
Saa chache baada ya vyombo vya habari vya serikali ya Iran kuthibitisha Jumapili, Machi 1, kifo cha Ayatollah Ali Khamenei, jeshi la Israel limetangaza kuwa limezindua wimbi jipya la mashambulio “katikati mwa Tehran.”
Imechapishwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Israel inasema imeendeleza mashambulizi yake katika maeneo mbalimbali ya mji mkuu wa Iran, Tehran leo Jumapili Machi 1.
Milipuko yasikika juu ya Tel Aviv
Wakati huo ho Iran inaendelea kushambulia kambi za kijeshi za Marekani katika eneo hilo na nchini Israel, vyombo vya habari vya serikali vimeripoti, pia vikitaja vifo vya mkuu wa majeshi ya Iran, waziri wa ulinzi, mkuu wa Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu, mshauri wa Kiongozi Mkuu, na mkuu wa ujasusi.
Israel imewaua maafisa wakuu 40 wa Iran
Jeshi la Israel limesema leo Jumapili kuwa limewaua maafisa 40 wa ngazi za juu wa Iran, akiwemo Kiongozi Mkuu wa nchi hiyo, Ayatollah Ali Khamenei, katika shambulio lake la awali dhidi ya Iran siku ya Jumamosi: “Hatua ya kwanza ya operesheni hii ilikuwa shambulio la awali ambapo tuliwaangamiza maafisa 40 wa ngazi za juu, akiwemo Khamenei, katika dakika moja (…) mchana kweupe,” msemaji wa jeshi la Israel Luteni Kanali Nadav Shoshani amewaambia waandishi wa habari.
Kwa upande wake shirika la habari la serikali ya Iran, IRNA, likinukuu Hilali Nyekundu ya Iran, linaripoti kwamba mashambulizi 60 yamepigwa Tehran ndani ya kipindi cha saa 24, na kusababisha vifo 57.
Jeshi la Israel linasema limeharibu nusu ya akiba ya makombora ya Iran.
“Wakati wa operesheni hii, tuliharibu takriban nusu ya akiba ya makombora ya utawala wa Iran na kuzuia uzalishaji wa angalau makombora mapya 1,500,” Brigedia Jenerali Effie Defrin, msemaji wa jeshi la Israel, amesema katika hotuba iliyorushwa kwenye televisheni. “Hivi majuzi utawala huo ulitengeneza makombora mengi kwa mwezi mmoja na ulikusudia kuongeza uzalishaji wake hadi mamia kadhaa kwa mwezi.”