
Morogoro. Mvua zinazoendelea kunyesha zimeacha majonzi baada ya watu wawili kupoteza maisha na wengine wawili kujeruhiwa kwa kupigwa na radi Wilaya ya Kilombero, Mkoa wa Morogoro.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumanne, Februari 24, 2026, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Alex Mkama amesema tukio hilo limetokea usiku wa jana Jumatatu Februari 23,2026 katika kitongoji cha Mbesi, kijiji cha Utengule, Halmashauri ya Mlimba, wakati watu hao wakiwa njiani wakitoka matembezini.
Kamanda Mkama amesema radi hiyo iliwapiga ghafla wakati mvua kubwa ikiendelea kunyesha hali iliyosababisha vifo vya watu wawili papo hapo na wengine wawili kujeruhiwa.
Amewataja waliofariki dunia ni Tano Lunasi (36) na Ngimila Mashana (27), wote wakiwa ni wakulima na wakazi wa eneo la Mbesi huku majeruhi ni Manyanda Masasila (35) na Michael Msanga (28) wakulima na wakazi wa Mbesi ambao waliwahishwa hospitalini kwa ajili ya matibabu.
“Majeruhi walipatiwa matibabu na hali zao ziliendelea kuimarika, hivyo waliruhusiwa baada ya kupatiwa huduma,” amesema Kamanda Mkama.
Amesema Jeshi la Polisi linaendelea kufuatilia matukio yanayohusiana na athari za mvua katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo huku likiwataka wananchi kuchukua tahadhari za ziada ili kulinda usalama wa maisha yao.
Kamanda Mkama amewasihi wananchi kuepuka kutembea au kusafiri wakati mvua zikinyesha na badala yake kujisitiri katika maeneo salama.
“Tunawaomba wananchi wawe waangalifu zaidi katika kipindi hiki cha mvua, kwani madhara yake yanaweza kuwa makubwa ikiwemo kupoteza maisha,” amesema kamanda Mkama.
Jeshi la Polisi limesema litaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu namna ya kujilinda dhidi ya majanga yanayosababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa, huku likisisitiza umuhimu wa kuchukua tahadhari mapema.