Vertex International Securities Limited imejipanga kutanua wigo wake Zaidi ya kuwa kampuni ya udalali kwenye soko la hisa na sasa inajielekeza kuwa ‘mjenzi kwenye soko’ katika kipindi ambacho masoko ya mitaji nchini yanaonesha dalili za kuingia awamu mpya ya upanuzi, yakichochewa na mageuzi ya kanuni, ukuaji wa ukwasi na kuongezeka kwa ushiriki wa wawekezaji.
Februari 27, 2026 kampuni hiyo iliandaa kongamano na kuwakutanisha viongozi wa sekta hiyo chini ya kaulimbiu “Kutoka Ustahimilivu hadi Upanuzi: Kuendeleza Soko la Mitaji la Tanzania kupitia Ubunifu na Ujumuishaji,” kutathmini utendaji wa mwaka 2025 na kujadili matarajio ya mwaka unaofuata.
Kongamano hilo la kila mwaka lililofanyika katika Hoteli ya Hyatt Regency, Dar es Salaam, liliwakutanisha watunga sera, mabenki, wasimamizi wa mifuko na wawekezaji.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Vertex International Securities Ltd, Mateja Mgeta, alisema kwa kuandaa tafakuri na majadiliano ya kila mwaka, Vertex inalenga kukuza utamaduni wa ushirikiano katika mfumo mzima wa kifedha, kuhakikisha ubunifu na ujumuishaji vinabaki kuwa kiini cha upanuzi wa soko la mitaji.
“Masoko ya mitaji yana jukumu kubwa katika kuhamasisha mtaji wa muda mrefu,” alisema.
Alibainisha kuwa mapitio ya 2025 yalilenga kuchambua viashiria vya utendaji pamoja na mageuzi ya kimuundo, huku yakitathmini namna soko linavyoweza kuchangia kwa ufanisi zaidi katika malengo ya maendeleo ya Tanzania.
Meneja wa Uendeshaji wa Vertex, Frank Kakwezi, aliwasilisha takwimu zinazoonesha kuwa jumla ya thamani ya mtaji wa soko ilipanda kwa asilimia 34 kutoka Sh17.9 trilioni mwishoni mwa 2024 hadi Sh23.99 trilioni kufikia Desemba 2025.
Mzunguko wa mauzo ya hisa uliongezeka kwa asilimia 190 katika kipindi hicho hicho, ishara si tu ya kupanda kwa thamani za hisa bali pia kuimarika kwa ukwasi.
Washiriki wa mkutano huo walieleza kuwa ukuaji huo umechangiwa na mabadiliko ya kanuni za biashara katika DSE, upanuzi wa majukwaa ya kidijitali na kuongezeka kwa uelewa wa uwekezaji miongoni mwa wananchi na taasisi.
Mkurugenzi wa Usimamizi na Uchunguzi wa Masoko wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), Exaud Julius (wa nne kushoto aliyeketi) ambaye pia ni mgeni rasmi na Afisa Mtendaji Mkuu wa Vertex International Securities Ltd, Mateja Mgeta (wa tatu kulia aliyeketi) wakifuatilia mjadala uliokuwa ukiendelea wakati wa kongamano la kutathmini utendaji wa mwaka 2025 wa soko la mitaji na kujadili matarajio ya mwaka unaofuata lililofanyika katika Hoteli ya Hyatt Regency, Dar es Salaam, February 27, 2026. Wengine ni wadau mbalimbali wa sekta ya fedha walioalikwa.
Miongoni mwa mageuzi yaliyotajwa ni marekebisho ya Kanuni ya 212, ambayo sasa inaweka mipaka ya mabadiliko ya bei kwa kuzingatia asilimia ya bei ya kufunga ya siku iliyopita, kulingana na ukubwa wa mtaji wa soko na idadi ya hisa za kampuni husika.
Hatua hiyo, pamoja na matumizi ya Bei ya Wastani Iliyopimwa kwa Kiasi cha Mauzo (VWAP) kama rejea ya bei ya kufunga, imetajwa kuongeza uwazi na uthabiti wa soko.
Mbali na hisa, mwaka 2025 pia ulishuhudia kuongezeka kwa uhitaji wa dhamana za Serikali.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Exodus Advisory, Ramadhan Kagwandi, alisema minada mingi ya dhamana ilipata maombi kupita kiasi, hali iliyosababisha ukwasi wa ziada kuelekezwa katika masoko ya hisa.
Hata hivyo, alisisitiza umuhimu wa kupanua wigo wa soko nje ya nchi na kwenye ukanda wa mashariki na kuanzisha bidhaa mpya ili kudumisha kasi ya ukuaji.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Fedha wa DSE, Lucas Sinkala, alisema idadi ya wawekezaji imeongezeka sambamba na kuanzishwa kwa bidhaa mpya, ikiwemo za Imani ya kiislamu ziitwazo Sukuk na majukwaa ya biashara kwa njia ya simu za mkononi.
Vertex pia ilitangaza kuzindua Mfuko wa Uwekezaji Vertex International Securities Exchange Traded Fund (Vertex-ETF) pamoja na Mfuko wa Hatifungani wa Vertex, hatua inayolenga kupanua chaguo za uwekezaji kwenye soko.
Mwenyekiti wa Bodi wa Vertex, Peter Machunde, alisema bidhaa hizo zitasaidia wawekezaji kupata uwekezaji uliotawanywa kwa gharama nafuu na kwa uwazi zaidi.
Katika mjadala wa taasisi, Mkurugenzi mtendaji wa Taasisi ya Mabenki Tanzania (TIOB), Patrick Mususa, alisema benki zina nafasi muhimu katika kukuza soko la hatifungani, lakini ushiriki bado ni mdogo kwani chini ya benki 10 kati ya takribani 40 zilizosajiliwa ndizo zinazofanya biashara ya hatifungani kwa kiwango kikubwa.
Kwa upande wa bima, Mtendaji Mkuu wa Jubilee Life Insurance Corporation of Tanzania Limited, Helena Mzena, alisema kampuni za bima zitaendelea kua mshiriki wa kimkakati kwenye masoko ya mitaji.
Akizungumza kwa niaba ya Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), Mkurugenzi wa Usimamizi na Uchunguzi wa Masoko, Exaud Julius, alisema mazingira ya sera na kanuni nchini yameimarika na kuweka msingi thabiti wa ubunifu huku yakilinda maslahi ya wawekezaji.
Alisema ongezeko la mzunguko wa mauzo na thamani ya miamala ni dalili ya kuimarika kwa imani ya wawekezaji katika soko la ndani.
Kwa ujumla, wadau walikubaliana kuwa masoko ya mitaji nchini yanaingia awamu ya upanuzi inayohitaji uwiano kati ya kasi ya ukuaji na tahadhari ya udhibiti.
Kwa Vertex, Mapitio ya Soko la Mitaji ya 2025 yamekuwa ishara ya dhamira yake ya kuwa zaidi ya kampuni ya udalali, bali mshirika wa kimkakati katika kujenga na kupanua soko la mitaji la Tanzania.