Dar es Salaam. Kila mtu ana simulizi ya safari yake ya maisha, baadhi zikiwa zimejaa mitihani mikubwa na yenye kusisimua, lakini kwa mwimbaji maarufu wa muziki wa taarabu na dada wa gwiji wa miondoko hiyo nchini, Mzee Yusuf mambo hayakuwa magumu kivile kutokana na kutumia vyema kipaji na sauti aliyojaaliwa.

Khadija Yusuf, mmoja wa waimbaji wa kike wa taarabu wanaotamba na kuheshimika ndani na nje ya Tanzania. Anasema kujiamini kwake na kukitumia kipaji cha muziki alichokionyesha tangu utotoni sambamba na kujituma,  vimpa heshima na kumnufaisha kimaisha, kitu ambacho anataka wanawake wengine nao wasikate tamaa.

Anasema sio kama hajawahi kukumbana na changamoto, lakini kwake changamoto zilikuwa ni kama fursa ya kuzidi kusonga mbele. Katika fani yake ya muziki na mambo mengine nje ya muziki anayofanya kwa kujiamini kama mwanamke na moyo alionao wa kusaidia wengine, vimechangia kumfikisha alipo.

Akizungumza na Mwananchi, Khadija anasema katika safari yake ya maisha na muziki alikutana na changamoto, lakini hakuruhusu zimkatishe tamaa na ndio maana amepata mafanikio anayojivunia na kutumia sauti yake kuhamasisha wanawake wenzake kupambania ndoto zao.

Staa huyo wa nyimbo kama Mkuki kwa Nguruwe, Zilipendwa, Hamchoki Kusema, Mkondombwe, Nilijua Mtasema, Fisadi Kiwembe, Hayanifiki, Riziki Mwanzo wa Chuki na nyingine. Anasema alianza muziki akiwa mdogo na kukua taratibu akishirikiana na bendi mbalimbali za taarab zilizompa uzoefu wa kipekee wa uimbaji.

“Muziki nilianza kama sehemu ya maisha yangu, nilipokuwa mdogo niliupenda sana na sasa bahati nzuri nilipata sapoti kwa familia, licha ya changamoto kadhaa zilizokumbana nazo, lakini naendelea kuongeza bidii na kuwasaidia wengine wenye vipaji, ili kukamilisha ndoto zao,” anasema Khadija.

KHAD 04

UTHUBUTU ALIONAO

Kupitia safari yake ya muziki wa taarab, Khadija anasema amekabiliana na changamoto za tasnia kubadilika na uwepo wa ushindani kwa miondoko ya rusha roho, iliyobeba mtindo mpya wa taarabu. Lakini utayari wa kwenda na wakati na kutopenda kukata tamaa ulimbeba yeye na waimbaji wenzake wakongwe.

“Tasnia ya taarab inakabiliana na mtazamo wa jamii, ushindani mkubwa na baadhi ya wanamuziki wa kiume waliokuwa na nafasi kubwa, nililazimika kuthibitisha kuwa mwanamke anaweza kufanikisha ndoto zake,” anasema Khadija na kuongeza;

“Siku zote muziki unahitaji kipaji, uvumilivu na imani kwamba kwa kufanya kazi kwa bidii na kuendelea kujifunza, unaweza kufanikiwa zaidi na ndio maana nilipambana na sitaki kuishia hapa nilipo.”

KHAD 01

FURSA ALIZOTUMIA

Khadija anasema alitumia fursa ya kujaliwa sauti tamu na kipaji cha kuimba kujitengenezea umaarufu na manufaa mengine ya kimataifa, kiasi kwamba wala hajutii kuingia kwenye fani hiyo ambayo kwa miaka ya nyuma ilijengewa dhana mbaya na jamii hasa kwa watoto wa kike kwa kuhisiwa ni wahuni.

Anasema kupata nafasi ya kuyatumikia makundi makubwa ya muziki wa taarabu yaliyotamba miaka ya 2000 kama Zanzibar Stars, East African Melody, Jahazi Modern Taarab na mengine kulimuinua kiuchumi na kumpa jina kubwa na kuzoa mashabiki lukuki kiasi hata shughuli zake nje ya jukwaa la muziki zilisonga mbele.

“Fursa kubwa zaidi ni pale nilipoanza kufanya kazi na kaka’angu Mzee Yusuf, hapo ndipo nilikuza kipaji changu na kupata umaarufu miongoni mwa mashabiki wa muziki huo. Na kupitia kufanya kazi na bendi kubwa za taarabu, nilijifunza mengi na kupata mwanga wa jinsi muziki unavyoweza kuamsha hisia na kuleta mabadiliko makubwa,” anasema Khadija mwenye asili ya visiwani Zanzibar anayejishughulisha na ujasiriamali nje ya fani hiyo ya muziki.

KHAD 02

KUJITOA KWA JAMII

Khadija anasema baada ya muda mwingi wa kupambana kujitengenezea njina na kuonyesha njia kwa wengine wenye vipaji, amekuwa akijitoa kwa jamii kuanzia wasanii wenzake kwa kushirikiana nao na kusaidia vipaji vipya vyenye ndoto za kuja kutamba katika muziki huo na mwingine nchini.

“Sio kila jambo unalolifanya kwa watu ni lazima ulitangaze na kulianika hadharani, lakini nimekuwa nikisaidia wasanii chipukizi hasa wa kike kuhakikisha wanafanikisha ndoto zao na huku mie mwenyewe nikiendelea kushirikiana na wanamuziki wengine katika kukuza taarab.

“Pia nimekuwa nikihimiza wanaume na wanawake hasa mashabiki wa muziki huu kuchangia zaidi kwani bila ya wao tasnia haiwezi kwenda, msisitizo wangu ni kutaka kuona ubunifu na mshikamano miongoni mwa wasanii. Hii ni muhimu kwa maendeleo ya muziki wa taarab,” anasema.

Anasema anashukuru Mungu kwa kupata mafanikio kupitia muziki huo, ingawa bado hajaridhika kwani anaona ana nafasi ya kufanya makubwa zaidi mbele ya safari mradi awe na uhai na afya njema.

“Ni kweli, nimefanikiwa kuwa mmoja wa wasaniii wenye nyimbo mbalimbali zilizopokewa vizuri na mashabiki, umaarufu wangu umeniwezesha kufika sehemu mbalimbali, lakini kubwa ni kutaka kuona mashabiki wana thamini muziki huu,” anasema.

KHAD 03

NDOTO MPYA

Khadija anasema kitu anachotamani kwa sasa ni kuona muziki wa taarab ukiendelea kustawi na kuinuka kwa sura mpya zenye vipaji vichanga hasa vya wanawake, ili nao wasikike na kuendeleza gurudumu la muziki huo kwani bado una thamani na nafasi ya kukua kimataifa bila kupoteza utambulisho wake wa asili.

Khadija anatoa wito kwa wanawake akiwataka wawe wavumilivu, uthubutu na matumaini ya kufika katika ndoto wanazoziota kama alivyopambana yeye wakati anaibuka katika muziki.

“Wasikate tamaa au kujizuia, wachague ndoto zao, wafanye kazi kwa bidii na wasiruhusu vikwazo vipunguze malengo na thamani yako, mwanamke anaweza kushinda pale anapothubutu na kuonyesha kipaji chake bila kujali anakumbana na maneno gani kutoka kwa wanaomzunguka ambao wengi hukatisha tamaa,” anasema, Khadija ambaye ni mama wa mtoto mmoja wa kike, ambaye keshaolewa na kumletea mjukuu.

Kuhusu Siku ya Wanawake Duniani inayoadhimishwa kila Machi 8 ya mwaka, Khadija Yusuf anasema kwake anachukulia kama tukio la kukumbuka nguvu, ndoto na sauti ya mwanamke popote alipo kuinua wengine, kama anavyotumia muziki wa taarab kuinua jamii na kuhamasisha wengine kufuata ndoto bila kukata tamaa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *