ya Saudi Arabia kufuatia sintofahamu iliyotokana na mgomo wake wa mechi tatu.

Nyota huyo mwenye umri wa miaka 41 alirejea uwanjani wiki iliyopita na kufunga mabao mawili katika ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Al-Hazem, akiweka pembeni mjadala uliokuwa umeibuka baada ya kuonyesha kutoridhishwa na sera ya usajili wa klabu yake.

Ronaldo, anayekadiriwa kulipwa Pauni 488,000 kwa siku (Sh1.7 bilioni), alidaiwa kukerwa na kile alichoona kama klabu yake haitendewi haki na inanyanyaswa na Mfuko wa Uwekezaji wa Umma wa Saudi Arabia (PIF).

Nyota wa Al-Nassr, Cristiano Ronaldo wakati akishangilia bao katika ushindi wa 4-0 kwenye mechi ya Ligi Kuu Saudi Arabia dhidi ya Al-Hazem. Picha na Mtandao

PIF ndio inasimamia asilimia 75 ya hisa kwenye klabu nne kubwa zinazoshiriki Ligi Kuu ya Saudi Arabia ambazo ni Al Ahli, Al Nassr, Al Hilal na Al Ittihad.

Ronaldo alidai kwamba Kocha wa Al Nassr, Jorge Jesus hakupata fungu la kutosha kutoka mfuko huo kulinganisha na wapinzani wao ingawa uhamisho wa Benzema unatajwa kufadhiliwa na wawekezaji wa nje na sio PIF.

Kitendo hicho kilizua maswali kuhusu mustakabali wake katika ligi hiyo, licha ya kuwa ndiye jina kubwa na linalovutia zaidi kibiashara.

Hata hivyo, alipoulizwa kuhusu hali hiyo baada ya mechi ya Jumamosi, Ronaldo amesisitiza kuwa ana furaha Saudi Arabia.

“Nina furaha sana. Kama ninavyosema mara nyingi, mimi ni sehemu ya Saudi Arabia. Ni nchi iliyonipokea vizuri mimi, familia yangu na marafiki zangu. Nataka kuendelea hapa,” amesema.

Ameongeza kuwa lengo lake ni kuisaidia timu kubaki kileleni na kuwania ubingwa.

Nyota wa Al-Nassr, Cristiano Ronaldo wakati akipiga shuti katika mechi ya Ligi Kuu Saudi Arabia dhidi ya AlHazem. Picha na Mtandao

“Kazi yetu ni kushinda na kuweka presha kwa wapinzani wetu. Tuko katika njia sahihi. Tunacheza vizuri na tunajiamini. Mechi baada ya mechi,” amesema.

Hata hivyo, Ligi Kuu ya Saudi ilitoa tamko likionya kuwa hakuna mchezaji anayeweza kuamua masuala yanayohusu klabu yake. Taarifa hiyo ilisisitiza kuwa kila klabu inaendeshwa kwa uhuru chini ya kanuni sawa za kifedha na kiushindani.

Al-Nassr kwa sasa wanaongoza msimamo wa ligi kwa tofauti ya pointi moja, huku Ronaldo akiwa na kiu ya kutwaa ubingwa wake wa kwanza Saudi Arabia tangu ajiunge na klabu hiyo msimu wa 2022-23.

Licha ya migogoro ya hivi karibuni, mashabiki wa Al-Nassr wameendelea kumuonyesha sapoti, wakipeperusha bendera kwa heshima yake wakati alipokuwa nje ya kikosi.

Sasa macho yanaelekezwa kuona kama Ronaldo ataiongoza Al-Nassr kufikia ndoto ya ubingwa msimu huu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *