Dar es Salaam. Katika kudhibiti bidhaa bandia, Tume ya Ushindani (FCC) imeanza kutumia mfumo wa ukaguzi wa bidhaa wa pamoja (Tanoga), unaofanya kazi kwa ushirikiano na mamlaka nyingine za Serikali.

Kaimu Mkurugenzi wa Uthibiti wa Bidhaa Bandia wa FCC, Salvator Chuwa, amesema kuwa lengo la kuingia kwenye mfumo huo wa kidijitali ni kurahisisha shughuli za ukaguzi wa bidhaa na kuhakikisha Tanzania inakuwa na mazingira rafiki ya biashara, huku wamiliki wa nembo za bidhaa wakipata thamani halisi ya uwekezaji wao.

Amesema lengo lingine ni kuhakikisha walaji wanalindwa ili wawe wanapata thamani halisi ya bidhaa wanazotumia na zenye kukidhi matarajio yao.

“Utekelezaji wetu unategemea mfumo wa kidijitali unaotambua mizigo yenye vihatarishi kwa kutumia Tanoga, ambapo kibali cha forodha hutolewa tu baada ya ukaguzi na idhini ya FCC,” amesema Chuwa kwenye semina ya wahariri iliyofanyika Februari 23, 2026.

Pia ameeleza kuwa tume hiyo imeanzisha Daftari la Kielektroniki la Alama za Biashara linalowezesha wakaguzi kuthibitisha papo kwa papo uhalali wa alama za biashara, nchi iliyotengeneza bidhaa pamoja na wazalishaji walioidhinishwa kabla ya bidhaa kuruhusiwa kuingia sokoni.

Kwa mujibu wa Chuwa, bidhaa zenye shaka huzuiliwa mara moja na notisi za ukamataji kutolewa, huku wahusika wakikabiliwa na adhabu ikiwemo faini, kutaifisha na kuharibu bidhaa bandia.

Chuwa amesema wamiliki wa alama za biashara wanatakiwa kuwasilisha maombi FCC pamoja na nyaraka husika, ambapo Mkaguzi Mkuu hupitia ndani ya siku 21 kabla ya kuidhinisha au kukataa, na alama zilizoidhinishwa huingizwa katika daftari rasmi.

Hata hivyo, ameeleza changamoto zinazojitokeza ni pamoja na uelewa mdogo kwa baadhi ya waagizaji na wafanyabiashara wadogo kuhusu mchakato wa kurekodi alama za biashara, utegemezi wa mifumo ya kidijitali pamoja na uwezekano wa wafanyabiashara haramu kutumia njia zisizo rasmi za mipakani.

“Mpango huu una faida kubwa kwa taifa. Unalinda usalama wa watumiaji, unaimarisha ushindani wa haki kwa biashara halali, unaongeza mapato ya serikali kwa kupunguza ukwepaji kodi na unaongeza imani kwa wawekezaji,” amesema Chuwa.

Ameongeza kuwa FCC inaendelea na utekelezaji wa miradi miwili mikubwa ya kidijitali ambayo ni Daftari la Kielektroniki la Alama za Biashara na Tovuti ya Maombi ya Alama za Biashara itakayorahisisha uwasilishaji, mapitio na uhuishaji wa maombi kwa njia ya mtandao.

Awali, Kaimu Mkurugenzi wa FCC, Khadija Ngasongwa amesema tume hiyo imeshafanya marekebisho ya sheria ili kufikia dhamira ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kufungua milango kwa wawekezaji na kukuza Biashara.

“Tumefanya marekebisho ya sheria kama alivyosema mheshimiwa Rais kwamba, tufungue milango kwa wawekezaji na kukuza biashara,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *