Uganda. Mwimbaji maarufu wa Uganda, Eddy Kenzo, amezua mjadala mtandaoni mwishoni mwa wiki hii baada ya kushiriki chapisho lililodai kuwa yeye ndiye Mganda maarufu zaidi nchini humo.
Madai hayo yalitoka katika ukurasa wa mitandao ya kijamii uitwao Africa First, unaojieleza kama jukwaa la kuonyesha uzuri, historia na ukweli wa Afrika.
Chapisho hilo lilikuwa na kichwa cha ‘Mtu maarufu zaidi katika kila nchi ya Afrika’ na lilitaja mtu mmoja kutoka kila nchi 54 za bara hilo.
Kwa Uganda, Kenzo alitajwa kuwa kinara, huku Diamond Platnumz akiongoza kwa Tanzania, Paul Kagame kwa Rwanda na Eliud Kipchoge kwa Kenya. Ukurasa huo ulidai kuwa vigezo vilivyotumika ni kupitia Google, umaarufu kwenye mitandao ya kijamii na ushawishi wa kimataifa.
Hata hivyo, watumiaji wa mitandao ya kijamii na baadhi ya mashabiki walihoji ukurasa huo umekosea, kwani Kenzo hana umaarufu huo wa kukaa nafasi ya kwanza Uganda.
Mmoja aliyejitambulisha kama Nantambi Namusisi aliandika; “Una uhakika taarifa hii ni ya kweli? Kenzo ni maarufu zaidi kuliko Idi Amin ndani na nje ya nchi? Amin aliacha historia ambayo itakuwa vigumu kwa Mganda yeyote kuisahau hata Museveni hawezi.”
Mtumiaji mwingine aliyejitambulisha kama Brian alihoji hadhi ya kimataifa ya msanii huyo kwa kuandika: “Cha kuchekesha ni kwamba hata ndani ya Uganda si maarufu hivyo, sasa huo umaarufu ameutoa wapi?”
Balaam, ambaye ni shabiki wa Kenzo alisema; “Mimi ni shabiki wako wa dhati, lakini hili hapana, wamekudanganya. Vigezo gani hasa vilitumika kupanga viwango hivi?” Alihoji.”
Kenzo aliyeanza muziki mwaka 2008 ameachia kazi mbalimbali zilizofanya vizuri Uganda miongoni mwao ni Body Language (2018), Signal (2019), Inabana (2019) aliyomshirikisha msanii wa Bongofleva, Harmonize.
Nje na kazi hizo Kenzo anakuwa msanii wa kwanza kutoka Uganda kuwania tuzo kubwa za muziki duniani Grammy, mwaka huu aliwania kwenye kipengele cha ‘Best African Music Performance’ ambapo Tyla kutoka Afrika Kusini aliibuka mshindi.
Pia anakuwa Mganda wa kwanza kushinda tuzo za BET kama ‘Viewer’s Choice Best New International Artist’ jambo linalomfanya kuwa moja ya wasanii wanaofanya vizuri sio tu Uganda bali Afrika Mashariki.