
Algeria imelitahadharisha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwamba linakabiliwa na hatari ya kukariri kushindwa kwake mtawalia katika miaka ya nyuma kuzuia mauaji ya kimbari baada ya Marekani kwa mara ya sita kutumia kura yake ya veto kupinga azimio lililoungwa mkono na nchi 14 wanachama kati ya nchi 15 wa UNSC.
Washington imetumia kura ya turufu kuzuia kupasishwa azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linalotaka usitishwaji vita Gaza, kuwezesha ufikaji wa misaada ya kibinadamu na kuachiliwa kwa mateka.
Marekani imepinga azimio hilo la Baraza la Usalama ambalo lilitaka kuchukuliwa hatua za haraka ili kuhusiana na mauaji ya kimbari yanayoendelea kufanywa na Israel katika Ukanda wa Gaza.
Mwakilishi wa Algeria katika Umoja wa Mataifa Amar Bendjama alianza hotuba yake katika kikao cha Baraza la Usalama kwa kuwaomba radhi Wapalestina.
“Tusameheni, kwa sababu dunia inazungumza kuhusu haki lakini inawanyima haki hizo, kwa sababu Israel inakingiwa kifua na kupewa himaya, kwa sababu ina kinga; si kwa mujibu wa sheria za kimataifa, bali kutokana na upendeleo wa mfumo huu wa kimataifa. Israel inatekeleza mauaji kila siku, na hakuna kinachotokea”, amesema Mwakilishi wa Algeria katika Umoja wa Mataifa.
Amar Bendjama ametahadharisha kuwa kwa hatua hii, Baraza la Usalama linakariri historia ya huko nyuma akikumbusha mauaji ya kimbari yaliyotokea huko Rwanda mwaka 1994 na Bosnia mwaka 1995.
Marekani imetumia kura ya turufu kuzuia kupasishwa azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linalotaka usitishwaji vita Gaza, kuwezesha ufikaji wa misaada ya kibinadamu na kuachiliwa kwa mateka.
Azimio hilo ambalo rasimu yake ilianza kujadiliwa tangu mwezi uliopita wa Agosti, liliungwa mkono na wanachama wote 14 wa baraza hilo isipokuwa Marekani licha ya ripoti zote kuonyesha kuwa, hali ya kibinadamu katika Ukanda wa Gaza ni mbaya mno.