Arusha. Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba, ametoa onyo kwa baadhi ya watumishi wa umma wanaojihusisha na tabia ya kukodisha maduka au vizimba kwa wafanyabiashara kwenye masoko, kinyume na utaratibu.

Ameagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Arusha kusimamia sensa ya wafanyabiashara waliokuwa na vizimba katika soko la Kilombero, ili ujenzi utakapokamilika wapewe kipaumbele cha kwanza.

Dk Mwigulu ametoa maagizo hayo leo Jumanne, Februari 24, 2026, alipozungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika eneo la Kilombero, baada ya kuweka jiwe la msingi la mradi wa ujenzi wa soko hilo.

Amesema miongoni mwa maeneo yanayohitaji hatua za haraka ni pamoja na hayo, na kwamba kipaumbele kinapaswa kutolewa kwa wafanyabiashara waliokuwa wakifanya biashara katika soko hilo kabla ya ujenzi unaoendelea hivi sasa.

“Angalizo au tahadhari hatutarajii vizimba vichukuliwe na watu wasiofanya biashara, ambao baadaye huwakodishia wanaofanya biashara. Vizimba hivyo wapewe watu wanaofanya biashara, haihitaji mtu kati.

“Mkurugenzi wa Jiji, watumishi wa Serikali hawafanyi biashara, hatutarajii wao ndiyo washikilie maeneo haya. Ifanyike sensa kama soko la zamani walivyoshika, sasa wafanyabiashara wenyewe wapate maeneo hayo.

 “Hapa ni soko la wafanyabiashara, wapewe wanaofanya biashara, siyo mtu kati amkodishie mwingine. Huo ni wizi kama wizi mwingine, turidhike na tunachopata. Mfanyabiashara akifungua aliyekukodishia siyo Serikali, na tukigundua ni mtumishi wa umma, atakuwa amepoteza kazi yake,” amesema.

Awali, alikagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa stendi kuu ya mabasi yaendayo mikoani unaotekelezwa katika eneo la Bondeni City, Halmashauri ya Jiji la Arusha, unaogharimu Sh14.3 bilioni, uliolengo la kuboresha miundombinu ya usafiri, safirishaji, na kupunguza msongamano katikati ya jiji.

Baada ya ukaguzi, Dk Nchemba amesema ameridhishwa na hatua zinazofanywa, lakini wanatakiwa kuharakisha mradi ili kufidia muda uliochelewa. Kufuatia majadiliano ya kurekebisha muda, wayamalize mapema yasije kukwamisha mradi, makadirio yatakayokubaliana yaweze kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati.

“Nimeona jinsi ambavyo imepangwa, na jiji la Arusha liko bize, la kitalii, la kibiashara, na mwaka ujao kuna mashindano makubwa ya Afcon. Tu harakishe mambo yanayohusisha miundombinu, kwani stendi inayotumika sasa pamebanana na mji unazidi kukua,” amesema.

RC na mgogoro

Awali, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Amos Makalla, amesema miradi yote ya kimkakati iliyopangwa watashirikiana kusimamia na kuhakikisha inakamilika kwa wakati.

Kabla ya kumkaribisha Dk Mwigulu, Makalla ameomba kuwasilisha kero mbili za mkoa, akibainisha kwamba wasipozisema yeye na mkuu wa wilaya watakuwa hawajawajibika.

Kero ya kwanza, amesema Dk Mwigulu amemtumia ujumbe mfupi wa maandishi na kuhusiana na mgogoro wa wenye maduka na wamachinga ambapo amezungukia maeneo yote ya masoko yaliyotengwa kwa ajili ya wamachinga hao na kutafuta suluhisho.

“Katika kuzunguka huko, nimebaini baadhi ya maeneo wamachinga waliyopewa siyo rafiki kwa biashara zao. Ndiyo maana hiyo nilimwelekeza mkuu wa wilaya na mkurugenzi wa jiji, tuboreshe masoko hayo na katika soko hili la Kilombero niliwaambia likikamilika, kipaumbele ni kwa waliokuwepo,” amesema.

Kero ya pili, ametaja ni kile kinachoitwa mgogoro wa wenye maduka katika stendi ya zamani na kudai kuwa anafahamu suala hilo na viongozi wengine na kuwa limekuwa likikuzwa kama ni jambo kubwa lakini ametafuta nyaraka na kulichunguza suala hilo na kubaini hakuna mgogoro.

“Nimejiridhisha hakuna mgogoro pale, ule unakuzwa kwa maana ya watu mmoja mmoja na katika hili nataka nikuhakikishie Waziri Mkuu. George Simbachawene (akiwa Waziri) alikutana na wafanyabiashata waliojenga eneo hilo la jiji.

“Akawaelekeza na kuwapa miaka mitatu hadi 2020 baada ya hapo watatoka katika kuwa wajenzi na wawe wapangaji na nilipoona kelele zile nikasema serikali yetu ni tulivu msigombane nao.

“Baadhi ya wanaolalamika wanalipa jiji Sh250,000 na wenyewe wanapangisha kwa wafanyabiashara Sh1.5 milioni, kwa hiyo hapo lazima patokee tatizo. Lakini maduka haya wapo viongozi na wengine ni wabunge wa maeneo mengine sitaki kuwataja na hao ndiyo wanaoleta shida,” amesema.

Ameongeza kuwa: “Nataka nikuhakikishie hatuna mgogoro, mimi nataka utulivu, kuwe na maelewano hatua kwa hatua wasishtukizwe waelewe na wahakikishiwe watakuwa sehemu ya eneo hilo Serikali ina nia nzuri. Nisingesema hapa ningeonekana mimi sijawajibika,”

Ufadhili wa mradi

Awali, akiwasilisha taarifa ya ujenzi wa stendi hiyo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Arusha, John Kayombo ameeleza mradi huo unaotekelezwa chini ya Mradi wa Uboreshaji wa Miundombinu ya Miji (Tactics), unafadhiliwa na Benki ya Dunia.

Amesema mradi huo wa Sh14.3bilioni pamoja na miundombinu mingine utakuwa na nafasi za kukaa abiria 1,408  wanaosubiri usafiri wakati kwa mmoja, maeneo ya maegesho mabasi makubwa 42, madogo 24, taxi binafsi 22, bajaji 86, pikipiki 129 na miundombinu mingine ikiwemo maduka.

Amesema changamoto zilizokabili mradi huo kuwa ni awali eneo lililosanifiwa liligundulika kuingiliana na miundombinu ya umeme mkubwa, hivyo kulazimika kusogeza majengo upande mwingine.

Nyingine ni uwezo wa tabaka dogo lisilofaa ambapo kwa sasa maelekezo ya mhandisi mshauri ililazimu kutoa tabaka lote la juu kabla ya kuanza msingi na kuwa changamoto hizo na nyingine zimechelewesha mkandarasi kufikia malengo yake kwa asilimia 14 ambapo kwa sasa ameboresha na anafanya kazi usiku na mchana.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *