Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres na wakuu wa mashirika ya Umoja huo wamelaani mashambulizi ya Marekani na Israeli dhidi ya Iran yaliyofanywa leo Jumamosi na yale ya kujibu kisasi yaliyotekelezwa na Iran dhidi ya Israeli na maeneo ya ghuba.

Mashambulizi dhidi ya Iran yanaripotiwa kulenga maeneo ya kijeshi pamoja na uongozi wa Iran. Vyombo vya habari vinasema milipuko imesikika huko Israeli na nchi za Ghuba baada ya Iran kufanya msururu wa mashambulizi kwa kutumia ndege zisizo na rubani au droni pamoja na makombora.

Taarifa iliyotolewa New York, Marekani hii leo na Msemaji wa Katibu Mkuu imemnukuu Guterres akitangaza kuwa mvutano wa kijeshi kwenye ukada huo unatwamisha amani na usalama duniani na amekumbusha kuwa “nchi zote lazima ziheshimu wajibu wao chini ya sheria ya kimataifa, ikiwemo Chata ya Umoja wa Mataifa, ambayo inazuia tishio la matumizi ya nguvu dhidi ya eneo huru la nchi au uhuru wa kisiasa wa taifa lolote lile, au kwa njia yoyote ile kinyume na Malengo ya Umoja wa Mataifa.”

Katibu Mkuu ametaka sitisho la haraka la uhasama na kuacha mwendelezo huo wa mvutano akionya kuwa “kushindwa kufanya hivyo kunahatarisha kupanuka kwa mzozo huo kikanda na madhara makubwa kwa raia na utulivu wa eneo zima.”

Shaka na shuku zozote kuhusu Iran zitatuliwe kwa mujibu wa Chata ya UN – Baerbock

Na kutoka kwa Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Annalena Baerbock kauli yake ni wazi kwamba analaani vikali kuongezeka kwa hatari kutoka na mvutano wa kijeshi huko Mashariki ya Kati, akionya kuwa hali hiyo inatishia amani na usalama wa kimataifa.

Taarifa iliyotolewa na msemaji wake inamnukuu akisema kwamba, “Chata ya Umoja wa Mataifa iko wazi kwamba nchi wanachama zinapaswa kusuluhisha migogoro yao kwa njia za amani na kujiepusha na vitisho au matumizi ya nguvu dhidi ya uhuru au mipaka ya nchi nyingine.”

Amesema kwamba wasiwasi ulioko kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran, shughuli zake za kikanda na madai ya ukiukwaji wa haki za binadamu lazima vishughulikiwe kwa mujibu wa Chata ya Umoja wa Mataifa na sheria za kimataifa na si vinginevyo.

Bi. Baerbock amezitaka Marekani, Israel na Iran kupunguza mvutano, kuepuka kuhusisha nchi jirani katika mgogoro huo, na kurejea kwenye diplomasia na mazungumzo.

Hatari ya uharibifu mkubwa usiofikirika

Kufuatia tukio la leo Jumamosi, viongozi waandamizi wa Umoja wa Mataifa nao wametoa kauli zao akiwemo Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Haki za Binadamu Volker Türk, ambaye kupitia ukurasa wa X amesema mabomu na makombora sio njia ya kumaliza tofauti bali “yanasababisha vifo, uharibifu na machungu kwa binadamu.” Amesema, “raia ndio wanaoishia kulipa gharama.”

Bwana Türk ametoa wito kwa pande zote kurejea katika mazungumzo ili kumaliza tofauti zao kwa mapana zaidi na kuepuka mzozo utakaosababisha vifo kwa raia na uharibifu mkubwa usiofikirika sio tu Iran bali ukanda mzima wa Mashariki ya Kati.

Mkurungenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya duniani, WHO, Dkt Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema kupitia taarifa yake ukurasa wa X kwamba amesema amesikitishwa sana na hali inayoendelea na amesihi viongozi kuchagua njia yenye changamoto ya mazungumzo badala ya njia ya hovyo ya uharibifu.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuwa na kikao cha dharura

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *