Dar es Salaam. Juni mwaka jana msanii wa Hip Hop, Country Wizzy alimtambulisha msanii mpya, Barbie Mia kwenye lebo yake ya I Am Music Co na kuwa msanii wa kwanza wa kike kusainiwa.

Tangu atambulishwe rasmi kama msanii wa kwanza wa kike wa Hip Hop chini ya lebo hiyo, Barbiemia ameanza kubeba matumaini makubwa ya mashabiki wa rap Bongo.

Barbie Mia anakuwa msanii wa pili wa kike wa Hip Hop kutambulishwa kwenye lebo, mwaka 2016 rapa Rosa Ree alijiunga na The Industry chini ya wasanii Navy Kenzo.

Kuwa msanii wa kwanza kusainiwa katika lebo sio jambo dogo unakuwa sura ya dira, nembo ya maono na kipimo cha mafanikio. Swali ni je? Barbie Mia anaweza kuweka historia mpya na hata kuvunja rekodi zilizowekwa na waliomtangulia?.

Barbie Mia sio jina jipya ni kwenye mitandao ya kijamii kwani hapo awali aliwahi kutrendi na kiki, kuna kipindi alikuwa anavuma na skendo ya kutoka na Diamond Platnumz mara Young Lunya.

Kwenye muziki sio mgeni kwani mwaka jana aliachia EP yake ya kwanza ya Life of Barbie zikiwa na ngoma nne kati ya hizo ‘Beatiful Girl’ aliyomshirikisha bosi wake ilifanya vizuri, ilikuwa na utofauti na ndivyo alivyojitambulisha tangu anaanza kurap.

Mwanadada huyo anafanya mziki fulani hivi laini yaani Hip hop ya kubembeleza sio muziki mgumu kama ulivyo muziki wenyewe yaani ameleta ladha tofauti kiasi cha hata baadhi ya wanawake kuanza kusikiliza.

Hivi karibuni ameachia kazi ‘Wasichana Wanachana’ wakishirikiana na wasanii wengine wa kike wa Hiphop wanaochipukia kwa kasi, Black Queen, Miss Rapper na Commender Rich.

Kazi hiyo imewaibua wasanii wengi hasa wa Hip hop kuona kwanza kolabo ya wasanii wa kike lakini pia uwezo mkubwa wa kuchana jambo lililowashtua wengi akiwemo rapa Frida Amani.

Barbie Mia anarudi katika tasnia wakati ambao Hip Hop ya Tanzania ipo katika mabadiliko makubwa. Wasanii wengi wamehamia katika mchanganyiko wa mitindo ili kufikia soko pana zaidi. Hivyo ujio wake kama rapa wa kike unakuja na matarajio ya kurejesha ushindani wa kweli katika rap ya wanawake.

Faida kubwa aliyonayo ni kuanza safari akiwa tayari ndani ya mfumo wa lebo. Hii ina maana ya uwekezaji wa moja kwa moja katika utambulisho, video, masoko na usimamizi wa kazi.

Lakini pamoja na faida hiyo, presha ni kubwa kila kazi atakayotoa itapimwa kwa jicho la tatu sio tu kama msanii binafsi, bali kwa lebo nzima.

ATAVUNJA REKODI?

Kuvunja rekodi katika muziki wa Hip Hop hakutegemei kipaji pekee, kunahitaji mkakati, Sauti na mtindo ni silaha kubwa. Ili kudumu, anapaswa kujitofautisha na waliomtangulia ajenge chapa yake na kwa hapa ameweza.

Mashabiki wanapenda msanii mwenye msimamo na maudhui yakitofauti. Ikiwa ataweza kujenga taswira ya rapa anayesimama katika ukweli na ubunifu, atakuwa na nafasi kubwa ya kushindana.

Kitu kinginie ni kwamba zama hizi za kidijitali, wimbo mmoja unaweza kumbeba msanii hadi kimataifa. Lakini pia wimbo dhaifu unaweza kumrudisha nyuma.

Hivyo, Barbiemia anahitaji nyimbo zenye ubora wa juu wa uandaaji, mashairi mazito na video zenye hadhi ya kimataifa.

Barbie Mia ni wa muda mrefu kidogo lakini kuibuka kwake tena kunamfanya ajiandae vilivyo hasa kimataifa anapaswa kufanya kolabo na wasanii wa nje, majukwaa ya kimataifa na matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii vitambeba wakati huu ambao ameibuka na moto.

INAWEZEKANA

Inaweza kuvunja rekodi bila kumtaja Rosa Ree ambaye anafanya vizuri kwa marapa wa kike. Rosa Ree aliweka historia kwa kushinda tuzo kadhaa za Hip Hop, ikiwemo TMA na EAEA mwaka 2022, na kuthibitisha kuwa msanii wa kike anaweza kushindana na wanaume katika rap.

Kama ilivyo kwa Barbie Mia ambaye alianza kusota kabla ya kusainiwa na lebo hiyo hata Rosa Ree alipata mafanikio hayo baada ya kujijenga kwa muda mrefu, nje ya lebo hivyo inawezekana kama ataamua.

Soko la muziki huo limekuwa pana, lakini pia limejaa ushindani. Wasanii wa kike sasa wana nafasi kubwa kuliko miaka ya nyuma. Hii ina maana kuwa Barbie Mia ameibuka tena wakati sahihi wakati ambao jamii imeanza kukubali na kuunga mkono rap ya wanawake kwa nguvu zaidi.

Hata hivyo, ushindani huo huo unaweza kuwa changamoto. Ili avunje rekodi, atalazimika kutoa kazi zitakazozungumzwa, si kwa siku moja bali kwa muda mrefu. Rekodi hazivunjwi kwa wimbo mmoja zinavunjwa kwa muendelezo wa kazi bora.

“Wakati naanza nilikuwa na picha ya muziki lakini sikupata muongozo mzuri kwenye tasnia ndio maana ilikuwa ngumu lakini Country Wizzy alikuwa ananifuatilia muda mrefu ndio maana niliposainiwa kuna vitu kidogo nilirahisishiwa,” anasema Mia

“Nimemfahamu Wizzy miaka 10 nyuma nikiwa na mtu wangu wa karibu na nimekuwa nikimsapoti kwa hiyo alivyonifuata nikasema acha nifanye kwa sababu kwa wakati huo nilikuwa nimeachana na Female Gang.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *