Arusha. Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu (AfCHPR) imemchagua Jaji Blaise Tchikaya wa Jamhuri ya Congo (Brazzaville) kuwa rais mpya wa taasisi hiyo ya haki barani Afrika, akimrithi mtangulizi wake, Jaji Dk Modibo Sacko.

Jaji Blaise Tchikaya amechaguliwa leo Februari 24, 2026 na jopo la majaji 11 wa mahakama hiyo katika uchaguzi uliofanyika ndani ya mahakama hiyo jijini Arusha.

Akizungumza baada ya kuchaguliwa, Jaji Tchikaya amesema hiyo ni heshima kubwa lakini pia ni wajibu mzito ambao anaahidi kuutendea haki.

“Ninachukua jukumu hili nikiwa na dhamira ya dhati ya kulinda na kutekeleza mamlaka ya Mahakama hii na kuendelea kuipa heshima taasisi inayotegemewa kutoa haki za pande zote za wadai na wadaiwa,” amesema.

Uchaguzi wa Jaji huyo unakuja katika wakati ambapo Mahakama ikijiandaa kuadhimisha miaka 20 tangu kuanzishwa kwake.

Hata hivyo, wadau wanatazama maadhimisho hayo kama fursa ya kuimarisha misingi ya kisheria, kuongeza ufanisi wa taasisi na kuthibitisha nafasi ya Mahakama katika mfumo wa ulinzi wa haki za binadamu barani Afrika.

Akizungumzia hilo, Jaji Tchikaya amesema anatarajia kushirikiana na majaji waliopo kuthamini umri wa mahakama hiyo lakini pia kushughulikia changamoto zote zinazojitokeza.

“Tunapojiandaa kwa uzinduzi wa maadhimisho ya miaka 20 ya Mahakama, ninatarajia kushirikiana kwa karibu na majaji wenzangu, Msajili, watumishi na wadau wote kutathmini mafanikio ya Mahakama na kukabiliana na changamoto zilizopo.”

“Haya yote yatakwenda sambamba huku tukiimarisha zaidi nafasi ya taasisi hii katika kulinda haki za binadamu na watu barani Afrika,” amesema.

Katika hotuba yake ya kuaga kama rais, Jaji Sacko ametoa shukurani za dhati kwa majaji wenzake, msajili, watumishi na wadau wote kwa ushirikiano wao katika kipindi cha uongozi wake.

“Hii ni taasisi, ushirikiano uleule mlionipa kuendesha mahakama hii katika kipindi changu ndio huohuo natarajia tumpe rais mpya ili kuhakikisha taasisi hii inayotegemewa kwa haki Afrika inaendelea na kusimama vilivyo,” amesema.

Uongozi mpya wa Mahakama sasa unaundwa na Jaji Blaise Tchikaya kama rais na Lady Justice Bensaoula Chafika wa Algeria kama Makamu wa Rais.

Jaji Tchikaya ni nani

Jaji Tchikaya ana uzoefu mpana katika sheria ya umma ya kimataifa na haki za binadamu.

Awali, aliwahi kuchaguliwa kuwa Jaji wa Mahakama ya Afrika Julai 2018 kwa muhula wa miaka sita na aliwahi kuwa Makamu wa rais wa Mahakama kuanzia Juni 2021 hadi Julai 2023.

Pia, ni Profesa na Mhadhiri Mwandamizi wa sheria ya umma ya kimataifa, taratibu za mashauri ya kimataifa na sheria za haki za binadamu, akiwa amefundisha katika vyuo vikuu barani Ulaya, Karibiani na Afrika.

Jaji Tchikaya, pia, amesoma katika Chuo Kikuu cha Marien N’Gouabi, Brazzaville kabla ya kuendelea na masomo ya juu nchini Ufaransa, ambako alipata Stashahada ya Masomo ya Juu (DEA) katika Sheria ya Umma na baadaye Shahada ya Uzamivu (PhD) katika Sheria ya Umma ya Kimataifa kwa daraja la juu kutoka Chuo Kikuu cha Paris X-Nanterre chini ya usimamizi wa Profesa Alain Pellet.

Katika taaluma yake, aliwahi pia kuwa mjumbe na rais wa kwanza wa Tume ya Umoja wa Afrika ya Sheria ya Kimataifa (AUCIL), ambako alisimamia kuanzishwa na uendeshaji wa chombo hicho cha bara.

Zaidi Jaji Tchikaya ameandika na kuchapisha vitabu na makala nyingi katika eneo la sheria ya umma ya kimataifa, ikiwemo International Law Jurisprudence 1922–2015 na African Union Law: Principles, Institutions and Jurisprudence.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *