
Utawala haramu wa Israel uliwaua wanahabari wasiopungua 84 mwaka wa 2025 – idadi kubwa zaidi kuliko dola lolote duniani katika mwaka uliokuwa mbaya zaidi kuwahi kurekodiwa kwa vyombo vya habari.
Hayo yamesemwa na Kamati ya Kuwalinda Waandishi wa Habari (CPJ) jana Jumatano katika ripoti yake ya kila mwaka na kuashiria “utamaduni endelevu wa kutokujali sheria wa jeshi la Israel, kwa kufanya mashambulizi ya kikatili dhidi ya wanahabari.”
Jumla ya wafanyakazi 129 wa vyombo vya habari waliuawa mwaka jana 2025, idadi kubwa zaidi kurekodiwa tangu kundi hilo la kutetea wanahabari lianze kunakili kumbukumbu mwaka wa 1992.
Kwa mujibu wa CPJ, utawala wa Kizayuni wa Israel ulihusika na zaidi ya theluthi mbili ya idadi ya vifo hivyo. Aghalabu ya wanahabari waliouawa na Israel walikuwa Wapalestina, lakini mashambulizi ya anga ya Israel pia yaliwaua wafanyakazi 31 katika ofisi za wanahabari wa Yemen, CPJ imesema.
Aidha kwa mujibu wa CPJ, mwaka 2024 ulikuwa mwaka mbaya pia katika historia iliyorekodiwa kwa waandishi wa habari waliouawa, ambapo utawala wa Israel uliua asilimia 70 ya waandishi wa habari 124 waliopoteza maisha mwaka huo.
Ripoti ya CPJ imesema “Huko Gaza na Lebanon, kumeshuhudiwa kesi ambapo waandishi wa habari waliuawa na jeshi la Israel, kinyume na sheria za kimataifa ambazo zinawatambulisha waandishi wa habari kama raia wakati wa vita.”
Hata hivyo, Ofisi ya Vyombo vya Habari vya Serikali ya Gaza inasema idadi ya waandishi wa habari waliouawa na utawala wa Israel ni kubwa zaidi ya takwimu za CPJ.