Dar es Salaam. Kila mwaka maelfu ya wanafunzi wa vyuo vikuu na vya kati nchini humaliza masomo yao wakiwa na vyeti mikononi lakini mioyo ikiwa na maswali mazito wataingiaje kwenye soko la ajira bila uzoefu wa kazi?
Ndani ya vyuo, wanajifunza nadharia, nje ya lango la chuo waajiri wanataka vitendo na watu wenye uzoefu.
Katikati ya pengo hilo, kilio cha kukosa nafasi za mafunzo kwa vitendo kimekuwa kikiongezeka, huku waajiri nao wakitupia lawama kwa wanafunzi wakidai hawana ari ya kujifunza, nidhamu ya kazi na uelewa wa mahitaji halisi ya soko la ajira.
Mvutano huo umeendelea kwa miaka mingi, ukiacha maswali kuhusu nani ana wajibu mkubwa zaidi wa kumwandaa kijana wa Kitanzania kwa ulimwengu wa kazi.
Je, ni vyuo kubadili mitalaa? Ni waajiri kufungua milango ya viwanda na kampuni zao au ni wanafunzi wenyewe kubadili mtazamo na nidhamu ya kujifunza?
Kwa muda mrefu, wanafunzi wamekuwa wakilalamikia ugumu wa kupata maeneo ya mafunzo kwa vitendo, hali inayowalazimu wengine kumaliza masomo bila hata siku moja ya uzoefu wa kazi.
Wanasema hali hiyo inawaweka katika nafasi ngumu wanapoingia sokoni kutafuta ajira, ambako waajiri wengi huanza kwa swali moja: “Una uzoefu wa kazi wa miaka mingapi?”
“Mimi niliomba kwenye kampuni zaidi ya saba, nikapiga simu, nikatuma barua pepe, lakini sikupata majibu.
Wengine waliniambia wazi hawachukui wanafunzi wa mafunzo kwa vitendo,” anasimulia Neema Hassan, mwanafunzi wa mwaka wa tatu wa Shahada ya Uhasibu.
Anasema baadhi ya wenzake hulazimika kutumia mafunzo ya vitendo katika taasisi zisizoendana na taaluma zao, alimradi wapate alama za kukamilisha masomo.
Mwanafunzi wa mwaka wa nne wa Shahada ya Uhandisi wa Mitambo katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Abdulrahman Juma, anasema tatizo la ukosefu wa maeneo ya mafunzo kwa vitendo limekuwa sugu, kiasi cha kuwafanya wanafunzi wengi kumaliza masomo wakiwa hawajawahi kufanya kazi katika mazingira halisi ya taaluma zao.
“Unakuta umejifunza mashine kwa nadharia darasani, lakini hujawahi hata kuishika kiwandani. Unapomaliza chuo unaambiwa huna uzoefu, wakati mfumo wenyewe haukukupa nafasi ya kuupata,” anaeleza.
Mwanafunzi wa mwaka wa tatu wa Shahada ya Rasilimali Watu katika Chuo Kikuu cha Mzumbe, Janeth Maganga, anasema baadhi ya taasisi binafsi huweka masharti magumu kwa wanafunzi wa mafunzo kwa vitendo hali inayokatisha tamaa wengi.
“Taasisi nyingine zinataka ulipe ili upewe nafasi ya mafunzo. Mwanafunzi asiye na uwezo wa kifedha analazimika kutafuta mahali popote hata kama hakuhusiani na anachosoma,” anasema.
Naye Peter Mgaya, mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), anasema ugumu wa kupata maeneo ya mafunzo kwa vitendo, unachangia wahitimu wengi kukosa ujasiri wanapoingia sokoni.
“Unapoulizwa umefanya kazi wapi, unashindwa kuelezea kwa sababu hata mafunzo uliyofanya hayakuwa ya kitaalamu. Hili linapunguza nafasi zetu za kushindana na wengine,” anasema.
Mwanafunzi wa Shahada ya uuguzi, Agnes Mwakalinga, anasema kwa baadhi ya fani za afya, uhaba wa maeneo ya mafunzo huwalazimu wanafunzi kugawanywa kwa zamu au kusukumwa mbali na makazi yao, hali inayoongeza gharama za maisha.
“Unatumwa hospitali ya mbali bila maandalizi ya kutosha. Wengine wanashindwa kabisa kwenda kutokana na gharama, lakini bado wanatakiwa kutimiza matakwa ya chuo,” anasema.
Kwa upande wake, Hassan Mohamed, mwanafunzi wa mwaka wa pili Taasisi ya Usimamizi wa Biashara (IFM), anasema wakati mwingine vyuo huacha mzigo mzito kwa wanafunzi binafsi badala ya kuwa na mikataba rasmi na taasisi au kampuni.
“Kama chuo kingekuwa na makubaliano ya moja kwa moja na kampuni, sisi wanafunzi tusingepitia usumbufu huu wote. Mfumo wa sasa unatufanya tuonekane tunaomba msaada badala ya haki yetu ya kujifunza kwa vitendo,” anasema.
Wakati wanafunzi wakieleza hivyo kwa upande wa waajiri, simulizi ni tofauti, wenyewe wanasema wanasema changamoto si uhaba wa nafasi pekee, bali pia tabia ya baadhi ya wanafunzi wanaopelekwa mafunzoni kukosa nidhamu, kuchelewa kazini, kutokuwa tayari kujifunza kuanzia chini na kutegemea zaidi nadharia walizofundishwa darasani.
“Unamchukua mwanafunzi unamfundisha kwa gharama zako, halafu anakaa kwenye simu au anaona kazi ndogo ndogo hazimhusu. Hili nalo ni tatizo,” anasema mmoja wa mameneja rasilimali watu ambaye hakutaka jina lake linukuliwe.
Bado wapo waajiri wanaoona kutoa mafunzo kwa vitendo ni kupoteza muda hivyo wanaishia kukataa kuwachukua wanafunzi.
Mwelekeo mpya
Februari 9, 2026, ulifanyika uzinduzi wa mpango wa pamoja wa ushirikiano kati ya vyuo na viwanda wenye lengo la kukuza ujuzi na ajira kwa wahitimu wa ngazi mbalimbali za vyuo vya kati na vyuo vikuu.
Uzinduzi huo uliwaleta pamoja wadau wa elimu, ajira na uzalishaji, ambao kwa pamoja walikiri kuwepo kwa pengo kubwa kati ya elimu inayotolewa vyuoni na mahitaji ya soko la ajira.
Wadau hao wanasema mpango huo mpya wa Serikali, endapo utatekelezwa kwa ukamilifu na ufanisi, una uwezo wa kufungua milango ya ajira, kuimarisha ujuzi wa vijana na kuchochea ukuaji wa uchumi wa Taifa.
Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (Must) Yohana Lucas akiwa kama kiongozi wa serikali ya wanafunzi, anakiri kupokea malalamiko ya wanafunzi wenzake wengi wanaokataliwa nafasi za kujifunza kwa vitendo.
Anasema bado wapo waajiri wanaoona kutoa mafunzo kwa vitendo ni kupoteza muda hivyo wanaishia kukataa kuwachukua wanafunzi.
“Hali hii inatukatisha tamaa. Tunaamini mpango huu wa Serikali utakwenda kulazimisha ushirikiano na kutupa fursa zaidi za kujifunza,” anaeleza.
Mkurugenzi wa kampuni ya Emirate Aluminium & Glass Co Ltd, Deogratius Marandu, anasema kwa muda mrefu viwanda vimekuwa vikibeba mzigo wa kuwafundisha wafanyakazi wapya kutokana na mitalaa ya vyuoni kutogusa kikamilifu mahitaji ya uzalishaji.
“Hakuna mtalaa unaofundisha kuhusu aluminium. Inatulazimu kuwafundisha tunaowaajiri kuanzia mwanzo, jambo linalotupotezea muda na gharama,” anasema Marandu. Anaeleza kuwa baada ya kuona changamoto hiyo, kampuni yake iliingia ushirikiano na Veta ili vijana wafundishwe kwanza ujuzi wa vitendo, kisha wachukuliwe viwandani.
Anasema mpango huo wa Serikali ukitekelezwa ipasavyo, utapunguza gharama kwa waajiri, kuondoa malalamiko ya pande zote na kuongeza tija kazini.
Kwa upande wake, mmiliki wa viwanda vya sukari vya Kagera na Mtibwa, Seif Seif, anasema viwanda vinahitaji zaidi ya vyeti kwa kile alichoeleza kuwa vinahitaji wahitimu wenye nidhamu, moyo wa kujifunza na uelewa wa kazi kwa vitendo.
Anasema kampuni yake imekuwa ikichukua wanafunzi kutoka vyuoni, kuwapa mafunzo maalumu na baadaye kuwaajiri wale wanaoonyesha uwezo na bidii.
“Tungependa kufanya hili kwa ukubwa zaidi, lakini hilo litawezekana endapo tutawekewa mazingira wezeshi na rafiki. Uwekezaji kwenye rasilimali watu ni jambo la lazima kama tunataka viwanda vyetu viwe shindani,” anasema.
Naye Ofisa Mtendaji Mkuu wa Tanzania Startup Association (TSA), Zahor Muhaji, anasema mafanikio ya mpango wa ushirikiano yatategemea kwa kiasi kikubwa motisha kwa sekta binafsi. Anaeleza kuwa waajiri wengi wanatambua umuhimu wa mafunzo kwa vitendo, lakini gharama na muda vinawafanya wasite.
“Kama mwajiri akiwekeza fedha zake kutoa mafunzo kwa vitendo, apewe nafuu ya kodi. Hii itawahamasisha wengi kufungua milango yao kwa wanafunzi,” anasema na kuongeza pia walimu wa vyuo wanapaswa kwenda kujifunza kwenye tasnia ili waelewe mahitaji halisi ya soko, badala ya kufundisha nadharia pekee kwa miaka yote.
Hata hivyo, wapo wanafunzi waliopata fursa na kuona matunda yake. Amina Jerome, mhitimu wa Chuo Kikuu cha Kilimo (SUA), ni miongoni mwa wanufaika wa ushirikiano kati ya vyuo na viwanda.
Anasema Mtibwa Sugar iliwachukua wanafunzi na kuwapa mafunzo ya vitendo yaliyomwezesha kubobea katika kilimo cha miwa na hatimaye kupata ajira.
“Nilibahatika kupata nafasi hii. Nawashauri vijana wenzangu tutumie vizuri fursa za mafunzo kwa vitendo. Uzembe wa mtu mmoja unaweza kuwanyima wengine nafasi baadaye,” anasema.
Msimamo wa Serikali
Makamu wa Rais Dk Emmanuel Nchimbi anasema ushirikiano kati ya taasisi za elimu na viwanda, si hiari bali ni hitaji la lazima katika dunia ya sasa.
Anasema kuwa vyuo haviwezi kubaki kuwa visiwa vya nadharia na viwanda haviwezi kukua bila nguvu kazi yenye ujuzi unaoendana na soko.
“Katika dunia ya leo vyuo haviwezi kubaki kuwa visiwa vya nadharia na viwanda haviwezi kukua bila nguvu kazi yenye ujuzi wa soko. Sekta ya viwanda inategemewa sana katika mapitio ya mitalaa, utoaji wa mafunzo kwa vitendo, uanagenzi na kusaidia ujuzi unaohitajika sasa na baadaye,”anasema.
Kufainikisha hilo Dk Nchimbi anaelekeza sekta binafsi kushirikiana na vyuo kuwekeza kwenye tafiti hususani za kisayansi na teknolojia pamoja na kuhimiza ubunifu na ujifunzaji.