London, England. Kocha wa Arsenal, Mikel Arteta, amesema ushindi mnono wa mabao 4-1 dhidi ya Tottenham Hotspur, ni hatua ya mabadiliko katika mbio za ubingwa wa Ligi Kuu England.
Ushindi huo katika dabi ya Kaskazini mwa London umeifanya Arsenal kujitanua kwa pointi tano kileleni, mbele ya mabingwa watetezi Manchester City.
Arteta, amekuwa na hisia kali baada ya mchezo huo, akiwajibu waliokuwa wameanza kuwakosoa wachezaji wake kufuatia sare dhidi ya Wolves wiki iliyopita.
Baadhi ya wachezaji wa Arsenal katika mechi ya Ligi Kuu England ambayo wameibuka na ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya Tottenham. Picha na Mtandao
“Siwezi kujivunia na kufurahia zaidi ya hapa. Siyo tu kwa mechi hii, bali namna tulivyoishi saa 72 zilizopita. Ilikuwa ngumu sana baada ya Wolves. Hakuna maelezo ya kueleza tulivyodondosha ule mchezo,” amesema Arteta.
Ameongeza kuwa walihisi hasira, huzuni na aibu, lakini waliamua kuutumia wakati huo kama chachu ya mabadiliko.
“Tuliamua kuifanya iwe hatua ya mabadiliko. Hii ni zaidi ya kazi, ni mapenzi yetu, ni kusudi letu,” amesema.
“Tumeonyesha sisi ni wa aina gani, lakini lazima uonyeshe tena na tena. Safari ya milima na mabonde haiwezekani katika mbio za ubingwa,” amesisitiza.
Katika ushindi huo, Eberechi Eze alifunga mabao mawili sawa na mshambuliaji, Viktor Gyokeres akipachika mawili pia, na kuwaacha Spurs wakiwa pointi nne tu juu ya mstari wa kushuka daraja.
Kiungo mshambuliaji wa Arsenal, Eberechi Eze akishangilia moja ya bao alilofunga katika ushindi wa 4-1 iliyopata timu yake katika mechi ya Ligi Kuu England dhidi ya Spurs Jumapili, Februari 22, 2026. Picha na Mtandao
Arteta amefichua kuwa Eze alikuwa amekasirika baada ya kutolewa katika sare dhidi ya Brentford na kuachwa benchi dhidi ya Wolves.
“Alikuwa amenikasirikia, lakini unatakiwa kuonyesha ubora wako pale inapohitajika zaidi. Watu wanapokutilia shaka, simama na ujibu na ndivyo alivyofanya,” amesema.
Kwa upande wa Tottenham, kocha wa muda Igor Tudor amekiri wazi kuwa pengo kati ya timu hizo lilikuwa kubwa mno.
Kocha wa muda wa Tottenham, Igor Tudor akionekana kusikitika baada ya timu yake kukubali kipigo cha mabao 4-1 nyumbani dhidi ya Arsenal katika Ligi Kuu England. Picha na Mtandao
“Kulikuwa na tofauti kubwa sana kati ya timu hizi mbili. Ni vizuri kujua tulipo. Hii inaonyesha uhalisia,” amesema Tudor.
Ameongeza kuwa klabu ipo katika hali ya dharura na sasa wanapaswa kuwa wanyenyekevu, kufanya kazi kwa bidii na kubadili tabia pamoja na mtazamo wao kama timu.
“Dawa ni kujiangalia kwenye kioo na kubadili tabia. Kufanya kazi kwa bidii ndio njia pekee,” amesisitiza.
Matokeo hayo yanaifanya Arsenal kuimarisha matumaini ya ubingwa, huku Tottenham wakiendelea kusaka majibu katika msimu mgumu unaoonekana kuwatesa.