KOCHA Mkuu wa Fountain Gate, Mohamed Ismail ‘Laizer’, amesema kuwakosa wachezaji watatu waliofikia makubaliano ya kutua ndani ya kikosi hicho katika dirisha dogo la Januari 2026, ni pigo kubwa kwake, kutokana na matarajio aliyokuwa nayo.

Nyota walioshindwa kujiunga na timu hiyo katika dirisha dogo ni, mshambuliaji wa Mbeya Kwanza, Boniface Mwanjonde, winga, Tariq Mohamed Mkonga aliyetoka JKU SC ya visiwani Zanzibar na kiungo, Saleh Masoud Abdallah ‘Tumbo’ aliyetokea Pamba Jiji.

Wachezaji wote watatu, walifikia makubaliano ya kujiunga na timu hiyo na tayari walisaini mikataba ya miaka miwili kwa kila mmoja wao, ingawa dili hizo zilikufa mwishoni, baada ya Fountain Gate kupokea barua rasmi ya kufungiwa kusajili.

Akizungumza na Mwanaspoti, Laizer, amesema alikuwa na matarajio makubwa kwa wachezaji wote watatu ili wakaongeze nguvu kikosi hicho, lakini dili hizo zilishindikana, jambo lililowavunja moyo benchi lao nzima la ufundi.

“Kwa sasa tunaendelea kupambana na wachezaji waliopo, kiukweli tulitarajia mambo makubwa kwa sababu ya viwango ambavyo walikuwa navyo katika timu walizotoka, mwenendo wetu sio mzuri, hivyo, tunapaswa kuzidisha juhudi sana,” amesema Laizer.

Fountain ndio timu ambayo tangu mwaka 2026, umeanza haijaonja ladha ya ushindi katika mechi za Ligi Kuu, tangu mara ya mwisho kikosi hicho kilipoifunga Tanzania Prisons bao 1-0, kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa, Babati, Novemba 26, 2025.

Timu hii iliyohamishia makazi yake kwa sasa jijini Arusha ikiutumia Uwanja wa Sheikh Amri Abeid tangu Nov26 imecheza mechi tano imechapwa tatu na kutoka sare mbili.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *