Dar es Salaam. Kwa zaidi ya miongo miwili, jina la Beldina Nyakeke limekuwa sehemu ya sauti ya jamii ya Mkoa wa Mara.

Akiwa mwandishi wa habari wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Beldina ameitumia kalamu si tu kuripoti matukio, bali kama daraja la matumaini kwa jamii.

Katika mahojiano maalumu na mwandishi wa makala hii, Beldina anasema safari yake ya miaka 20 ya uandishi imejaa changamoto, uamuzi mgumu na ushuhuda wa nguvu ya habari katika kubadili maisha.

“Uandishi wa habari si kazi tu ya kuandika kinachotokea. Ni wajibu wa kuibua yale yanayopaswa kutokea,” anasema.

Akiwakilisha Mkoa wa Mara, Beldina anasema amekuwa karibu na jamii akisikiliza, akihoji na kuandika simulizi zinazogusa mioyo ya wasomaji.

Anaamini kuwa mwandishi wa habari anapokaa karibu na jamii, anakuwa shahidi wa changamoto na pia kiungo cha suluhisho.

“Nilitambua mapema kuwa ningeweza kuwa sauti ya wale ambao hawana pa kusemea. Na nilipoanza kuona makala zangu zikileta mabadiliko halisi, nikajua hii ndiyo njia yangu,” anaeleza.

Mwandishi wa habari wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Beldina Nyakeke (kulia) akizungumza na mmoja wa wafanyabishara wa chakula maarufu mama ntilie ikiwa ni sehemu ya kutekeleza majukumu yake ya kazi.

Moja ya makala zilizomgusa zaidi ni ya kijana yatima mwenye ulemavu kutoka Dodoma. Baada ya kufiwa na wazazi wake, kijana huyo alipata msaada wa msamaria mwema aliyempeleka Mwanza kwa ahadi ya kumsomesha.

Isivyo bahati, kabla ndoto hiyo haijaanza, msamaria huyo alipata ajali na kufariki dunia na matumaini ya kijana huyo yakazimika ghafla.

Akiwa hana msaada, alijikuta akiishi maisha ya mitaani. Alifika Musoma akitumaini kupata mwanzo mpya, lakini hali ilikuwa ngumu.

“Ulifika wakati kijana huyo analala njaa hata siku nne mfululizo,” anasema Beldina.

Bahati ilimwangukia alipokutana na bibi mmoja aliyemchukua kuishi naye licha ya maisha yake kuwa duni. Kupitia mpango wa Memkwa, kijana huyo alijiunga na masomo na kuonesha uwezo mkubwa darasani.

Changamoto ilikuwa ni mahitaji ya shule, hasa usafiri kutokana na hali yake ya ulemavu.

Kalamu iliyofungua milango

Beldina anasema aliandika makala kuhusu kijana huyo, si mara moja bali mfululizo, akifuatilia hatua kwa hatua maisha yake na mafanikio yake darasani.

Anasema alipojitokeza kufanya vizuri katika mtihani wa darasa la saba, makala nyingine zilifuata.

“Nilitaka jamii ione uwezo wake, si ulemavu wake,” anasema.

Mwitikio ulikuwa mkubwa, anasema wafadhili walijitokeza, wakagharamia masomo yake kuanzia sekondari hadi chuo kikuu, pamoja na matibabu yake.

“Leo, kijana huyo ni mtumishi wa Serikali akifanya kazi katika Ofisi ya Mganga Mkuu wa Wilaya ya Bahi, mkoani Dodoma,” anasema.

Ingawa bado anakumbana na changamoto za kimazingira kutokana na ulemavu wake, anasema amesimama kama ushuhuda hai wa nguvu ya habari.

“Huo ni ushindi si wangu peke yangu, bali wa jamii nzima iliyoguswa na kuamua kuchukua hatua,” anasema Beldina.

Mtoto aliyekunywa kemikali

Simulizi nyingine ya Beldina ni ya mtoto aliyekunywa maji yenye kemikali shuleni, tukio lililomfanya adhoofike kupita kiasi na kushindwa kula. Wazazi wake walishakata tamaa.

Beldina alipoandika makala ya kwanza kuhusu tukio hilo, anasema hakujua kuwa angeingia katika safari ndefu ya harakati za haki na tiba.

Anaeleza makala zilifuata, zikieleza hali ya mtoto huyo na changamoto za familia yake.

Kupitia uandishi huo, anasema mtoto huyo alipata matibabu katika hospitali mbalimbali, ikiwamo Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, baadaye alipelekwa nchini India kwa matibabu zaidi, hatimaye alipona na kurejea shuleni.

Lakini safari haikuishia hapo, anasema Mahakama iliamuru taasisi iliyomiliki shule kuwajibika kwa uzembe uliosababisha tukio hilo.

Beldina anasema aliitwa mahakamani kutoa ushahidi kuhusu makala zake na mchakato mzima wa habari.

“Ilikuwa mara ya kwanza kuitwa mahakamani kwa sababu ya kazi yangu. Nilihisi uzito wa jukumu la uandishi wa habari, pia nilihisi fahari kwa kusimama upande wa ukweli,” anasema.

Kuinua familia kupitia elimu

Katika moja ya makala zake, Beldina aliandika kuhusu kijana kutoka familia masikini aliyekuwa katika hatari ya kukatisha masomo kutokana na changamoto za kifedha. Makala hiyo iligusa wadau na ufadhili ukapatikana.

Kijana huyo alisoma hadi ngazi ya chuo cha kati. Mafanikio yake yalibadilisha mwelekeo wa familia nzima. Wazazi wake walipata hamasa ya kuboresha shughuli zao za kiuchumi na hatimaye kununua kiwanja kwa ajili ya ujenzi wa nyumba.

“Hapo ndipo unaona kuwa elimu ya mtoto mmoja inaweza kuwa mwanga wa familia nzima,” anasema Beldina.

Mafanikio binafsi

Safari ya miaka 20 haikuwa tu ya mafanikio kwa jamii, pia ya ukuaji binafsi. Kupitia kazi yake, Beldina amejenga mtandao mpana wa kitaaluma, akikutana na watu wenye ushawishi na wataalamu wa sekta mbalimbali.

Amefanikiwa pia kuanzisha biashara yake binafsi, ambayo imekuwa chanzo cha kipato na malezi ya familia.

Anaamini kuwa uandishi wa habari umempa si tu kipato, bali ujasiri wa kuthubutu na kupanua wigo wa ndoto zake.

“Uzoefu wa muda mrefu umenifundisha nidhamu, utafiti wa kina na uthubutu. Uandishi umenilea kama mtaalamu na kama binadamu,” anasema.

Uandishi ni wito

Kwa Beldina, uandishi wa habari si taaluma tu bali ni wito. Ni dhamira ya kusimama katikati ya jamii, kusikiliza vilio vya waliokata tamaa na kuviandika kwa uwajibikaji na weledi.

Anasisitiza kuwa mwandishi wa habari anapaswa kuwa na moyo wa huruma, pia misingi imara ya maadili.

“Unapoandika kuhusu maisha ya mtu, unagusa heshima na mustakabali wake. Lazima uwe mwangalifu, lakini pia jasiri,” anasema.

Anasema tabasamu la wale waliopata msaada kupitia makala zake, zinamtia moyo na kumpa hamasa ya kuendelea kuwa mwandishi wa habari.

“Kuona mtu aliyelala njaa leo akiwa na ajira au mtoto aliyekuwa kitandani leo akiwa darasani, hayo ni malipo makubwa kuliko chochote,” anasema Beldina.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *