Mashambulizi ya utawala wa Israel dhidi ya Qatar yamezidisha mivutano kati ya Uturuki na Israel na kuibua uwezekano wa kutokea makabiliano ya moja kwa moja kati ya Ankara na Tel Aviv.

Kwa mujibu wa Pars Today, wachambuzi wa Kizayuni wanadai kuwa tangu kutekelezwa Operesheni ya Kimbunga cha al Aqsa ya tarehe 7 Oktoba 2023, utawala wa Kizayuni umebadilisha doktrini ya usalama wake ili kukabiliana na vitisho vyote tarajiwa dhidi yake, badala ya kuahirisha kutoa majibu. Israel katika muda wa miaka miaka miwili baada ya matukio ya Oktoba 7, imetekeleza mashambulizi mengi na ambayo hayajawahi kushuhudiwa dhidi ya nchi jirani; hatua ambayo imedhihirisha mwenendo wa kupenda uchokozi na uvamizi wa utawala huo. Hadi sasa Israel imezishambulia nchi sita za eneo la Mashariki ya Kati yaani Palestina (Gaza), Lebanon, Syria, Yemen, Iran na kisha hivi karibuni Qatar katika muda wa miaka miwili wa kujiri vita dhidi ya Gaza. Kwa hakika, mashambulizi dhidi ya Qatar ni kengele ya hatari kwa nchi kama Uturuki na Pakistan.

Aidha mashambulizi ya maneno kati ya viongozi wa utawala wa Kizayuni na Uturuki yameongezeka. Benjamin Netanyahu Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni alisema akiwa huko Baitul Muqaddas kwamba: “Tupo hapa Quds. Huu ni mji wetu. Bwana Erdogan huu si mji wenu. Huu ni  mji wetu na utaendelea kuwa mji wetu daima. Hautaganywa tena”. Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki amemjibu Netanyahu ambaye amedai kuwa Quds siku zote itabaki kuwa sehemu ya Israel kwa kusema: “Abadan hatutaruhusu mji mtukufu wa Quds uchafuliwe na mikono michafu.” Amesisitiza kuwa, kiaidiolojia Netanyahu ni kama ndugu wa Hitler.

Shambulio la karibuni dhidi ya Doha mji mkuu wa Qatar linaashiria kupanuka kwa wigo wa uvamizi wa Israel kwa nchi mpya ambazo hapo awali hazikuwa zikilengwa moja kwa moja. Kitendo hiki ambacho ni ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa kimeibua wasiwasi mkubwa katika eneo la Mashariki ya Kati. Baada ya kuwashambulia viongozi wa Hamas huko Qatar, Israel imetuma ujumbe kwa Uturuki kwamba: Kimbilio la mwisho la Hamas nchini Uturuki linaweza kuwa shabaha inayofuata. Wachambuzi wengi wa sera za nje wanaamini kuwa unachama wa Uturuki katika Muungano wa Kijeshi wa Nchi za Magharibi (Nato) hauidhaminii nchi hiyo ulinzi wowote mkabala wa mashambulizi ya Israel. 

Uchambuzi wa magazeti ya Kizayuni na hasa gazeti la Haaretz pia unaonyesha kuwa Uturuki huwenda ikawa shabaha inayofuata ya Israel kutokana na uungaji mkono wake kwa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) na kufuatia hatua yake ya kuimarisha uwepo wake wa kijeshi huko Syria. Uwezekano huu umepata nguvu kwa kuzingatia makabiliano makubwa wa pande mbili huko Syria na matamshi ya kiuhasama ya pande hizo ikiwa ni pamoja hatua ya Netanyahu ya kutambua rasmi mauaji ya halaiki ya Armenia. Uturuki ambayo ni mwanachama wa Nato imeimarisha miundombinu yake ya kijeshi ikiwemo mifumo yake ya ulinzi na kuunda silaha huku ikijiandaa kukabiliana na vitisho vya Israel. Weledi wengine wa mambo wanaamini kuwa shambulio la karibuni la Israel dhidi ya vifaa vya rada vya Uturuki nchini Syria, ambalo liliua wanajeshi kadhaa wa Uturuki, na nia ya Ankara ya kuunga mkono makundi ya kieneo dhidi ya Israel ni dalili za wazi za makabiliano hayo.

Hii ni katika hali ambayo juhudi za usuluhishi za mwezi uliopita za Jamhuri ya Azerbaijan kwa ajili ya kuzuia uwezekano wa kujiri mapigano kati ya Uturuki na Israel zilikuwa tu ni njia ya ufumbuzi wa muda na jitihada hizo zimeshindwa kutatua chanzo cha mvutano. Katika upande mwingine, kuongezeka ushirikiano kati ya Uturuki na Qatar huko Syria hasa baada ya kuenguliwa madarakani Bashar al Assad kumezidisha wasiwasi wa Israel. 

Kwa upande wa kijeshi, Israel ina teknolojia, jeshi la anga na silaha za nyuklia za hali ya juu, huku jeshi la Uturuki ambalo ni moja ya majeshi makubwa ya Nato likiwa pia na uwezo wa kuibua changamoto kuu. Juhudi za Israel za kuzuia Uturuki isiuziwe ndege za kivita aina ya F-35 zinaashiria wasiwasi ulionao Tel Aviv kuhusu kuimarika kijeshi Ankara. 

Wachambuzi wa mambo wa nchini Uturuki wanaamini kuwa hatua yoyote ya Israel ya kukiuka anga ya Uturuki itakabiliwa na jibu kali na mjibizo wa haraka kutoka Ankara. 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *