
AWAMU hii Namungo imekataa uteja mbele ya Singida Black Stars, baada ya kutoka sare ya bao 1-1 katika mechi ya Ligi Kuu Bara iliyopigwa leo Februari 26, 2026 kwenye Uwanja wa Majaliwa uliyopo Ruangwa, mkoani Lindi.
Kipindi cha kwanza kilichomalizika kwa timu hizo kushindwa kufungana, Namungo ilipiga shuti moja golini, huku lingine likitoka nje wakati Singida haikulenga goli zaidi ya mashuti manne kutoka nje.
Kwa upande wa kona, kila timu ilipata mbili, Namungo ilifanya faulo nane, Singida sita na kwa asilimia kubwa Singida ilimiliki mchezo.
Kipindi cha pili, Singida ilionekana kushambulia zaidi ambapo dakika ya 58 ilipata bao la kuongoza lililofungwa kwa mkwaju wa penalti na mshambuliaji Elvis Rupia, hilo likiwa ni bao lake la pili Ligi Kuu Bara.
Namungo ikasawazisha dakika ya 90+1 kupitia mshambuliaji Fabrice Ngoy ambaye baada ya bao hilo kafikisha mabao manane na kuendelea kukaa kileleni mwa wanaoongoza chati ya ufungaji.
Tofauti na matokeo ya msimu wa 2024-2025, Oktoba 21, 2024, Namungo 2-3 Singida BS, mechi nyingine iliyopigwa Mei 16, 2025, Singida BS 1-0 Namungo na mechi ya leo Februari 26, 2026 Namungo 0-1 SBS.
Kwa matokeo hayo Singida BS imeendelea kusalia nafasi ya 10, katika mechi 10 ilizocheza, imeshinda nne, sare nne, imepoteza mbili, ina pointi 16 sawa na TRA United iliyopo nafasi ya 11 kwa utofauti wa mabao.
Kwa upande wa Namungo, imecheza mechi 16, imeshinda tano, sare sita, imepoteza sita, imefikisha pointi 21 inaishusha Mtibwa Sugar nafasi ya sita iliyolingana nayo pointi isipokuwa kwa utofauti wa mabao.