Shirikisho la Soka barani Ulaya (UEFA), limempa adhabu ya muda ya mechi moja kiungo wa Benfica, Gianluca Prestianni, wakati uchunguzi ukiendelea kuhusu tuhuma za kumtukana kibaguzi mshambuliaji wa Real Madrid, Vinícius Júnior.

Tukio hilo lilitokea wiki iliyopita katika mchezo wa kwanza wa mtoano wa Ligi ya Mabingwa Ulaya uliochezwa kwenye Uwanja wa da Luz, jijini Lisbon, ambapo mchezo ulisimamishwa kwa takribani dakika 10 baada ya Vinicius kumlalamikia mwamuzi kuwa ametukanwa kwa kauli ya kibaguzi.

Kwa mujibu wa taarifa ya UEFA, Kamati ya Nidhamu, Maadili na Udhibiti (CEDB) imemfungia kwa muda Prestianni kwa ukiukwaji wa awali wa Kifungu cha 14 cha Kanuni za Nidhamu kinachohusu tabia ya kibaguzi. Hatua hiyo inamfanya mchezaji huyo kuukosa mchezo wa marudiano utakaopigwa leo Santiago Bernabeu.

Baadhi ya wachezaji wa Real Madrid, wakijaribu kumtuliza nyota wa Benfica,  Gianluca Prestianni baada ya kuripotiwa kumtolea maneno ya kibaguzi mchezaji wa Madrid, Vinicius Jr. Picha na Mtandao

Kifungu hicho kinaeleza kuwa yeyote atakayethibitika kudhalilisha utu wa mtu kwa misingi ya rangi, kabila, dini au mwelekeo wa kijinsia anaweza kufungiwa angalau mechi 10 au kupewa adhabu nyingine stahiki.

Benfica wamethibitisha kupokea taarifa hiyo na kusisitiza kuwa wataikatia rufaa. Klabu hiyo imeeleza kuwa inasikitishwa na uamuzi wa kufungiwa mchezaji wao wakati uchunguzi bado unaendelea, huku ikisisitiza msimamo wake wa kupinga aina zote za ubaguzi.

Ripoti kutoka Hispania zinaeleza kuwa UEFA imechukua hatua hiyo ya haraka kwa hofu ya kuepusha tukio jingine la mzozo kama lile la mwaka 2012 lililowahusisha Luis Suárez na Patrice Evra, ambapo Suárez alikataa kumpa mkono Evra baada ya kutumikia adhabu ya mechi nane kwa kumtukana kibaguzi.

Winga wa Real Madrid, Vinicius Jr akiwa katika mgogoro na nyota wa Benfica, Gianluca Prestianni wakati akidai kutolewa maneno ya kibaguzi katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya iliyopigwa Februari 17, 2026. Picha na Mtandao

Katika tukio la sasa, Vinicius alidai Prestianni alimwita “mono” (neno la Kihispania lenye maana ya tumbili). Hata hivyo, kiungo huyo wa Benfica alikanusha akidai kuwa maneno yake yalitafsiriwa vibaya, huku baadhi ya ripoti zikieleza alikiri kutumia kauli ya matusi yenye mlengo wa ushoga badala ya kibaguzi.

Mchezaji wa Madrid, Kylian Mbappé, alidai mwenzake alitukanwa mara kadhaa, wakati kiungo Aurélien Tchouaméni pia alinukuliwa akisema Prestianni alikiri kutumia kauli isiyofaa.

Kocha wa Benfica, Jose Mourinho wakati akijaribu kumtuliza nyota wa Real Madrid, Vinícius Júnior baada ya kulaumu kutolewa maneno ya kibaguzi katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya iliyopigwa Februari, 17 2026. Picha na Mtandao

Kocha wa Benfica, José Mourinho naye aliingia kwenye mjadala huo, akisema Vinicius alichochea hali kwa shangwe zake baada ya kufunga bao zuri. Kauli zake zilipingwa na wachambuzi akiwemo Clarence Seedorf, aliyesema si sahihi kuhalalisha ubaguzi kwa kisingizio cha uchochezi.

Mchezaji wa zamani wa Man United, Rio Ferdinand ambaye kwa sasa ni mchambuzi wa masuala ya soka. Picha na Mtandao

Ferdinand amtetea Mourinho

Ferdinand amesema anaamini Mourinho huenda alikosea namna ya kushughulikia suala hilo, lakini haamini kuwa kocha huyo ni mbaguzi.

“Naam, huenda baadaye atakaa na kusema alikosea namna ya kulizungumzia, lakini hilo halimfanyi kuwa mbaguzi,” amesema Ferdinand, akisisitiza kuwa Mourinho amewahi kuwasaidia na kuaminiwa na wachezaji wengi weusi katika taaluma yake.

Sasa macho yote yanaelekezwa kwenye uamuzi wa mwisho wa UEFA, huku Prestianni akiwa katika hatari ya kufungiwa hadi mechi 10 endapo atapatikana na hatia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *