Dar es Salaam. Katika tasnia ya mitindo Tanzania, ushindani ni mkubwa na changamoto hazikosekani. Lakini miongoni mwa wanawake waliothubutu na kujenga jina linalotambulika ndani na nje ya nchi ni Khadija Mwanamboka.

Ni mbunifu wa mavazi ambaye ameigeuza ndoto yake ya utotoni kuwa harakati ya kuibeba mitindo ya Kitanzania katika majukwaa ya kimataifa.

Kwa sauti ya utulivu lakini yenye msimamo, Khadija anaanza kusimulia safari yake katika mahojiano na Mwananchi:

MWANA 01

“Nilianza kupenda ubunifu wa mavazi nikiwa mdogo sana, nilikuwa napenda kuchora michoro ya nguo na kufuatilia mitindo kutoka ndani na nje ya nchi, wakati wengine wanaona kama ni mchezo tu, mimi nilikuwa naona kama ndiyo maisha yangu ya baadaye.”

Anasema mapenzi yake kwa mitindo hayakuishia katika ndoto za utotoni, kadri alivyokua, ndivyo alivyotambua kipaji chake kinaweza kuwa chanzo cha ajira kwake na kwa wengine.

“Nilijua kabisa mitindo ni sekta yenye fursa kubwa, niliona siyo tu nafasi ya kujitegemea, bali ya kuwainua wanawake na vijana wengine wenye vipaji, ndiyo maana niliamua kuichukulia kwa uzito na kuifanya taaluma,” anasema.

MWANA 02

JUKWAA LA VIPAJI

Katika hatua ya kuthibitisha dhamira yake, Khadija alianzisha Tanzania Mitindo House, jukwaa linalolenga kusaidia wabunifu chipukizi kujitangaza na kupata nafasi ya kuonyesha kazi zao katika maonyesho makubwa.

“Nilipoanzisha Tanzania Mitindo House, lengo langu halikuwa mimi pekee kufanikiwa, nilikuwa nataka kuunda mfumo ambao utawasaidia wabunifu wengine kupata nafasi ambazo mimi nilizitafuta kwa muda mrefu,” anasema.

kutokana na jukwaa hilo, wabunifu wengi chipukizi wamepata nafasi ya kuonekana na kushiriki katika matamasha mbalimbali ya mitindo, Khadija anaamini kuwa mafanikio ya kweli ni pale unapoweza kufungua milango kwa wengine.

“Ukifanikiwa peke yako na ukasahau wengine, mafanikio hayo hayana maana kubwa, mimi naamini katika kushirikishana fursa,” anasisitiza.

MWANA 03

KUITANGAZA NCHI

Khadija ameshiriki na kuandaa matamasha kadhaa makubwa ya mitindo, ikiwemo Samia Fashion Festival na matukio yanayohusu Miss Tanzania na kutokana na majukwaa hayo, ubunifu wake umeonekana na kuthibitisha mitindo ya Kitanzania inaweza kushindana kimataifa.

“Tunao uwezo mkubwa sana hapa Tanzania, tatizo siyo ubunifu, tatizo mara nyingi ni kujiamini na kupata majukwaa sahihi, ndiyo maana nimekuwa mstari wa mbele kuhakikisha tunatengeneza majukwaa yetu wenyewe,” anasema.

Anaongeza, kila tukio analoshiriki au kuandaa huliona kama nafasi ya kuonyesha utamaduni, ubunifu na hadhi ya mwanamke wa Kitanzania, changamoto za mwanzo

Kama ilivyo kwa wengi wanaoanza safari ya ubunifu, Khadija hakuepuka changamoto.

“Changamoto zilikuwepo, hasa mwanzoni, kulikuwa na ukosefu wa mitaji, wakati mwingine watu hawakuamini uwezo wangu kwa sababu mimi ni mwanamke, lakini nilijifunza mafanikio yanahitaji uvumilivu na nidhamu ya hali ya juu,” anasema.

Anakiri kulikuwa na nyakati za kukata tamaa, lakini hakuruhusu hali hiyo imrudishe nyuma.

“Kila nilipokutana na kikwazo, nilijiambia hii ni sehemu ya safari, ukishindwa kuvumilia changamoto, huwezi kufika mbali.”

MWANA 05

MCHANGO KWA JAMII

Mbali na ubunifu wa mavazi, Khadija amejikita pia katika miradi ya kijamii, amewahi kubuni mavazi kwa ajili ya kusaidia watoto wenye mahitaji maalumu na kuwahamasisha wanawake kujiajiri kutokana na sanaa ya mavazi.

“Nimegundua mitindo inaweza kuwa zaidi ya biashara, inaweza kuwa chombo cha kubadilisha maisha, kutokana na mafunzo na matamasha, nimeona wanawake wakijiamini na kuanza kujitegemea,” anasema.

Kwa upande wake, anaamini siku ya wanawake si ya kusherehekea tu bali ya kutafakari na kuchukua hatua.

“Siku ya Wanawake ni zaidi ya sherehe, ni muda wa kujiuliza tunafanya nini kubadilisha maisha ya wanawake wengine. Kutokana na kazi yangu, ninaamini tunaweza kuleta mabadiliko makubwa.”

MWANA 06

UJUMBE KWA WANAWAKE

“Mwanamke anaweza kufanikiwa katika sekta yoyote kama atakuwa na nidhamu, uvumilivu na malengo. Usiogope kuanza kidogo, kila mafanikio makubwa yalianza na hatua ndogo,” anasema.

Leo hii, Khadija Mwanamboka anaendelea kuipeleka mitindo ya Tanzania katika majukwaa ya kimataifa huku akibaki kuwa mlezi wa vipaji vya vijana na wanawake wanaotamani kujipambanua katika ulimwengu wa ubunifu.

Safari yake ni ushahidi kuwa ndoto za utotoni zinaweza kuwa dira ya mafanikio makubwa ikiwa zitachanganywa na bidii, uthubutu na moyo wa kusaidia wengine.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *