Dar es Salaam. Ndivyo tunaweza kusema kufuatia staa wa Bongofleva, Diamond Platnumz (36), kukaa muda mrefu bila kutoa albamu akivuka hata matarajio yaliyokuwa yamewekwa na baadhi ya mashabiki wake.
Diamond, mwanzilishi wa WCB Wasafi, ni miaka minane imepita tangu alipoachia albamu yake ya mwisho, ikiwa ni miaka miwili zaidi ukilinganisha na albamu yake iliyokuwa imetangulia.
Mnamo Februari 2025, mwimbaji huyo alitangaza ujio wa albamu yake ya nne ndani ya mwaka huo akisema kwa asilimia kubwa itakuwa ya Bongofleva, lakini hakutimiza ahadi hiyo.
Diamond aliyetoka kimuziki kupitia wimbo wake, Kamwambie (2009), kutoka albamu ya kwanza kwenda ya pili alipumzika kwa miaka miwili, na kutoka ya pili kwenda ya tatu alipumzika miaka sita.
Hata hivyo, kutoka hiyo ya tatu kwenda ya nne inayosubiriwa, tayari amepumzika miaka minane na haijulikani ni lini itatoka ingawa mashabiki wengi walidhani ingekuwa kama mwaka mmoja au miwili iliyopita.
Albamu yake ya mwisho ni A Boy From Tandale (2018) chini ya Universal Music Group (UMG), lakini hii ilijumuisha nyimbo zilizotoka kitambo kama Number One Remix (2014), Nana (2015) na Kadogo (2016).
Ni albamu iliyosheheni majina makubwa kama P-Square, Ne-Yo, Tiwa Savage, Vanessa Mdee, Rick Ross, Jah Prayzah, Rayvanny, Omarion, Flavour N’abania, Young Killer, Morgan Heritage, Davido na kadhalika.
Tangu hapo akakaa kimya upande wa albamu na badala yake amechagua kutoa singo moja moja, kitu ambacho ni tofauti na mastaa kama Wizkid na Burna Boy ambao kuna wakati mashabiki wanawaweka daraja moja na Diamond.
Hata hivyo, mastaa hao wa Nigeria hawajawahi kukaa miaka sita hadi minane bila kutoa albamu. Wao kila mara wanaachia albamu, na hii ni moja ya sababu ya wao kuendelea kuwika zaidi kimataifa na hata kushinda tuzo kubwa.
Wizkid, mshindi wa Grammy Awards 2021, hadi sasa ametoa albamu sita ambazo ni Superstar (2011), Ayo (2014), Sounds From the Other Side (2017), Made In Lagos (2020), More Love, Less Ego (2022) na Morayo (2024).
Naye Burna Boy ametoa albamu saba, L.I.F.E (2013), On a Spaceship (2015), Outside (2018), African Giant (2019), Twice as Tall (2020), Love, Damini (2022), I Told Them… (2023), na No Sign of Weakness (2025).
Ukiangalia mtiririko huo wa kazi zao, hakuna aliyekaa miaka minane bila kutoa albamu kama Diamond, albamu zao zinapishana kati ya mwaka mmoja hadi mitatu, na zimekuwa na matokeo mazuri katika soko.
Mathalani albamu ya Wizkid, Made In Lagos (2020) ilichaguliwa kuwania Grammy, nayo ya Burna Boy, Twice as Tall (2020) ilishinda Grammy 2021, ikiwa ni baada ya ile ya nyuma yake kuwania ila haikupata ushindi.
Pengine Diamond, mkali wa kibao cha Komasava (2024), angekuwa amepiga hatua kubwa zaidi kimuziki upande wa kimataifa kama angetoa albamu nyingine walau tatu zenye uzito sawa au zaidi ya A Boy From Tandale.
Lakini, inavyoonekana hajataka kufanya hivyo tena au hana nguvu hiyo kwa sasa, na labda ndiyo sababu badala ya kutoa albamu aliamua kuja na Extended Playlist (EP), First of All (2022) yenye nyimbo 10.
First of All (2022) au FOA kama wengi wanavyoiita, ni EP iliyochanganya ladha mbalimbali za muziki wa Afrika kama Bongofleva, Afrobeats, Soukous, Amapiano na Zouk.
EP hiyo hiyo iliwashirikisha Focalistic, Pabi Cooper, Zuchu, Mbosso, Jaywillz na Adekunle Gold. Wengi wa wasanii hao, wamezidiwa vitu vingi ukilinganisha na wale waliokuwapo katika albamu ya A Boy From Tandale.
“Lengo langu kuu ni kuonyesha jinsi Afrika ilivyobarikiwa kwa vipaji. Sikutaka kujifungia sehemu moja tu, kwa sababu muziki unahusu mapenzi, maisha, sherehe na hata unaweza kukufanya ulie,” Diamond aliiambia Apple Music wakati huo.
Lakini, mashabiki wengi walikosoa hatua hiyo ya Diamond kutoa EP wakidai kwa daraja alilopo kimuziki alipaswa kufanya zaidi ya hapo! Hata hivyo, yeye alijitetea kuwa huo ni utangulizi wa albamu, ambayo hadi sasa haijatoka.
Diamond, mshindi wa tuzo tatu za MTV Europe Music Awards (MTV EMAs), albamu zake mbili za mwanzo ni Kamwambie (2010), Lala Salama (2012) iliyokuwa na nyimbo maarufu kama Moyo Wangu, Mawazo na kadhalika.
Ikumbukwe kwa mwaka uliopita baadhi ya wasanii wa Bongofleva waliotoa albamu ni Darassa (Take Away The Pain), Jay Melody (Addiction), Lady Jaydee (Silver), Moni Centrozone (Watoto wa Mtaani) na kadhalika.
Kwa upande wa EP kulikuwa na Nedy Music (The Voice of The Island), Lava Lava (Time), Yammi (After All), Phina (Melanin Therapy), Jux (A Day To Remember), Mbosso (Room Number 3) na kadhalika.