
Waziri Mkuu wa Senegal amependekeza sheria mpya itakayoongeza adhabu dhidi ya mahusiano ya jinsia moja, ambapo watakaopatikana na hatia wanaweza kuhukumiwa kifungo cha hadi miaka kumi jela.
Kwa sasa, mahusiano ya jinsia moja tayari ni kinyume cha sheria katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi na yanaadhibiwa kwa kifungo cha hadi miaka mitano. Katika hotuba yake mbele ya bunge wiki hii, Waziri Mkuu Ousmane Sonko amesema ushoga au mahusiano ya jinsia moja ni “vitendo kinyume na maumbile” na kusema kuwa wanaopinga msimamo huo “watakwenda kwa mabwana wao wa Magharibi” kupinga hatua za serikali dhidi ya LGBTQ.
Waziri Mkuu amewaambia wabunge kuwa muswada huo unapendekeza kuongeza kifungo cha jela kutoka miaka mitano hadi miaka kumi kwa watu wanaojihusisha na kile alichokiita “vitendo visivyo vya kawaida.”
Ameongeza kuwa endapo tendo hilo litahusisha mtoto mdogo, adhabu ya juu kabisa itatumika. Aidha, wahusika wanaweza pia kutozwa faini ya hadi faranga milioni 10 za CFA (takribani dola 17,953 za Kimarekani).
Kwa mujibu wa muswada huo, “uwakilishi wowote wa hadharani… unaolenga kuhamasisha mahusiano ya jinsia moja utaadhibiwa kwa kifungo cha miaka mitatu hadi saba jela na faini.”
Mapema mwezi huu, wanaume 12 walikamatwa na kushtakiwa kwa “vitendo kinyume na maumbile” pamoja na kusambaza VVU kwa makusudi.”
Mahusiano ya jinsia moja ni kosa la jinai katika nchi kadhaa za Afrika. Uganda ilikabiliwa na lawama kali kutoka nchi za Magharibi baada ya kupitisha sheria kali dhidi ya wanahusika na mahusiano ya jinsia moja mnamo Mei 2023, inayotoa adhabu ya kifo au kifungo cha hadi miaka 20 gerezani.
Marekani ilijibu kwa kuiwekea Uganda vikwazo na kuiondoa katika mpango muhimu wa biashara huria, huku Benki ya Dunia ikisitisha mikopo mipya. Uganda imeshikilia msimamo wake huo wa kutetea maadili ya Afrika.
Mwezi Septemba uliopita, wabunge wa Burkina Faso walipitisha sheria kuhusu ndoa na maadili ya kifamilia, ambayo kwa vitendo ilipiga marufuku mhusiano ya jinsia moja nchini humo.