
Mpaka wa Gatumba-Kavimvira kati ya miji ya Uvira (DRC) na Gatumba (Burundi) umefunguliwa rasmi leo Jumatatu, Februari 23, baada ya kufungwa kwa zaidi ya miezi miwili kufuatia vita vya AFC/M23. Burundi ilifunga mpake wake na DRC baada ya waasi wa AFC/M23 kukamata mji wa Uvira.
Imechapishwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Hakuna sherehe rasmi iliyofanyika kwa ajili ya ufunguzi huo; pande zote mbili zimekubaliana kuruhusu wasafiri kupita. Mkuu wa idara ya uhamiaji huko Kavimvira (DRC), baada ya mkutano na Kamishna Mkuu wa Uhamiaji wa Burundi, Bw. Maurice Mbonimpa, amebainisha kwamba “taratibu za uhamiaji ni za lazima kama kawaida (visa kwa hati muhimu)” na kwamba mpaka huo utakuwa wazi kila siku kuanzia saa 2:00 asubuhi hadi saa 11:00 jioni.
“Wale walio Burundi sasa wanaweza kuvuka salama,” taarifa ya mamlaka za uhamiaji ilifafanua.
Ni furaha tele miongoni mwa wakazi wa pande zote mbili, ambao walikuwa wamezuiwa kuvuka mpaka tangu kufungwa kwake.
“Ninaendesha biashara ndogo huko Uvira, naenda Ruvumera katika mji mkuu, Bujumbura, kununua bidhaa zangu, kisha nitarudi leo, kama kawaida. Mpaka uko wazi. Tunazishukuru mamlaka yetu na ile za Burundi kwa kusikiliza maombi yetu,” amesema mfanyabiashara mmoja wa Kongo, akinukuliwa na vyombo kadhaa vya habari.
Raia kadhaa wa Burundi wameelezea furaha yao kwa kufunguliwa kwa mpaka huu. “Kufunguliwa tena kwa mpaka ni faraja kubwa kwa wengi wetu Warundi. Maisha yetu yanategemea nchi zetu hizi ndugu na rafiki,” amesema raia mmoja wa Burundi.
Burundi ilifunga mpaka wake katika maeneo ya Gatumba mnamo Desemba 10 baada ya waasi wa AFC/M23 kuteka mji wa Uvira. Gavana wa mkoa wa Kivu Kusini, huko Uvira, Jean-Jacques Purusi Sadiki ndiye alitangaza kufunguliwa kwa mpaka huo siku ya Jumapili.