
Dar es Salaam. Katika miaka ya hivi karibuni, mfumo wa familia umeendelea kubadilika kwa kasi kubwa. Wazazi wengi wanatumia muda mwingi kazini, watoto wanakua katika mazingira ya kidijitali, huku majukumu ya malezi yakizidi kuwa changamoto.
Katikati ya mabadiliko hayo, swali linalojitokeza ni kama nafasi ya babu na bibi katika malezi ya watoto bado ina nguvu kama ilivyokuwa zamani au imeanza kupotea.
Kwa miaka mingi, babu na bibi walikuwa nguzo muhimu katika familia. Mbali na kuwa walezi, walikuwa walimu wa maadili, washauri na wahifadhi wa mila na desturi.
Kupitia hadithi, methali na uzoefu wao wa maisha, walisaidia kuwajenga watoto kuwa watu wenye nidhamu, heshima na uwajibikaji.
Mtaalamu mmoja wa saikolojia aliwahi kusema kwamba, watoto wanaopata nafasi ya kuwa karibu na babu na bibi zao hupata faida kwa sababu hujifunza kutoka kwa watu wenye uzoefu mkubwa wa maisha.
Alisema uhusiano huo huwapa watoto hali ya usalama, utulivu na utambulisho wa kifamilia.
Hata hivyo, maisha ya kisasa yamebadilisha kwa kiasi kikubwa nafasi hiyo. Ukuaji wa miji, ajira zinazowalazimu watu kuhamia mbali na familia zao pamoja na kuongezeka kwa familia ndogo, umefanya babu na bibi wengi kuwa mbali na wajukuu wao. Na katika baadhi ya familia, watoto hukua bila kuwa na mawasiliano ya karibu na babu na bibi zao.
Lakini pamoja na mabadiliko haya tunayoendelea kuyashuhudia, mchango wa babu na bibi bado ni muhimu kuliko wakati mwingine wowote.
Kwa mujibu wa wataalamu wa malezi, watoto wanahitaji kuwa na watu wengi wanaowapenda na kuwaongoza, babu pamoja na bibi ni sehemu ya mtandao huo wa msaada unaochangia ukuaji wao.
Katika Tanzania na nchi nyingi za Afrika, bado kuna familia ambazo babu na bibi wanabeba jukumu kubwa la malezi.
Wapo wanaolea wajukuu wakati wazazi wanatafuta riziki mijini au nje ya nchi. Wengine hutoa msaada wa kila siku kwa kuwafundisha watoto maadili, lugha za asili na historia ya familia.
Faida nyingine kubwa ya uwepo wao ni uwezo wa kufundisha maadili kwa njia ya uzoefu. Tofauti na vitabu au mitandao ya kijamii, babu na bibi hufundisha kwa mifano halisi ya maisha waliyoishi.
Mara nyingi watoto huwasikiliza kwa makini kwa sababu huwatambua kama watu wenye hekima na uzoefu mkubwa.
Hata hivyo, wataalamu wanaonya kuwa mchango wa babu na bibi unapaswa kwenda sambamba na mabadiliko ya wakati.
Baadhi ya migongano hutokea pale wazee wanapotumia mbinu za malezi zilizopitwa na wakati au zinazokinzana na uamuzi wa wazazi. Hali hiyo inaweza kusababisha mkanganyiko kwa mtoto na hata migogoro ndani ya familia.
Nimesoma andiko moja la mtaalamu wa masuala ya familia, Profesa Karl Pillemer wa Chuo Kikuu cha Cornell nchini Marekani, anasema ushirikiano kati ya wazazi na babu pamoja na bibi ni muhimu ili kuhakikisha mtoto anapata malezi yenye mwelekeo mmoja. Profesa huyo anasema wazee wanapaswa kuheshimiwa kwa uzoefu wao, lakini pia wanahitaji kuelewa mazingira mapya ambayo watoto wa leo wanakulia.
Katika dunia ya teknolojia, baadhi ya watu huona kwamba simu, televisheni na mitandao ya kijamii imechukua nafasi iliyokuwa ikishikiliwa na wazee katika kuwafundisha watoto.
Hata hivyo, baadhi ya wazazi na hata wataalamu wengi hawakubaliani na mtazamo huo. Wanasema teknolojia inaweza kutoa taarifa, lakini haiwezi kuchukua nafasi ya upendo, ushauri wa moja kwa moja na hekima inayotokana na uzoefu wa maisha.
Kwa upande mwingine, watoto wanaokua bila kuwasikia babu na bibi zao mara nyingi hukosa fursa ya kujifunza historia ya familia zao. Utafiti mbalimbali unaonyesha watoto wanaofahamu historia ya familia zao huwa na uwezo mkubwa wa kukabiliana na changamoto za maisha kwa sababu wanajenga hisia ya kujiamini na kujitambua.
Kwa hiyo, ingawa mfumo wa maisha umebadilika, nafasi ya babu na bibi katika malezi haijapotea. Kilichobadilika ni namna ya kuitekeleza.
Leo hii wanaweza wasiwe karibu yaani ana kwa ana, lakini bado wana nafasi ya kushiriki malezi kupitia mawasiliano ya simu, ziara za kifamilia na ushauri kwa wazazi na watoto.
Kwa maana nyingine, familia za kisasa zinapaswa kutafuta njia za kuimarisha uhusiano kati ya watoto na babu pamoja na bibi zao.
Hii ni kwa sababu malezi bora hayajengwi na wazazi pekee, bali na familia nzima. Kadiri jamii inavyobadilika, ndivyo inavyokuwa muhimu zaidi kuhifadhi hazina ya hekima, maadili na uzoefu walionao wazee wetu.
Ni vema kila mzazi na mlezi akatambua kuwa mchango wa babu na bibi katika malezi bado una nguvu. Isipokuwa changamoto iliyopo si kupotea kwa nafasi yao, bali ni jinsi familia za leo zitakavyotumia kwa ufanisi hazina hiyo muhimu kwa ustawi wa kizazi cha sasa na kijacho.