
Dar es salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imemfutia kesi na kumuachia huru, mshtakiwa Tumaini Moshi (33) aliyekuwa anakabiliwa na kesi ya unyang’anyi wa kutumia silaha baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini ( DPP), kutokuwa na nia ya kuendelea na mashtaka dhidi yake.
Mshtakiwa huyo alikuwa anakabiliwa na shtaka moja la unyang’anyi wa kutumia silaha na kujipatia vitu mbalimbali vyenye thamani ya Sh1.5 bilioni mali ya Klabu ya The Voice Tz Limited.
Uamuzi huo umetolewa leo Februari 27, 2026 na Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Ushindi Swallo baada ya Wakili wa Serikali, Bony Lawrence kuieleza Mahakama kuwa DPP amewasilisha hati ya kutokuwa na nia ya kuendelea na kesi dhidi ya mshtakiwa
Wakili Lawrence alidai kuwa, DPP amemfutia kesi hiyo ya jinai namba 28915 ya mwaka 2025 chini ya kifungu namba 92(1) cha Sheria ya Makosa ya Jinai, Sura ya 20 ilivyofanya marejeo mwaka 2023.
” Mheshimiwa hakimu, tunaitaarifu Mahakama hii kwa DPP hana nia ya kuendelea na kesi dhidi ya mshtakiwa wa kwanza katika kesi hii, Tumaini Moshi, ambaye alikuwa anakabiliwa na kesi ya unyang’anyi wa kutumia silaha” alidai Lawrence.
Hakimu Swallo alikubaliana na ombi hilo na kumwachia huru mshtakiwa huyo, chini ya kifungu hicho.
” Mahakama inakubaliana na ombi la upande wa Jamhuri kama lilivyowasilishwa, lakini kwa kifungu kilichotumika kuondoa kesi hii, Mahakama inakufahamisha kuwa Jamhuri wakiona kuna uhitaji wa kukushtaki basi watatumia kifungu hicho kukushtaki tena,” alisema Hakimu Swallo na kisha kumwachia huru.
Kwa mara ya kwanza Tumaini alifikishwa Mahakamani hapo Novemba 7, 2025 na kusomewa kesi ya uhaini yenye mashtaka mawili ya kula njama na kutenda kosa, kesi ambayo ilifutwa na DPP na kubaki na kesi moja ya unyang’anyi wa kutumia silaha.
Hata hivyo, Desemba 23, 2025, Tumaini na mwenzake Gasper Mmari(24) ambaye hajafutiwa kesi hiyo ya unyang’anyi walipandishwa Mahakama hapo na kusomewa shtaka moja la unyang’anyi wa kutumia silaha.
Hadi Tumaini anafutiwa kesi hiyo, Mahakama hiyo ilikuwa tayari imesikiliza shahidi mmoja wa upande wa Jamhuri, ambaye ni mlinzi wa Klabu hiyo, Masoud Hassan.
Hata hiyo, kwa upande wa mshtakiwa Mmari kesi yake itaendelea Machi 3, 2026 kwa ajili ya kuendelea na usikilozwaji.
Kesi ya msingi
Mshtakiwa anadaiwa Oktoba 29, 2025 eneo la Kinyerezi katika Klabu ya The Voice Tz Limited, yeye na mwenzake (Gasper Mmari) ambaye hajafutiwa kesi hiyo, walifanya unyang’anyi wa kutumia silaha kisha kuiba vitu vilivyokuwepo katika klabu hiyo.
Siku hiyo, Moshi na Mmari wanadaiwa kuiba viti 350 vya mbao na vya plastiki vikiwa na thamani ya Sh150 milioni.
Pia, wanadaiwa kuiba vifaa vya ofisi vikiwa na thamani ya Sh40 milioni.
Vile vile, waliiba runinga 57, zikiwa na thamani ya Sh480 milioni.
” Washtakiwa hao pia wanadaiwa kuiba Music System wenye thamani ya Sh250milion na POS mashine ikiwa na thamani ya Sh80milioni,” inadaiwa.
Inadaiwa pia waliiba vyombo vya jikoni nyenye thamani ya Sh25 milioni, vifaa vya baa vyenye thamani ya Sh15 milioni na vinywaji mbalimbali vyenye thamani ya Sh518 milion .
Mbali na kuiba vitu hivyo, washtakiwa hao wanadaiwa kuiba Sh16.9 milioni na kwamba vitu vyote vina thamani ya Sh1.5 bilioni, mali ya Klabu ya The Voice Tz Limited.
Hata hivyo, kabla ya kutekeleza wizi huo, washtakiwa hao waliwatishia kuwapiga kwa kutumia mawe, fimbo na nondo, watu watatu ambao ni Jammy Galus, Masoud Ahmed na Benedict Katarunga ili waweze kupata vitu hivyo bila kikwazo.
Hadi anafutiwa kesi hiyo, mshtakiwa huyo amekaa mahabusu kwa siku 111, ambazo ni sawa na miezi mitatu na siku 19 kutoka na kesi hiyo kutokuwa na dhamana kwa mujibu wa sheria.