
Awamu ya tatu ya mazungumzo ya kidiplomasia kuhusu mradi wa Nyuklia wa Iran, yamefanyika jijini Geneva nchini Uswiszi, kati ya wajumbe wa Marekani na Iran, wakati rais Donald Trump akitishia kuishambulia Tehran kijeshi iwapo mkataba hautapatikana.
Imechapishwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Mazungumzo haya yasiyo ya moja kwa moja, yanalenga kuzuia mzozo ambao huenda ukatokea iwapo pande zote hazitokubaliana.
Msuluhishi wa mzozo huo Waziri wa Mambo ya nje wa Oman Badr Albusaidi, amesema, pande zote zimeonesha nia ya kupata suluhu kuhusu mradi wa nyuklia wa Iran, ambao rais Trump anasema ni hatari kwa usalama wa Marekani na dunia.
Mazungumzo haya yanakuja, wakati huu Marekani ikionekana kujiandaa kuishambulia Iran baada ya kutuma vifaa vyake vya kijeshi, katika eneo la Mashariki ya Kati.
Licha ya rais Trump kusema, angependa kutatua changamoto hiyo kwa njia ya kidiplomasia, anafikiri pia kuishambulia Iran, kama njia ya kuipa shinikizo ya kupata suluhu.
Iran kwa upande wake, imesema iko tayari kujibu mashambulio ya Marekani, ikikanusha madai kuwa mradi wake wa kurutubisha madini ya Uranium unalenga kutengeza silaha za maangamizi ili kuishambulia Marekani na washirika wake kama Israeli.