
Mwendesha baiskeli rai awa Uholanzi, Jurgen Zomermaand, hapo jana alifanikiwa kushinda hatua ya 3 ya mashindano ya Tour du Rwanda kutoka kwenye mji wa Huye na kuishia Rusizi.
Imechapishwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Hatua hii ambayo ilikuwa na umbali wa kilometa 145, inatajwa kuwa moja ya hatua ngumu zaidi kwa waendesha baiskeli tangu kuanza kwa mbio hizi mwishoni mwa juma lililopita.
Akiendesha chini ya kampuni ya Riding for Development, Jurgen Zomermaand, alitumia muda wa saa 3 dakika 44 na sekunde 53.62, akimaliza kwa sekunde 20.36 zaidi mbele ya Mbelgiji Van Gils Lucas wa kampuni ya Lotto-Groupe Wanty.
Wengine waliofanikiwa kushika nafasi za juu kwenye hatua hiyo ni pamoja na:
1. Jurgen Zomermaand (Development Team Picnic PostNL) – 3h 44’53.62”
2. Van Gils Lucas (Lotto–Groupe Wanty) – +20.36”
3. Matteo Vanhuffel (Development Team Picnic PostNL) – +20.50”
4. Ribeiro Bravo (Soudal Quick-Step Devo Team) – +22.70”
5. Cisneros Diaz De Leon (Soudal Quick-Step Devo Team) – +28.22”
Katika hatua nyingine kocha wa timu ya waendesha baiskeli wa Rwanda, Felix Sempoma, amesema bado anaamini kuwa waendesha baiskeli wazawa watafanya vizuri licha ya kutoanza vema mashindano ya mwaka huu.
Felix amesema hata ikitokea kuwa hawatafanya vizuri, itakuwa wamejifunza na kupata uzoefu wa kutosha kwa ajili ya mashindano mengine ya baiskeli.
Mara ya mwisho kwa mwendesha baiskeli wa Rwanda kushinda hatua ya mashindano ya Tour du Rwanda tangu nchi hiyo ilipopandishwa hadhi na UCI, ilikuwa mwaka 2022, wakati Moise Mugisha aliposhinda hatua ya mwisho ya mashindano hayo.
Leo itakuwa ni hatua ya 4 kutoka mji wa Karongi kuelekea Rubavu, umbali wa kilometa 127.2.